Subscribe:

Ads 468x60px

ASKARI WANYAMAPORI WATUHUMIWA KUZAMISHA NG’OMBE 51 MTONI NA WENGINE 100 KUPOTEA.


Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Mariwanda wilayani Bunda  Samson Kisung’uda

ASKARI WANYAMAPORI WATUHUMIWA KUZAMISHA NG’OMBE 51 MTONI NA WENGINE 100 KUPOTEA.
Juni 22,2013.
Mara-ASKARI  wa mapori ya akiba ya Ikorongo na Grumeti  kwa kushirikiana na Kampuni ya Singita Game Reserve ,wanatuhumiwa kusababisha vifo vya  ng’ombe 51na 100 kupotea wa mkazi mmoja wa Kijiji cha Mariwanda wilayani Bunda.
Tukio hilo linadaiwa kutokea aprili 22,majira ya saa 10.30 jioni mwaka huu katika eneo la Mto Rubana eneo la Mariwanda limethibitishwa na polisi na ofisi ya mifugo wilaya ya Bunda na uongozi wa kijiji hicho.
Kiteku Meshinya Kisereta mwenye mifugo akiongea na Mwandishi wa blog hii katika ofisi ya Wasaidizi wa Kisheria na Haki za Binadamu wilayani Serengeti (WASHEHABISE)alisema,chanzo cha vifo hivyo ni askari hao waliowakamata kwa kuingia hifadhini kuwasagwa na kuwazamisha mtoni ili wavuke na kufa 51,na wengine 100 hawajaonekana.
“Mizoga iliyoopolewa majini 51 na kuthibitishwa na polisi na ofisi ya mifugo…wengine 100 haijulikani walikopotelea..,siku hiyo nilitaarifiwa kupitia simu namba 0682 760012,0756 019672 na 0786 757603,kuwa ng’ombe wangu wamekamatwa na askari wa Grumeti nikalipe faini…wakati najiandaa kwenda nikataarifiwa na mchungaji wangu kuwa wamezamishwa mto Robana”alisema.
Alisema alilazimika kujulisha uongozi wa kijiji ,mkuu wa wilaya ya Bunda akamtuma Oc Cid ambapo walifika na kukuta ng’ombe 46 wamekufa maji,na aprili 24 walipata mizoga 5 na kufanya idadi ya 51,lakini wengine 100 haikujulikana wako wapi na hakuwahi kuwapata.
“Si mara ya kwanza ng’ombe wangu kukamatwa kutokana na shida ya maji wanajikuta wamevuka…askari hupiga simu ama wanasema tuma fedha ya faini kwa Mpesa…ukilipa wanaachiwa ingawa hawatoi stakabadhi….hata siku hiyo walinipigia niende na fedha,ajabu wakaamua kuwasukumia mtoni baada ya kuchelewa,”alisema kwa masikitiko.
Aliwataja askari waliohusika na tukio hilo kuwa ni Peter Gorobani na Juma Mwiyuga askari wa Kampuni ya Singita Grumeti Reserves,ambao walikuwa chini ya uongozi wa   Anthony Mamboleo wa Pori la Ikorongo ambaye yuko chini ya Mkurugenzi wa wanyamapori.
Serikali ya Kijiji 
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Mariwanda Samson Kisung’uda alisema tukio hilo ni mwendelezo wa Manyanyaso wanayopata wananchi dhidi ya mwekezaji na wizara,”wananchi wamefikia hatua mbaya maana hawa mwaka juzi walifukuza kijana aliyekuwa anachunga ng’ombe akazama mtoni akafa,hakuna hatua zilizochukuliwa dhidi ya wahusika”alisema.
Alisema mambo kama ya Mtwara huenda yakajitokeza kwa kuwa wananchi wanahasira na kampuni ya Singita Grumeti Reserves kutokana na vijana wake wanavyowatendea unyama wananchi,”sisi viongozi tunapata shida sana…siku hiyo ilikuwa wanaungana na vijiji vya jilani kwenda kuteketeza magari yao….tulitumia ushawishi kuwatuliza …kukaa kimya bila watakuja shangaa”alibainisha.
Kutokana na ukubwa wa tatizo waliwasiliana na Mbunge wa jimbo hilo Steven Wasira ambaye ni Waziri ofisi ya Rais Uhusiano na kuagiza kuandika barua kwenda kwa waziri wa Maliasili na Utalii ili aweze kuchukua hatua.
Barua hiyo ya mei 10,2013 imefafanua ilivyotokea na kunakilishwa kwa viongozi mbalimbali ,akiwemo mkuu wa mkoa wa Mara ,mbunge.Rpc,Dc na Ocd Bunda kwa Taarifa,hata hivyo hawajapata majibu kutoka wizara licha ya Mbunge wao kuwahakikishia kuwa alimkabidhi waziri mwenye dhamana.
Watuhumiwa.
Anthony Mamboleo askari wa pori la Ikorongo alipoulizwa kwa njia ya simu,alikiri kuwepo kwa tukio hilo,lakini hakutaka kulizungumzia”naomba umtafute kaimu meneja wa Ikorongo akupe taarifa zaidi”alisema na kukata simu.
