Subscribe:

Ads 468x60px

Nilifanyiwa unyama na kaka yangu

Nilifanyiwa unyama na kaka yangu  Send to a friend
Sunday, 02 September 2012 07:24

ALINIZIBA MDOMO KWA NGUO YA NDANI, AKANIFUNGA KWENYE MTI PORINI, AKANIBAKA
Anthony Mayunga
UKATILI wa kijinsia unaendelea kushika kasi nchini ambapo hivi karibuni, mkazi mmoja wa Kijiji cha Kemugesi, wilayani Serengeti mkoani Mara amembaka dada yake na kasha kumfunga porini kwa zaidi ya saa saba, huku yeye akitokomea kusikojulikana.
Kijana huyo, jina tunalo alitenda unyama huo saa 1:00 asubuhi ya Julai 22, mwaka huu, huku taarifa nyingine zikidai kuwa kijana huyo pia aliwahi kumtendea ukataili kama huo shangazi yake.
Akisimulia mkasa huo, binti aliyeathirika na ukatili huo(Jina tumelihifadhi kwa sababu za kimaadili), alisema kuwa kaka yake huyo alimbaka huku akiwa amemsokomeza nguo ya ndani mdomoni kumzuia asipige kelele.
“Kaka alinibaka akiwa ameniwekea nguo yangu ya ndani mdomoni,  huku akinibana nisipige kelele. Kisha akanifunga kwenye mti na nilikaa kuanzia  saa 5 asubuhi hadi saa 12 jioni,” anasimulia binti huyo mwenye umri wa miaka 15.
Anaelezea kuwa kaka yake huyo ambaye wanachangia baba, alimwomba aende naye shambani akamsaidie kuvuna pamba na ndipo alitekeleza unyama huo.

Binti huyo ambaye ni mmmoja wa watoto 29 wa baba yao aliye na wake wanne anasema kuwa  licha ya kupata maumivu makali kutokana na kubakwa, kaka yake huyo pia alimpiga sana na kumsababishia maumivu makali sehemu mbalimbali za mwili.
Hata hivyo, mbali na binti huyo kufanyiwa unyama, baba yake mzazi anahaha kuhakikisha kwamba binti huyo na mama yake wanamaliza suala hilo nyumbani akidai kuwa kijana wake anasumbuliwa na majini na kwamba akifungwa anaweza kufia jela.

Ilivyotokea
Binti huyo anasimulia kuwa siku ya Jumapili  Julai 22, saa 1:00 asubuhi mwaka
huu, walikwenda na kaka yake huyo kuvuna pamba wakiwa na kijana wao wa kazi, anayewasaidia kuchunga ng’ombe.
"Tulivuna pamba bila matatizo, kwenye saa 4:45 asubuhi akasema tukachume mahindi shambani kwetu kwa ajili ya kwenda nayo nyumbani kwa
ajili ya kuchoma. Tukatoka vizuri hadi tulipoacha madumu ya pamba. Nikakaa, lakini yeye akamwagiza kijana wa kazi arudi shambani kumbe, alitaka kutekeleza nia yake. Hapo alinivamia na kunikaba shingoni,"anasema kwa unyonge na kuongeza:
"Alinibeba na kukimbia nami hadi kichakani na kuchana nguo yangu ya ndani, gagulo na kuniwekea nguo ya ndani mdomoni huku amenibana shingo, akaanza kunibaka. ...Nilipata maumivu makali sana, alichukua muda mrefu akinifanyia unyama huo.”
“Damu zilivuja sana na baada ya kumaliza akanipiga na kwenda kunifungia kwenye mti,   kisha akanipiga teke na kusema kuwa nitafia hapo na nyumbani hawataniona tena,” anaeleza binti huyo.
Anasema kuwa kijana wao wa kazi aliposikia kelele alifika eneo la tukio, lakini kaka yake huyo alimfukuza na kutishia kumuua na kuwa akisikia popote kasema jambo hilo, atamuua.
“Nilihangaika sana kujinasua, nikawa nasugua mikono kwenye mti ndio maana nimechubuka hivi. Hatimaye kitambaa cha machoni kikalegea nikapata nafasi ya kuangalia alipofungia, nilihangaika hadi nikaweza kufungua,” anasema.
Anasema kuwa baada ya kujifungua kwenye mti alikwenda nyumbani na kumkuta mama yake akiwa na wasiwasi kwa kuwa alioongozana nao walirudi na hawakueleza walipomwacha.
Anasema kuwa alimsimulia mama yake kilichotokea naye aliamua kumpeleka kwa Mwenyekiti wa Kitongoji.
Anaongeza kuwa njiani walikutana na mama wa mtuhumiwa na baada ya kumweleza alichofanya motto wake, alisema kuwa kijana wake ana matatizo mengi, hivyo hawezi kushangaa kusikia hilo.

