Subscribe:

Ads 468x60px

MJAMZITO WA MIEZI 9 AKATWA MGUU KISHA KUWEKEWA TINDIKALI






Anna Sabai aliyefanyiwa ukatili na mmewe,
Na Anthony Mayunga-Mwananchi.
machi,2014.
Serengeti:“NI zaidi ya miezi sita toka nifanyiwe ukatili na mme wangu na mama mkwe….nahangaika kuuguza mguu niliokatwa panga  kisha nikawekea maji ya betri … sijui kama utapona… kichanga nacho kinasumbua ,jamani nimekosa nini mimi kwa Mungu”
Ni maneno yenye kutia simanzi na ambayo yanaamsha kilio ya Anna Sabai(20)mkazi wa kitongoji cha Manyata kijiji cha Nyamakendo kata ya Mbalibali wilayani Serengeti,ambaye anapasa sauti akiuliza ,wako wapi watetezi wa akina mama ,maana kwa hali aliyonayo anahitaji msaada.
Ukatili aliofanyiwa Anna mama wa watoto wawili katika ndoa yake yenye migogoro na mmewe Hamisi Sabai (20)unazidi kuuweka mkoa wa Mara kwenye taswira mbaya  ,kwa matukio ya ukatili wa wanawake.
Kwa nini analalama?
Agosti mosi ,2013 ikiwa ni tarehe ambayo wakazi wa wilaya hiyo humiminika mnadani ,akiwa ni mjamzito wa miezi  9,akihesabu siku tu kwa ajili ya kujifungua, aliamriwa na mme wake kwenda kuchunga ng’ombe,bila kujali hali aliyokuwa nayo.
“Kwa kweli nilikuwa na hali mbaya sana…nikiwa machungani nilikaa chini ya kivuli huku ng’ombe wanachunga….hali ilivyozidi kuwa mbaya nikalala usingizi hapo….alipokuja mme wangu akakuta nimelala…akaanza kunishambulia kwa kipigo ,akidai kuwa nilikuwa na mwanamme …mapenzi yamenoga hadi nikasinzia na kuacha ng’ombe wanachunga wenyewe”anasema kwa masikitiko.
Anasema pamoja na kujieleza na kwa kuzingatia hali yake,walipofika nyumbani mama mke wake Bhoke Sabai alizidi kumchochea kijana wake kuwa  nilikuwa na mwanaume ,natakiwa kupewa kipigo ili nikome.
“Pamoja na kuwa wakati ananipiga sikuwa najitetea kujibu mapigo….lakini akaona aache fimbo akachukua panga na kunikata mguu wa kushoto …niliumia sana ,huku ujauzito…nikawa natamani kufa,maana hali ilikuwa mbaya…sina msaada,kisha nikafungiwa ndani ili watu wasijue  ,wala hakuna kwenda kutibiwa,”anabainisha huku akitokwa machozi.
Ili kuzuia damu isitoke amwagiwa tindikali.
Anna huku amebeba mtoto wake kutembea kwake kwa shida anasema,ili watu wasije kujua unyama aliotendewa walileta maji ya betri na kumwagia kwenye kidonda,”hakika maumivu yalikuwa zaidi ya uchungu wa kujifungua,nilifikia hatua kama ningepata kitu cha kujimaliza ningekufa….huku nasumbuliwa na mimba …naumizwa hivi…jamani wanaharakati wanaotetea wanawake wako wapi…maana nitakatwa mguu hivihivi”anasema na kuibua simanzi.
Matokeo yake mguu ukaoza ,kwa kuwa alikaa ndani muda mrefu ,ndugu zake hawaambiwi,huku mama mkwe wake akimkejeri kila wakati,na kuwa hajaona watu wenye roho ya kikatili kama hao,kwa kuwa walilenga kumuua bila kosa.
Aokolewa na Mama yake mzazi.
Anasema kuwa akiwa amekata tamaa kwa kuwa alikuwa anafungiwa ndani mara kwa mara majilani wasijue,lakini kuna wakati alilazimika kumlilia Mungu,kwa nini afe bila ndugu zake kumwona,ndipo bila kutarajia alistua mama yake mzazi Mnanka Chacha(48)akifika hapo  baada ya kutaarifiwa na majilani.
“Nilipomwona Mama nikasema basi sasa hata kama nikifa …niko mikono salama,huenda maiti yangu itapewa heshima kama binadamu…maana kama ningefia mkononi mwa hao  huenda maiti ingetupwa kama mbwa….nilijisikia ahueni kwa kumuona mama”anabainisha.
Afikishwa hospitali kwa matibabu.
Anasema kwa kupitia polisi mama yake alimfikisha hospitali Teule ya Nyerere kwa ajili ya matibabu ,madaktari walipomwona walimwambia kuwa hawana uwezo tena wa kumtibu kwa hali aliyonayo wakamwandikia barua kwenda hospitali ya rufaa ya Bugando.
Akosa pesa .
Kutokana na ukata wake na mama yake ,alishindwa kwenda Bugando na kuamua kurudi nyumbani kwake kwa ajili ya kutafuta wasamaria wema ili aweze kwenda Bugando kwa ajili ya matibabu.
Mme achana barua ya rufaa.