Juma Mwiyuga(askari wa Singita Grumeti game reserves(VGS)alisema yeye alishatoa maelezo polisi ilivyotokea ,”kwanza nilikuwa post sikuwepo…lakini nilishatoa maelezo polisi…haya mambo mimi sipendi kuyazungumzia zaidi”alijibu.
Peter Gorobani alipoulizwa alisema hilo suala hawezi kulisemea mpaka afuatwe ofisini kwake atasema mambo mengi,alipoulizwa ofisi yake ilipo ili blog imtafute  akasema”sasa unataka kuja ofisini….aaah,kwaheri”akakata simu.
Kaimu Meneja Ikorongo.
Upendo Kimaro kaimu Meneja mapori ya akiba ya Ikorongo na Grumeti alipoulizwa kuhusu tukio hilo alikiri kuwepo lakini akasema kuna anayeshughulikia”sisi tunafanya kazi chini ya Kanda tunatoa taarifa Kikosi cha Kuzuia Ujangili (KDU)wanasema suala hilo liko Mahakamani tafuta katibu Mkuu ama Mkurugenzi wa wanyama pori watalisemea maana tunawashitaki sisi”alisema.
Hata hivyo suala hilo halijafikishwa mahakamani kama alivyodai meneja huyo ,alipotakiwa kueleza jalada lipi liko mahakamani kwa kuwa jalada la polisi BND/INQ/22/2013 lililofunguliwa na Meshinya dhidi yao halijafikishwa mahakamani,alisema”basi litakuwa polisi…maana nasi tuliwashitaki”alisema bila kutaja mashitaka hayo.
Mkurugenzi akana hana taarifa.
Mkurugenzi wa Wanyamapori Tanzania Alexander Songorwa alipoulizwa kwa njia ya simu kuhusu malalamiko ya mfugaji huyo alisema hana taarifa,”wewe ni Mwandishi wa pili ,juzi nimeulizwa kwa kweli sina taarifa nafuatilia nitajulisha kama kuna maandishi yoyote yameletwa na mtu wetu wa huko”alisema.
Hata hivyo alijibu kwa ujumbe mfupi wa simu(sms)kuwa hakuna taarifa iliyowahi wasilishwa kwake na maafisa wake kama walivyodai.
Ofisa Mifugo akiri.
Masuke Ogwa ofisa mifugo wilaya ya Bunda kupitia simu ya Mkurugenzi mtendaji halmashauri ya wilaya ya Bunda Simon Mayeye alikiri kushuhudia mizoga ya ng’ombe na kuwa walikufa maji,”mazingira yaliyopelekea wafe ni kazi ya polisi…lakini kwa ujumla nilishuhudia ng’ombe kama 51 au 52 wamekufa na ripoti ipo nitaikabidhi polisi “alisema
Singita.
Afisa mahusiano wa Kampuni ya Singita Grumet Game Reserves Shaabani Madanga alisema analifahamu suala hilo,na mlalamikaji amelifikisha kwa Waziri,”hata hivyo kwa huko linashughulikiwa na Ikorongo Game Reserves”alisema.
Wanaharakati.
Mwenyekiti mtendaji wa shirika la Wasaidizi wa Kisheria na Haki za Binadamu wilaya ya Serengeti Samweli Mewama alisema ,uwekezaji unaowatia umaskini wananchi huibua hasira na chuki na kuomba serikali kuchukua hatua ili mfugaji atendewe haki.
Mtandao wa wafugaji ,warina asali na waokota matunda(Ping’os)walisema wanafuatilia tukio hilo ili kuhakikisha mwananchi huyo anatendewa haki,kwa mazungumzo ama mahakamani.
Waziri
Juhudi za kumpata Waziri wa Maliasili na Utalii Khamisi Kaghasheki hazikuzaa matunda baada ya simu yake kuita bila kupokewa,na hata alipotumiwa maswali kutaka kujua hatua gani imechukuliwa,licha ya kupokelewa lakini hakujibu.
Matukio Mengine.
Blog hii  imebaini oktoba 8,2008 askari wa Ikorongo na Kampuni ya Singita Grumeti Reserve aliswaga ng’ombe kwa kutumia magari na kusababisha ng’ombe  65  mali ya Gorobani Marosina mkazi wa Issenye wenye thamani ya sh,24,600,000 kuzama Mto Robana na kufa na kuthibitishwa na Paulo Munkhoma Augustine afisa mifugo na taarifa yake yenye kumb.Na.Vy/a.20/1/30 kwenda kwa Dc ikionyesha tathimini aliyotakiwa kulipwa .
Hata hivyo licha ya Tathimini kuonyesha alivyostahili kulipwa kwa kuzingatia bei ya mnada wa mwezi huo ,mfugaji huyo alitishwa na uongozi wa wilaya kushitakiwa na kulipwa sh.mil.7.
Mwanzoni mwa Mwaka huu kampuni hiyo kwa staili hiyo ya kuswaga kwa kutumia magari walizamisha ng’ombe zaidi ya 40 mali ya mkazi wa Motukeri aliyejulikana kwa jina la Kijiji,naye alitishiwa na hakulipwa fidia .
Mwisho,ufuatiliaji unaendelea.