"Kama aliweza kumbaka shangazi yake, kisha akamfunga na kamba na kumwacha porini, sishangai kama amemtendea mdogo wake, maana anatisha kwa matendo yake,”alisema mama wa kijana huyo.

Julai 23,walifika Kituo Kidogo cha Polisi Kenyana na kupewa fomu ya matibabu (PF 3) ambapo polisi walidai wapewe Sh30,000 za mafuta ili wakamtafute mtuhumiwa.
“Walisema wanataka hizo fedha wanunue petroli na waende watatu kwa pikipiki, mama alisema kuwa hana, basi ikawa ndiyo tumekosa ushirikiano zaidi ya kwenda zahanati ya Kenyana kupata matibabu, kisha tukarudi nyumbani,"anaeleza binti huyo.
Kwa mujibu wa binti huyo, Julai 29 mjomba wake,  Chacha Makindi mkazi wa Kemugesi alimchukua hadi Kituo cha Polisi Mugumu ambapo walifungua jalada na kupewa barua ya kwenda kwa Mtendaji wa Kijiji ili mtuhumiwa
akamatwe.
Hata hivyo mtuhumiwa huyo hajakamatwa kwa kile kinachodaiwa kuwa baba yake amemficha.

Binti huyo anadai kuwa hajui kusoma wala kuandika licha ya kuwa alisoma hadi darasa la tano na kuacha kutokana na matatizo ya
kifamilia ambapo wenzake sasa wako kidato cha kwanza.


"Kwetu hakuna hata mtoto aliyefika sekondari, yaani watoto wote 29 na baba
hajali kabisa hata kununua sare. Ndiyo maana niliacha masomo na sasa
sipendi kurudi kijijini nitakaa hapa kwa ndugu yangu...maana hali huko
si nzuri,"anadai binti huyo.


Wanaharakati
Julai 30 akiwa na mjomba wake walifika ofisi ya Wasaidizi wa Kisheria na Haki za Binadamu, ili kupata msaada wa kisheria hali iliyomfanya
baba yake mzazi ajisalimishe baada ya kuandikiwa barua na kuanza kumhudumia kwa ajili ya matibabu .


Kaimu Katibu Mtendaji wa Shirika la Wasaidizi wa Sheria na Haki za Binadamu wilayani Serengeti, Monica Daniel anasema kuwa baada ya kuona mchezo uliopo wa baba yake, waliamua kuingilia kati na wanasimamia matibabu yake .


"Baba yake anataka mambo yaishe, anamlaumu sana mke wake kwa madai kuwa alishamwacha, hivyo kwa tatizo hili hataki kutoa msamaha kwa mtoto wa mke mwenzake.
Sisi tulibaini kuwa huyu mzazi alipoachana na mke wake mdogo hata watoto pia hawapi huduma,"anasema Monica.

Kuhusu vipimo alivyofanyiwa binti huyo Monica alisema: "Katika vipimo amekutwa na maambukizi katika njia ya mkojo(UTI) na macho pia yalikuwa yameumizwa, ambapo baba yake ametoa Sh00,000 za matibabu.”

Anaongeza kuwa wanajiandaa kwenda kumpima binti huyo kama amepata maambukizi ya Vurusi vya Ukimwi.
Hata hivyo, alisema kuwa baba wa binti huyo anaomba shirika lao lisaidie kumshauri mama ya binti huyo ili wayamalize nyumbani na kuendelea na matibabu ya kienyeji akiamini kuwa kijana wake aliyetenda unyama huo anasumbuliwa na majini.
“Sisi tumempa msimamo kuwa haki lazima itendeke, kama ni mgonjwa anatakiwa akapimwe
akili ikithibitika watamwachia. Kwa nini anamficha kama ni mwehu? Hilo tumelikataa kwa kuwa hata aliyejeruhiwa anataka afikishwe mahakamani,"anabainisha Daniel.

Monica aliomba hatua kali zichukuliwe kwa mtuhumiwa wa tukio hilo kwa kuwa kitendo alichofanya ni cha kikatili na hakifai kunyamaziwa.
Alidai kuwa hata mzazi wake anatakiwa kuhojiwa na polisi sababu za kutetea unyama aliofanya kijana wake kwa kuwa ni kinyume kabisa cha sheria ya Mtoto ya mwaka 2009.

Polisi
Polisi wanadai kuwa wanaendelea kumsaka mtuhumiwa huyo na kuwa maagizo yalishatolewa kwa Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Kemugesi kuhakikisha kuwa wanamnasa au kutoa taarifa ili akamatwe na kufikishwa katika vyombo vya
sheria .



0 comments:

Post a Comment