Katika kuhakikisha juhudi za kupelekwa hospitali hazizai matunda ,akiamini kuwa mme wake alikuwa ameishajirudi alimpa barua ya rufaa ili watafute fedha za matibabu,lakini yeye akaichana,akawa hana jinsi ya kufanya.
“Alichana barua ya rufaa…ikawa sina namna yoyote ya kwenda kutibiwa hospitali ya rufaa ya Bugando….ikabidi nikae tu nyumbani nikiangalia mguu wangu unaoza….kwa kweli nahitaji msaada kwa watu wanaoguswa maana kula yangu hata ya mtoto ni ya shida…siweze kwenda zaidi ya hapa”anasema.
Anabainisha kuwa alichana barua huku akilalama kuwa nimetoa siri polisi na kwa watu wengine hivyo ili kunikomoa akaona aichane ili kupoteza ushahidi.
Ajifungua mtoto wa kiume.
Agosti 24,2013 ikiwa ni siku 24 toka amefanyiwa ukatili na mme wake alijifungua mtoto wake wa pili wa kiume ambaye anazunguka naye katika hali aliyonayo,na kama si  msaada wa wasamaria  wema  kumpeleka dispensari ya Machochwe huenda angepata shida zaidi,lakini mme wake hakuwa na mpango wowote.
“Hakuna matumizi mme wangu anayotoa  kwangu na kwa mtoto….dada kwa kuona hali hiyo amenichukua niko kwake mtaa wa bomani mjini Mugumu na mwanangu huyu…maana yule wa kwanza alifariki”anabainisha.
Anawaomba wanawake wanaofanyiwa ukatili wafike polisi kutoa taarifa kwa kuwa kwa tatizo lake amebaini kuwa askari wa dawati la jinsia akimtaja kwa jina la Sijali amekuwa kama ndugu,anamnunulia dawa na amehangaika naye kwa muda mrefu bila kuchoka.
Diwati la jinsia wajitosa kuwasaka watuhumiwa.
Katibu wa dawati la jinsia polisi wilaya ya Serengeti Sajenti Sijali Nyambuche anasema kwa muda mrefu wamekuwa wakiwasaka watuhumiwa ,lakini wanakosa ushirikiano kutoka kwa jamii ikiwemo baadhi ya viongozi.
“Tukajifanya kusahau,nao wakajisahau wakaendelea na maisha ikiwemo kilimo cha tumbaku,na tukafanikiwa kuwakamata kirahisi ,mama na mtoto kwa tuhuma za kujeruhi”anasema Sijali.
Anasema wamefungulia jalada namba MUG/DAW/IR/30/2014 kwa tuhuma za kusababisha dhara .
Afanyiwa uchunguzi tena.
Katibu wa dawati analazimika kumfikisha hospitali ili kujua hatima ya mguu huo, kama unatibika ama kukatwa.
Daktari adai misuli ilivurugwa.
Dk.Richard wa hospitali teule ya Nyerere anasema baada ya kupiga picha ya Xray wamebaini kuwa mishipa haikukatwa wakati wa shambulio hilo,bali kuna misuli iliyoharibiwa ,kutokana na hali hiyo mguu huo utakuwa kama mwenye ugonjwa wa matende.
“Ni bora akabaki hivyo,akawa anapata dawa inapotokea maumivu…kwa kuwa vidole havichezi vimeisha kufa ganzi …maana zaidi ya hapo ni kukata mguu atapata ulemavu na maumivu mapya….nashauri anapokuwa anahisi hali tofauti aje apate dawa kuliko kukatwa mguu”anashauri Dk.
Mme ajifanya amezimia asitoe maelezo.
Sabai katika hali ya kushangaza baada ya kukamatwa na kulala mahabusu na mama yake anapotakiwa kutoa maelezo ,ghafla anaanguka na kujifanya amezimia,hata hivyo haikumsadia alipozinduka akatoa maelezo huku akidai kuwa mke wake alilala na mwanamme mwingine  ambaye hakumtaja na kuacha ng’ombe wanazunguka.
Lakini anakana kuwa hakumwekea maji ya betri kwenye kidonda,huku akishindwa kueleza kwa nini alimkata na kushindwa kumpeleka hospitali,na kuchana barua ya rufaa kwenda Bugando kwa matibabu.
Mama yake alidai yeye hakuhusika na ukatili huo.
Wanaharakati.
Mratibu wa kitengo cha kuzuia ukatili wa kijinsia kupitia CCT wilayani Serengeti,Sophia Mchonvu,anasema matukio ya ukatili wa kijinsia yameshika kasi wilayani hapo,na kuomba vyombo husika kutoa adhabu kali ili liwe fundisho .
Matukio mengine.
Mwaka 2000 Kadogo Waya alipigwa na mme wake kutokana na wivu wa mapenzi kisha akamwagia tindikali na miguu ikaoza na kupelekea kukatwa miguu yote,hivi karibu mkazi mmoja wa kijiji cha Bisarara wilayani hapa alimjeruhi vibaya mke wake na kung’ata mtoto kisa kikiwa ni kugoma kwenda kuchunga ng’ombe usiku ndani ya hifadhi ya Taifa ya Serengeti,n
Mawasiliano kwa atakayeguswa,0759891849,0787239480,au 0684518319 Katibu wa dawati la jinsia.
Mwisho.