TAMKO LA MTANDAO WA WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU KWA WAZIRI WILLIAM LUKUVI NA HALI HALISI YA USALAMA MKOANI ARUSHA



 KAULI YA MTANDAO WA WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU KWA WAZIRI WILLIAM LUKUVI NA HALI YA USALAMA MKOANI ARUSHA TAREHE 19 JUNI 2013 Mtandao wa Wateteziwa Hakiza Binadamu unaounganisha asasi za kiraia zinazotetea haki za binadamu zaidi ya mia moja, pamoja na mashirika wananchama Mkoani Arusha, tumesikitishwa na kushtushwa sana na kauli iliyotolewana Waziriwa Nchi, Ofisiya Waziri Mkuu (Sera, Uratibuna Bunge) William Lukuvi dhidi ya asasi zakiraia.
Katika kauli yake Bungeni tarehe 17 mwezi Juni, akizungumzia tukio la bomu dhidi ya wafuasi wa Chama cha Demokrasiana Maendeleo (CHADEMA), Lukuvi ameendeleza kile ambacho kwa muda mrefu serikalii liyopo madarakani imekuwa ikikifanya yaani kutumia lugha mbaya za kuwachonganisha wateteziwa haki za binadamu na asasi za kiraia kwa ujumla na kuwaita kwamba ni wachochezi, vibaraka wa upinzani na lugha nyingine zenye dhihaka.
“Katika siku za karibuni, zimekuwepo jitihada za makusudi za baadhi ya vyama vya siasa, makundi ya kijamii na watu binafsi kupandikiza chuki kwa raia dhidi ya vijana wetu wa Jeshi la Polisi, kuwafanya raia wawachukie askari, kuwafanya raia wasiwaamini askari, kuwafanya raia wasiwape ushirikiano askari na hatimaye kuwa na taifa ambalo halitawaliki,” alisema Lukuvi
Kauli kama hii kutolewa kiongozi mkubwa wa serikali tena katika Bunge la Tanzania ni kejeli kwa waliopoteza ndugu zao Mjini Arusha, na ni kauli ya vitisho dhidi ya asasi zisizo za kiserikali nchini. Nchi yetu imekumbwa na kasumba ya viongozi kuacha kutatua dalili zinazoashiria upotevu wa amani na kutaka kuonyesha kuwa asasi za kiraia na makundi mengine ndio chanzo cha matatizo hayo. Kauli kama za Mh Lukuvi zimeshatolewa ndani ya miezi sita iliyopita na mawaziri na viongozi wengine
--------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------
Board of Directors:
Dr. Helen Kijo Bisimba, Kharous Mpatani, Martina Kabisama, Tike Mwaipabipile, Joseph Parsambei,
Saed Kubenea, Hamisa Mmanga and Ernest Kimaya. 

