Subscribe:

Ads 468x60px

VIJANA WANAODAIWA KUTEKWA ,KUPIGWA,KUTESWA NA KUFUNGIWA OFISI YA CCM SERENGETI

MBUNGE,DIWANI WADAIWA KUONGOZA KIKUNDI CHA KUTEKA WATU NA KUWAPIGA,
Walifungiwa ndani ya vyumba CCM,wakaokolewa na kamati ya ulinzi na usalama.
Juni 17,2013
KATIBU wa Cwt Taifa (Mbunge)Amina Makiragi kwa kushirikiana na diwani mteule wa CCM kata ya Manchira Marko Shaweshi wanatuhumiwa kuongoza kikosi cha kuteka,kutesa,kisha kuwafungia vijana zaidi  ya 25 katika vyumba vilivyoandaliwa CCM  wasipige kura.
Kitendo hicho ambacho kinatafsriwa kama ugaidi kinadaiwa kutokea juni 16 mwaka huu  nyakati na maeneo tofauti katika kata hiyo,kimethibitishwa na polisi wilayani hapa ,kwa pamoja wakiongozana Ocd,Dso na Katibu tawala walifanikiwa kuwatoa mahabusu hizo wakiwa wameumizwa.
Katika mahabusu hizo walichanganywa wanawake na wanaume pomoja ,huku wakiporwa vitu mbalimbali ,simu,vitambulisho vya kupigia kura,kadi za benki na pesa na baadhi walidumbukizwa kwenye matope.
Anjeliste James(31)mkazi wa kitongoji cha Miserere kijiji cha Miseke kata ya Manchira akiwa na wenzake  kituo cha polisi Mugumu kwa ajili ya kupata pf3 ,alisema,”Makiragi,Shaweshi na vijana wao wa green guard wanne  wakiwa na gari land cruiser T352 AHD,waliniteka nikienda kupiga kura na kunipiga….kisha kunipeleka chumba cha mateso polisi…nilikuta vijana zaidi ya 20 nikawekwa humo”alisema kwa masikitiko.
“Kabla ya kuingizwa humo ndani walinipiga na kusema wananiweka katika kundi la wanaume waweze kunishughulikia … walichukua simu yangu,kitambulisho cha kupigia kura..toka saa 5 asubuhi niliokolewa na kamati ya ulinzi na usalama saa 10.30 jioni…,mbunge dk,Stephen Kebwe alikuwepo unyama huu unatendeka na hakusema kitu…walikuwa wamepanga “alisema akitokwa machozi.
Baraka Nestory(27)mkazi wa kitongoji cha Miserere kijiji cha Miseke alisema kundi hilo kwa kutumia gari la CCM wakiongozwa na vijana wawili wa kijijini hapo Amosi Benson ,Ally John na vijana wanne wageni walioletwa kwa kazi ya utekaji walimpiga na kumpeleka chumba cha mateso CCM.
“Kufika CCM nilikuta viongozi mbalimbali nikaamriwa kulala chini kisha nitembee kama nyoka…huku nikikanyagwa mgongoni…kulikuwa na vyumba viwili vya mateso nikaingizwa humo huku wakisema nitakoma kwa kutokuunga mkono CCM”alibainisha.
Mrumbe Kisarema(33)mkazi wa kitongoji cha Majengo Miseke alitekwa akiwa na Anjelister na kupigwa kwa muda mrefu na watu wanane wakiongozwa na viongozi hao kisha kufungiwa ndani ya chumba kilichokuwa na kundi kubwa la watu,baadhi wakiwa wanavuja damu na wamepakwa matope.
Peter John Odao(26)mkazi wa Miseke alitekwa na kikundi kilichojitambulisha kama makamanda wa serikali hya CCM na Makiragi akaamru wampige huku akisema kama hatakubali kuwa upande wa CCM atapata shida na kumpora simu yake kisha kumzungusha hadi CCM na kufungiwa mahabusu .
“Walilenga kupunguza kura…tusipige kura sisi na familia zetu…na ndivyo ilivyofanyika mpaka wakashinda kwa kura 676 dhidi ya 624 za Chadema …sisi zaidi ya 25 hatukupiga kura na hata familia zetu zilihangaika kutufuata”alisema.
Innocent Simon(30)mkazi wa Rwamchanga alikamatwa akitoka kanisani na kundi hilo kisha kupelekwa darajani na kuzamishwa ndani ya tope wakachukua fedha sh.40,000,nikavuliwa viatu nikapelekwa mahabusu nikadhani polisi kumbe CCM ,niliokolewa na polisi nikakaa hapo hadi saa 2,usiku.
Julius Makima (42)mkufunzi wa M4C kanda hiyo na ambaye ni katibu wa Chadema Sirari alisema alitekwa akiwa kijiji cha Miseke,na Makiragi akachukua simu zake ,vijana wao wa utekaji wakachukua kadi za benki,sh.20.000 na kufikishwa CCM na kuwekwa mahabusu na kupigwa sana.
“Tukiwa ndani viongozi wa chama walikuwa wanapiga simu kutoa maelekezo kuwa….chukueni mishare pigeni magari ya Chadema yakae chini…kisha hao viongozi hasa Heche na Mbunge uchwara wakamatwe wapigwe na wafikishwe hapa wakiwa hoi…iliniuma sana maana kila chama kikifanya hayo nchi itakuwa wapi….hizi ni dalili za kushindwa kuongoza”alisema.
