MTOTO ALIYEZALIWA UTUMBO UKIWA NJE AKIWA CHINI YA UANGALIZI WA WAUGUZI NYERERE HOSPITALI WILAYANI SERENGETI KABLA YA KUPELEKWA HOSPITALI YA RUFAA YA MWANZA
MTOTO
ALIYEZALIWA UTUMBO NJE APELEKWA BUGANDO
Oktoba
22,2013.
Serengeti:HOSPITALI
Teule ya Nyerere wilayani Serengeti imetoa rufaa ya mtoto aliyezaliwa katika kijiji cha Nyichoka wilaya
ya Serengeti utumbo ukiwa nje kwenda hospitali ya rufaa ya Bugando kwa ajili ya
matibabu zaidi.
Mtoto huyo wa kike
alizaliwa oktoba 20 mwaka huu utumbo ukiwa nje hali iliyowachanganya
wazazi wake Edward Mgabo(25)na Hadija Rajabu(21) kutokana na hali aliyokuwa
nayo,lakini akiwa mwenye afya njema.
Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo Dk,Calvin Mwasha amesema
wamelazimika kutoa rufaa kwenda Bugando kwa kuwa hawana madaktari bingwa wa
matatizo kama hayo,na hali aliyonayo anahitaji huduma za haraka ili kunusuru
maisha yake.
“Matatizo kama haya hutokana na ukuaji…miezi mitatu ya mimba
…viungo hutengenezwa ,hapo ndipo hutokea mambo kama hayo….ni mambo ambayo
hutokea kitaalam yanajulikana na ndiyo maana kuna wanaoyashughulikia”alisema.
Alisema inapotokea inahitaji huduma za haraka sana ikiwa ni
pamoja na upasuaji mara moja ili kudhibiti mambo yanayoweza kuchangia kupata
maambukizi mengine.
Akisimulia tukio hilo baba wa mtoto huyo Mgabo
alisema,”tukiwa tunaenda zahanati ya Nyichoka mke wangu alizidiwa na
kujifungulia njiani…tulisaidiwa na watu wakamfunga kitovu mtoto …lakini utumbo
ukaonekana uko nje,tukaambiwa tuwahi zahanati Muuguzi naye akasema hana uwezo
twende wilayani”alisema.
Alibainisha walipofika kila mmoja anaonekana kushangaa na
kusema hilo tatizo wanatakiwa kwenda Bugando”huyu ni mtoto wangu wa kwanza kwa
mwanamke huyu ambaye nilimkuta na mtoto mwingine…tunapambana kupata fedha ili
kuokoa maisha ya mtoto wetu “alisema kwa masikitiko.
Mama mzazi wa mtoto Hadija alisema wakati wa ujauzito
hapakuwa na tatizo lolote ,na hata wakati anajifungulia njiani hapakuwa na
shida kwa kuwa mtoto alikuwa mzima ,lakini alishangaa kuona utumbo uko nje na
akawa amekata tamaa kama ataweza kuishi.
Muuguzi wodi la wajawazito Anjelina Biseko alisema kuwa
watoto kama hao wanapofikishwa Bugando huwekwa kwenye mifuko maalum kwa muda wa
miezi mitatu kisha hufanyiwa upasuaji ili kurudisha hali yake ya kawaida
Muuguzi mkuu wa hospitali hiyo Neema Mechara alisema kwa
mwaka huu hilo ni tukio la kwanza kutokea,lakini kumewahi kutokea tukio kama
hilo kwa mtoto kuzaliwa viungo vya ndani vikiwa nje,na wengine maumbile ya
ajabu ajabu.
Mwisho.