wasiopungua watano. Waziri Kagasheki alizishutumu wazi wazi asasi za kirahia zinazotetea haki za wafugaji Loliondo kuwa ni wachochezi wa mgogoro huo, wakati huo huo Naibu waziri wa Ardhi aliendeleza shutuma na vitisho hivyo dhidi ya Asasi zinazotetea rasimali ardhi nchini. Tunamsihi Lukuvi, atambue kuwa imani ya wananchi dhidi ya jeshi la polisi nchini haijawahi kuondolewa na asasi za kiraia, bali huondolewa na matendo ya kidhalimu ya jeshi hilo dhidi ya wanachi na vyama vyao. Jeshi la polisi litaweza kurudisha imani kwa wananchi endapo tu litaacha kutumika na watawala kwa maslahi binafsi na kisiasa na sio kwa kauli za kubeza zitolewayo na viongozi wa serikali dhidi ya asasi za kiraia na makundi mengine. Itakumbukwa kwamba hivi karibuni katika uchaguzi wandani wa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi, mwenyekiti wa chama hicho ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Tanzania, na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. JakayaKikwete, aliwatahadhrisha wana –CCM wasiendelee kulitegemea Jeshi la Polisi kama nguzo yake kisiasa. Viongozi waache mzaha katika hali ya usalama wa Taifa kwa sasa kwani hakuna anaependa amani ya Taifa itoweke. Hadi sasa matukio ya kutishia amani ya Nchi yamekuwa yakishika kasi bila kuona jitihada za makusudi za kukomesha hali hiyo. Toka kushambuliwa kwa wahariri Saed Kubenea na Ndimara Tegambwage, kutekwa na kuteswa kwa Dk. Stephen Ulimboka, kuuawa kwa Mwangosi, Mwenyekitiwa Jukwaa la Wahariri Absalom Kibanda, kuuawa kwa mapadre na mashekh, mlipuko wa Olasit dhidi ya waumini wa Kanisa katoliki, migogoro ya kidini na mengineyo, hakuna hata moja lillilopatiwa ufumbuzi wa kudumu.
 USALAMA WA WAANDISHI WA HABARI
Mtandao pia unalaani kitendo cha Jeshi la Polisi kuwanyima uhuru waandishi wa habari, na kuwafukuza waandishi wa habari katika mikusanyiko ya mjini Arusha.Mtandao unalisihi jeshi la Polisi kumwachia mwandishi wa Chanel Ten Ashiraf Bakari, aliyekamatwa tarehe 18/6/2013 katika eneo la Soweto alipokuwa akichukua picha za matukio ya jeshi la polisi dhidi ya raia waliopiga kambi katika viwanja. Tunaalani kitendo cha jeshi la polisi kumkamata bwana Ashirafu aliyekuwa na vitendea kazi pamoja na kitambulisho chake cha uandishi wa habari.
--------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------
Board of Directors:
Dr. Helen Kijo Bisimba, Kharous Mpatani, Martina Kabisama, Tike Mwaipabipile, Joseph Parsambei,
Saed Kubenea, Hamisa Mmanga and Ernest Kimaya.

WITO WETU

1. Tunamsihi Waziri Lukuvi aifute kauli yake dhidi ya asasi za kirai aambazo kimsingi kwa mujibu wa utendaji kazi zao ni Watetezi wa Hakiza Binadamu katika fani mbalimbali na hawahusiki kwa namna yoyote ile katika hali ya sasa ya uvunjufu wa amani unaondelea nchini.
2. Aidha tunaomba asasi kwa upande wao zisijihusishe na itikadi yoyote ya kisiasa bali waendelee kuwatumikia Watanzania waitikadi zote bila ubaguzi wowote.
3. Jeshi la polisi mkoani Arusha limwachie mwandishi wa chanel Ten bwana Ashiraf Bakari, na kuwapa uhuru waandishi kureport habari yoyote.
4. Viongozi wote wakiwemo wa madhebu mabalimbali walaani vikali hali inaoyoendelea Arusha kwa sasa.
5. Balozi mbalimbali na Mashirika mbalimbali kukemea hali ya ukiukwaji wa haki za binadamu unaoendelea Mjini Arusha.
6. Viongozi watambue kazi za asasi za kiraia na kuziheshimu na kuacha kuwaita wachochezi.

Tarehe, 19/06/2013 Mungu Ibariki Afrika, Mungu Ibariki Tanzania!.
 Onesmo Olengurumwa Mratibu Wa Taifa Mtandao wa watetezi wa Haki za Binadamu

CHETI CHA KUSHIRIKI SEMINA YA WAHARIRI WA HABARI NA WAANDISHI WAANDAMIZI-IRINGA

 MKURUGENZI MTENDAJI MANISPAA YA IRINGA THERESIA MAHONGO KWA NIABA YA RC DK CHRISTINE ISHENGOMA AKINIKABIDHI CHETI CHA KUSHIRIKI SEMINA YA WAHARIRI WA HABARI NA WAANDISHI WAANDAMIZI ILIYOANDALIWA NA TANAPA KAULI MBIU VYOMBO VYA HABARI DHIDI YA MAPAMBANO YA  UJANGILI WA TEMBO
MKURUGENZI MKUU WA TANAPA ALLAN KIJAZI AKINIPA MKONO WA PONGEZI .