Mwenyekiti akamatwa na bastola.
Kamanda wa polisi wilaya hiyo Pius Mboko ameliambia Mwananchi kuwa Mwenyekiti wa Uv CCM wilaya ya Tarime Boniphace  Mohere alikamatwa kwa kosa la kupiga na diwani wa kata ya Stendi kuu Marwa Ryoba(Chadema)mbele yake wakati kundi la vijana wa CCM wakitaka kuchukua pikipiki ya Chadema.
“Niliwaweka chini ya ulinzi,diwani akatii huyo mwingine akaanza kupambana na polisi…wakati wanapambana wakagundua ana bastola…wakamnyanganya tukampiga pingu na nkweka ndani…tutawafikisha mahakamani kwa kosa la kupigana na kukutwa na silaha…kama anavielelezo sawa lakini kwenda nayo eneo la uchaguzi alikuwa na nia ovu”alisema.
Kuhusu vijana waliokamatwa alisema akiongozana na ofisa usalama wa Taifa,katibua tawala waliwakuta watu wamefungia ndani ya chumba CCM na wamepigwa na kuumizwa sana,walimchukua katibu mwenezi wa CCM nkwa mahojiano kuhusiana na vitendo viovu.
Mkuu wa wilaya atumia magereza kukamata watu ovyo.
Kaimu mkuu wa wilaya ya Serengeti ambaye ni mkuu wa wilaya ya Bunda Joshua Mirumbe alilazimika kutumia askari magereza kukamata vijana kwenye kata hiyo kwa kisingizio kuwa wanatoa rushwa ,na kuwafikisha polisi,hata hivyo polisi walikuwa wakiwaachia kwa kukosa ushahidi.
Hata hivyo baada ya kubaini kuwa wanaachiwa inasemekana ndio wakawa wanapelekwa chumba maalum CCM,mnyukano huo wa mkuu wa wilaya na Ocd wa kuwaachia watu ulitafsriwa na upande wa CCM kuwa anasaidia Chadema ambapo alitishiwa na mkuu wa wilaya kuwa atamuondoa wilayani hapo iwapo Ccm itashindwa kwa kuwa aligoma kutii agizo la kwenda kukamata watu usiku wanaopinga CCM majumbani ili wasipige kura.
Hata hivyo polisi wamesema kuwa wanaingiliwa kiutendaji na viongozi wa kisiasa kwa maslahi binafsi,na kuwa panapotokea uvunjifu wa amani hulaumiwa wao,huku wakisema magereza si jukumu lake la kwenda kukamata na kama ni ushirikiano wanafanya chini ya polisi si kutumiwa kisiasa.
Mkuu wa wilaya Mirumbe alikana tuhuma hizo huku akielekeza tuhuma kwa jeshi la polisi kuachia watu waliokuwa wanakamatwa na wanaCCM kuwa wanatoa rushwa,hata hivyo hakuwa tayari kubainisha ushahidi wa tuhuma hiyo ya rushwa.
Makiragi alipopigiwa simu na mwandishi kujitambulisha na kueleza sababu ya kumpigia alibadilika ghafla na kudai”hallow,hallow sikusikii vizuri,”akakata simu,alipopigiwa tena hakupokea.
Juhudi za kumsaka ziliendelea kwa kutumia namba nyingine akapokea na mwandishi alipojitambulisha tena,huku simu ikisika vema alisema”hallow ,hallow simu hii sijui ina matatizo ,niko eneo baya nitumie sms nikujibu”alisema na kukata simu.
Alipotumiwa maswali kwa njia ya simu licha ya kumfikia hakujibu hadi tunakwenda mitamboni.
Katibu wa CCM wilaya Abubakar Ghati alipoulizwa alidai kuwa walilazimika kuwakamata baada ya kubaini wanatoa rushwa ,lakini wakifikishwa polisi walikuwa wanaachiwa.
Naye Shaweshi ambaye alishinda nafasi ya udiwani (CCM)alipotakiwa kujibu tuhuma hizo alidai ni siasa tu”hizo ni siasa …sisi tulikamata watu waliokuwa na pikipiki cha Chadema,”alisema.
Kwa mjibu wa viongozi wa Chadema,hekima yaOcd ilisaidia kwa kuwa walikusudia kutangazia umma uvamie ofisi ya CCM kuwatoa watu waliokuwa wametekwa.
Mwisho.


MAJERUHI WAKIWA ENEO LA POLISIMUGUMUSERENGETI


 BAADHI YA VIJANA WANAODAIWA KUWA WAFUASI WA CHADEMA  WALIOTEKWA ,TESWA,KISHA KUFUNGIWA NDANI YA CHUMBA KILICHOANDALIWA KAMA MAHABUSU OFISI YA CCM WILAYA YA SERENGETI KWA MADAI KUWA WALIKUWA WAKIKIPINGA CHAMA WAKATI WA UCHAGUZI WA UDIWANI KATA YA MANCHIRA,WALIOKOLEWA NA KAMATI YA ULINZI NA USALAMA WILAYA,WAKIWA ENEO LA POLISI MUGUMU WAKISUBIRI PF3 KWA AJILI YA KWENDA HOSPITALI KUTIBIWA
MMOJA WA MAJERUHI MKUFUNZI WA CHADEMA KANDA AMBAYE PIA NI KIONGOZI WA CHAMA SIRARI JULIUS MAKINA AMBAYE ALIKUWA MIONGONI MWA WALIOKUWA WAKIENDESHA KAMPENI KATIKA KATA HIYO ANADAI ALIUMIZWA SANA.