VIJANA WANAODAIWA KUTEKWA ,KUPIGWA,KUTESWA NA KUFUNGIWA OFISI YA CCM SERENGETI

MBUNGE,DIWANI WADAIWA KUONGOZA KIKUNDI CHA KUTEKA WATU NA KUWAPIGA,
Walifungiwa ndani ya vyumba CCM,wakaokolewa na kamati ya ulinzi na usalama.
Juni 17,2013
KATIBU wa Cwt Taifa (Mbunge)Amina Makiragi kwa kushirikiana na diwani mteule wa CCM kata ya Manchira Marko Shaweshi wanatuhumiwa kuongoza kikosi cha kuteka,kutesa,kisha kuwafungia vijana zaidi  ya 25 katika vyumba vilivyoandaliwa CCM  wasipige kura.
Kitendo hicho ambacho kinatafsriwa kama ugaidi kinadaiwa kutokea juni 16 mwaka huu  nyakati na maeneo tofauti katika kata hiyo,kimethibitishwa na polisi wilayani hapa ,kwa pamoja wakiongozana Ocd,Dso na Katibu tawala walifanikiwa kuwatoa mahabusu hizo wakiwa wameumizwa.
Katika mahabusu hizo walichanganywa wanawake na wanaume pomoja ,huku wakiporwa vitu mbalimbali ,simu,vitambulisho vya kupigia kura,kadi za benki na pesa na baadhi walidumbukizwa kwenye matope.
Anjeliste James(31)mkazi wa kitongoji cha Miserere kijiji cha Miseke kata ya Manchira akiwa na wenzake  kituo cha polisi Mugumu kwa ajili ya kupata pf3 ,alisema,”Makiragi,Shaweshi na vijana wao wa green guard wanne  wakiwa na gari land cruiser T352 AHD,waliniteka nikienda kupiga kura na kunipiga….kisha kunipeleka chumba cha mateso polisi…nilikuta vijana zaidi ya 20 nikawekwa humo”alisema kwa masikitiko.
“Kabla ya kuingizwa humo ndani walinipiga na kusema wananiweka katika kundi la wanaume waweze kunishughulikia … walichukua simu yangu,kitambulisho cha kupigia kura..toka saa 5 asubuhi niliokolewa na kamati ya ulinzi na usalama saa 10.30 jioni…,mbunge dk,Stephen Kebwe alikuwepo unyama huu unatendeka na hakusema kitu…walikuwa wamepanga “alisema akitokwa machozi.
Baraka Nestory(27)mkazi wa kitongoji cha Miserere kijiji cha Miseke alisema kundi hilo kwa kutumia gari la CCM wakiongozwa na vijana wawili wa kijijini hapo Amosi Benson ,Ally John na vijana wanne wageni walioletwa kwa kazi ya utekaji walimpiga na kumpeleka chumba cha mateso CCM.
“Kufika CCM nilikuta viongozi mbalimbali nikaamriwa kulala chini kisha nitembee kama nyoka…huku nikikanyagwa mgongoni…kulikuwa na vyumba viwili vya mateso nikaingizwa humo huku wakisema nitakoma kwa kutokuunga mkono CCM”alibainisha.
Mrumbe Kisarema(33)mkazi wa kitongoji cha Majengo Miseke alitekwa akiwa na Anjelister na kupigwa kwa muda mrefu na watu wanane wakiongozwa na viongozi hao kisha kufungiwa ndani ya chumba kilichokuwa na kundi kubwa la watu,baadhi wakiwa wanavuja damu na wamepakwa matope.
Peter John Odao(26)mkazi wa Miseke alitekwa na kikundi kilichojitambulisha kama makamanda wa serikali hya CCM na Makiragi akaamru wampige huku akisema kama hatakubali kuwa upande wa CCM atapata shida na kumpora simu yake kisha kumzungusha hadi CCM na kufungiwa mahabusu .
“Walilenga kupunguza kura…tusipige kura sisi na familia zetu…na ndivyo ilivyofanyika mpaka wakashinda kwa kura 676 dhidi ya 624 za Chadema …sisi zaidi ya 25 hatukupiga kura na hata familia zetu zilihangaika kutufuata”alisema.
Innocent Simon(30)mkazi wa Rwamchanga alikamatwa akitoka kanisani na kundi hilo kisha kupelekwa darajani na kuzamishwa ndani ya tope wakachukua fedha sh.40,000,nikavuliwa viatu nikapelekwa mahabusu nikadhani polisi kumbe CCM ,niliokolewa na polisi nikakaa hapo hadi saa 2,usiku.
Julius Makima (42)mkufunzi wa M4C kanda hiyo na ambaye ni katibu wa Chadema Sirari alisema alitekwa akiwa kijiji cha Miseke,na Makiragi akachukua simu zake ,vijana wao wa utekaji wakachukua kadi za benki,sh.20.000 na kufikishwa CCM na kuwekwa mahabusu na kupigwa sana.
“Tukiwa ndani viongozi wa chama walikuwa wanapiga simu kutoa maelekezo kuwa….chukueni mishare pigeni magari ya Chadema yakae chini…kisha hao viongozi hasa Heche na Mbunge uchwara wakamatwe wapigwe na wafikishwe hapa wakiwa hoi…iliniuma sana maana kila chama kikifanya hayo nchi itakuwa wapi….hizi ni dalili za kushindwa kuongoza”alisema.
Mwenyekiti akamatwa na bastola.
Kamanda wa polisi wilaya hiyo Pius Mboko ameliambia Mwananchi kuwa Mwenyekiti wa Uv CCM wilaya ya Tarime Boniphace  Mohere alikamatwa kwa kosa la kupiga na diwani wa kata ya Stendi kuu Marwa Ryoba(Chadema)mbele yake wakati kundi la vijana wa CCM wakitaka kuchukua pikipiki ya Chadema.
“Niliwaweka chini ya ulinzi,diwani akatii huyo mwingine akaanza kupambana na polisi…wakati wanapambana wakagundua ana bastola…wakamnyanganya tukampiga pingu na nkweka ndani…tutawafikisha mahakamani kwa kosa la kupigana na kukutwa na silaha…kama anavielelezo sawa lakini kwenda nayo eneo la uchaguzi alikuwa na nia ovu”alisema.
Kuhusu vijana waliokamatwa alisema akiongozana na ofisa usalama wa Taifa,katibua tawala waliwakuta watu wamefungia ndani ya chumba CCM na wamepigwa na kuumizwa sana,walimchukua katibu mwenezi wa CCM nkwa mahojiano kuhusiana na vitendo viovu.
Mkuu wa wilaya atumia magereza kukamata watu ovyo.
Kaimu mkuu wa wilaya ya Serengeti ambaye ni mkuu wa wilaya ya Bunda Joshua Mirumbe alilazimika kutumia askari magereza kukamata vijana kwenye kata hiyo kwa kisingizio kuwa wanatoa rushwa ,na kuwafikisha polisi,hata hivyo polisi walikuwa wakiwaachia kwa kukosa ushahidi.
Hata hivyo baada ya kubaini kuwa wanaachiwa inasemekana ndio wakawa wanapelekwa chumba maalum CCM,mnyukano huo wa mkuu wa wilaya na Ocd wa kuwaachia watu ulitafsriwa na upande wa CCM kuwa anasaidia Chadema ambapo alitishiwa na mkuu wa wilaya kuwa atamuondoa wilayani hapo iwapo Ccm itashindwa kwa kuwa aligoma kutii agizo la kwenda kukamata watu usiku wanaopinga CCM majumbani ili wasipige kura.
Hata hivyo polisi wamesema kuwa wanaingiliwa kiutendaji na viongozi wa kisiasa kwa maslahi binafsi,na kuwa panapotokea uvunjifu wa amani hulaumiwa wao,huku wakisema magereza si jukumu lake la kwenda kukamata na kama ni ushirikiano wanafanya chini ya polisi si kutumiwa kisiasa.
Mkuu wa wilaya Mirumbe alikana tuhuma hizo huku akielekeza tuhuma kwa jeshi la polisi kuachia watu waliokuwa wanakamatwa na wanaCCM kuwa wanatoa rushwa,hata hivyo hakuwa tayari kubainisha ushahidi wa tuhuma hiyo ya rushwa.
Makiragi alipopigiwa simu na mwandishi kujitambulisha na kueleza sababu ya kumpigia alibadilika ghafla na kudai”hallow,hallow sikusikii vizuri,”akakata simu,alipopigiwa tena hakupokea.
Juhudi za kumsaka ziliendelea kwa kutumia namba nyingine akapokea na mwandishi alipojitambulisha tena,huku simu ikisika vema alisema”hallow ,hallow simu hii sijui ina matatizo ,niko eneo baya nitumie sms nikujibu”alisema na kukata simu.
Alipotumiwa maswali kwa njia ya simu licha ya kumfikia hakujibu hadi tunakwenda mitamboni.
Katibu wa CCM wilaya Abubakar Ghati alipoulizwa alidai kuwa walilazimika kuwakamata baada ya kubaini wanatoa rushwa ,lakini wakifikishwa polisi walikuwa wanaachiwa.
Naye Shaweshi ambaye alishinda nafasi ya udiwani (CCM)alipotakiwa kujibu tuhuma hizo alidai ni siasa tu”hizo ni siasa …sisi tulikamata watu waliokuwa na pikipiki cha Chadema,”alisema.
Kwa mjibu wa viongozi wa Chadema,hekima yaOcd ilisaidia kwa kuwa walikusudia kutangazia umma uvamie ofisi ya CCM kuwatoa watu waliokuwa wametekwa.
Mwisho.


MAJERUHI WAKIWA ENEO LA POLISIMUGUMUSERENGETI


 BAADHI YA VIJANA WANAODAIWA KUWA WAFUASI WA CHADEMA  WALIOTEKWA ,TESWA,KISHA KUFUNGIWA NDANI YA CHUMBA KILICHOANDALIWA KAMA MAHABUSU OFISI YA CCM WILAYA YA SERENGETI KWA MADAI KUWA WALIKUWA WAKIKIPINGA CHAMA WAKATI WA UCHAGUZI WA UDIWANI KATA YA MANCHIRA,WALIOKOLEWA NA KAMATI YA ULINZI NA USALAMA WILAYA,WAKIWA ENEO LA POLISI MUGUMU WAKISUBIRI PF3 KWA AJILI YA KWENDA HOSPITALI KUTIBIWA
MMOJA WA MAJERUHI MKUFUNZI WA CHADEMA KANDA AMBAYE PIA NI KIONGOZI WA CHAMA SIRARI JULIUS MAKINA AMBAYE ALIKUWA MIONGONI MWA WALIOKUWA WAKIENDESHA KAMPENI KATIKA KATA HIYO ANADAI ALIUMIZWA SANA.

VIJANA WALIOTEKWA NA VIONGOZI WA CCM NA KUFUNGIWA OFISI ZA CHAMA HICHO WILAYANI SERENGETI



MAJERUHI NA MAITI WA TUKIO LA BOMU MKUTANO WA KAMPEINI CHADEMA UWANJA WA SOWETO ARUSHA

 MAITI YA MTOTO AMBAYE HAJATAMBULIWA IKIWA KATIKA HOSPITALI YA MOUNT MERU ARUSHA,INADAIWA KIFO CHAKE KIMESABABISHWA NA KUPIGWA RISASI
 WANANCHI WAKIANGALIA MAITI YA MTOTO ,WAKIWA KATIKA PILIKA PILIKA ZA KUTAFUTA NDUGU ZAO AMBAO WALIKUWA HAWAJAONEKANA

HUZUNI NA SIMANZI IMETANDA JIJINI ARUSHA KAMA INAVYOONEKANA HAPO

MIONGONI MWA MAJERUHI AKIWA HOSPITALINI

MAJERUHI

 MAJERUHI
MAJERUHI

MAJERUHI.

SEMINA YA WAHARIRI WA HABARI NA WAANDISHI WAANDAMIZI IRINGA

MAJUKUMU YAKIENDELEA WAKATI WA SEMINA YA WAHARIRI NA WAANDISHI WAANDAMIZI UKUMBI WA SIASA NI KILIMO IRINGA ILIYOANDALIWA NA TANAPA
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII KHAMISI KAGASHEKI AKIFUNGUA SEMINA YA WAHARIRI WA HABARI NA WAANDISHI WAANDAMIZI IRINGA
MKURUGENZI MKUU WA TANAPA ALLAN KIJAZI AKITOA MAELEZO YA HALI HALISI ILIVYO KUTOKA NA KUKITHIRI KWA UJANGILI WA TEMBO KWA WAHARIRI WA HABARI NA WAANDISHI WA WAANDAMIZI IRINGA

MENEJA UHUSIANO WA TANAPA PASKAEL SHELUTETE AKIELEZEA LENGO LA SEMINA HIYO ILIYOANDALIWA NA SHIRIKA HILO,
MWENYEKITI WA KAMATI YA ARDHI MALIASILI NA MAZINGIRA JAMES LEMBELI(MBUNGE)AKIELEZEA MIKAKATI YA KAMATI KWA KUSHIRIKIANA NA WIZARA KATIKA KUPAMBANA NA UJANGILI WA TEMBO.

SEMINA YA WAHARIRI WA HABARI NA WAANDISHI WAANDAMIZI UKUMBI WA SIASA NI KILIMO MJINI IRINGA




KAMPEINI YA MAMAYEE YANIGUSA

                                       SIKUBAKI NYUMA KATIKA KUCHANGIA DAMU
                                                        NIMEGUSWA NA KAMPEINI HIYO

MKUU WA SHULE,OFISA ELIMU WATUHUMIWA KUCHOTA FEDHA ZA NYUMBA YA MWALIMU.


 MKUU WA SHULE,OFISA ELIMU WATUHUMIWA KUCHOTA FEDHA ZA NYUMBA YA MWALIMU.
MEI 1,2013.
Serengeti.

WAKATI taifa likiwa kwenye kihoro cha matokeo mabaya ya kidato cha nne,mkuu wa sekondari ya Nyambureti  kwa kushirikiana na ofisa elimu sekondari wilayani Serengeti wanatuhumiwa kula sh,mil.9 za ujenzi wa nyumba ya Mwalimu.

Fedha hizo zilitolewa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya Mwalimu toka akaunti ya Maendeleo ya halmashauri hiyo,ikiwa ni kuchangia nguvu za wananchi kwa ujenzi wa nyumba ya Mwalimu.

Ubadhirifu huo  unadaiwa kumhusisha mkuu wa shule hiyo  Patrick Majige kwa kushirikiana na ofisa elimu sekondari William Makunja na kupelekea nyumba hiyo  kutokujengwa.

Blogu hii ilibaini kuwa fedha hizo zilitolewa mwaka 2010 na kuwekwa akaunti ya shule benki ya NMB tawi la Mugumu wilayani hapa,hazikufanya kazi kusudiwa badala yake zilitumika kulipana  posho za safari zisizo na  na wito kwa idhini ya ofisa elimu sekondari.

Kwa mjibu wa uchunguzi wa blogu  ulibaini tarehe 1,1,2011 akaunti hiyo ilikuwa na kiasi cha sh,10,489,660= baada ya kupokea sh.mil.9 fedha za mradi na sasa benki hakuna fedha na nyumba haijajengwa.

Blogu hii imeona  ripoti ya mkaguzi wa ndani ya halmashauri hiyo ikionyesha kwa kipindi cha januari 1/2011 hadi desemba 31.2012 posho za safari zilikuwa zimegharimu sh.7,703,400=.

Safari zote zikiwemo za  kuitwa wilayani ambazo ziligharimu sh.1,254,000  hazikuwa na  viambatanisho vya barua za wito zote zikiidhinishwa na ofisa elimu sekondari ambaye pia hukaimu nafasi ya Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri mara kwa mara.

Taarifa hiyo imebainisha kuwa fedha hizo zimetumika kinyume cha lengo kusudiwa la ujenzi wa nyumba bila kufuata sheria,kanuni na taratibu za kubadili matumizi ya fedha ya miradi husika.

Katika hitimisho la mkaguzi amebainisha kuwa mkuu wa shule hiyo Majige anawajibika kwa kubadilisha matumizi ya fedha sh,mil.9 za ujenzi wa nyumba ,malipo ambayo yameidhinishwa na wakuu wake wa idara wakijua fedha hizo si za utawala.

Kuchulikuwa kwa fedha hizo kunakwamisha juhudi za wananchi waliokuwa wameandaa viashiria kama mawe,mchanga na saruji mifuko 48 toka  mwaka 2011ambayo iko hatarini kuharibika kutokana na kukaa muda mrefu.

Ofisa elimu.

Ofisaelimu shule za sekondari William Makunja ambaye hukaimu nafasi ya  Mkurugenzi Mara kwa mara  alipoulizwa kwa njia ya simu kuhusiana na tuhuma hizo kwanza alisita kisha akasema”shule gani hiyo Nyambureti…nilikuwa sijui nitafuatilia ili kujua kama nyumba haijajengwa”alisema.

Alipotakiwa kufafanua kama ameishampitishia  fedha mkuu wa shule na  kwa kazi zipi ,hakukubali wala kukataa,bali alibaki kushangaa kuhusu mwandishi kupata taarifa hizo.

Mkuu wa sekondari.

Majige ambaye ni mtuhumiwa wa ufujaji huo alipotafutwa kwa simu yake ya mkononi na kuulizwa  atoe ufafanuzi kuhusiana na tuhuma hizo  akasema”nipo hapa Mugumu..ulikuwa unataka kujua suala la nyumba ya Mwalimu…niko Mwanza ,unataka kujua fedha za nyumba….mimi nasema,aaah….sihusiki”alisema kwa kusitasita.

“Haya mambo tunatakiwa tuonane ili tuongee vizuri….maana haya mambo si mazuri …umepata wapi hizo habari zote….mimi sihusiki wala sijui….lakini ninge…”akakata simu bila kumalizia sentensi yake.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Good Pamba hakupatikana ofisi kwa kile kilichodaiwa kuwa yuko Musoma kikazi,hata hivyo anadaiwa kutokuchukua hatua licha ya kukabidhiwa taarifa ya ukaguzi.

Diwani.

Nicholaus Maro diwani wa kata hiyo anasema kutokana na ukosefu wa nyumba za walimu amepokea walimu wawili waliopangia hapo wanaishi kwake,huku akisisitiza kuwa tatizo hilo linapelekea walimu kuikimbia shule hiyo.

“Kama fedha zinaletwa za kujenga nyumba ya mwalimu ,mkuu anashilikiana na afisa wake wanakula fedha hizo,mamlaka ziko kimya ….hii inakatisha tamaa ,na wanaoathirika ni watoto wetu kitaaluma …hili hatutalinyamazia”amedai.

Mwisho.