Subscribe:

Ads 468x60px

RISASI ZINAVYOTUMIKA KUUA RAIA TARIME



Polisi wakiwa katika doria

Na Elias Msuya, Mwananchi

Posted  Jumapili,Marchi16  2014  saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Marwa alipatwa na ulemavu wa mguu Oktoba 9, mwaka jana, baada ya kupigwa risasi na polisi kwenye paja.

Tarime. Katika Kijiji cha Gomsala, Tarime mkoani Mara yupo Matuma Marwa (22), ambaye hakuwahi kufikiria kwamba siku moja atakuwa mlemavu pamoja na kuwa kila binadamu aliye hai ni mlemavu mtarajiwa.
Marwa alipatwa na ulemavu wa mguu Oktoba 9, mwaka jana, baada ya kupigwa risasi na polisi kwenye paja.
“Tulikuwa tunaelekea shambani, tukasikia milio ya risasi ikielekezwa tuliko sisi, risasi moja ilinipata kwenye paja na tangu wakati ule hadi sasa mguu wangu hauko sawa,” alisema Marwa na kuongeza:
“Kazi yangu ni mkulima, ila kwa sasa nashindwa kulima kwa kuwa mguu bado unauma.”
Marwa ni miongoni mwa watu waliopatwa na madhila yatokanayo na vita ya rasilimali baina ya wananchi na wawekezaji.
Marwa anaishi katika kijiji kilicho kandokando ya mgodi wa dhahabu wa North Mara.
Mgodi wa North Mara unamilikiwa na Kampuni ya African Barrick Gold tangu 2006 ilipoununua kutoka kwa Kampuni ya Placer Dome Tanzania, iliyokuwa ikimilikiwa na Afrika Mashariki Gold Mines.
Taarifa rasmi kutoka katika vijiji vinavyozunguka mgodi huo, zinaonyesha kuwa, mbali na waliojeruhiwa na kupata ulemavu wa kudumu, pia wapo waliopoteza maisha kutokana na kupigwa risasi na polisi wanaolinda usalama katika migodi hiyo.
Matukio hayo na mengine ya unyanyasaji, yanawafanya wakazi wa maeneo haya kuchukulia uwepo wa madini ya dhahabu kama kero kwao na siyo neema au baraka kama ilivyotarajiwa.
Watu 24 wanadaiwa kwamba wamekwisha uawa kwa kupigwa risasi katika matukio, akiwamo mkazi wa Kijiji cha Nyangoto, Ryoba Maseke ambaye alipigwa risasi Julai 12, 2012.
Shangazi wa Maseke, Suzana Mwita anasema, marehemu alikuwa mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya sekondari ya Mugumu, Serengeti na alifika kijijini kusalimia ndugu zake na hapo ndipo mauti yalipomkuta.
Mwaka huohuo, polisi pia wanadaiwa kwamba walimuua kwa risasi mkazi wa kijiji cha Kewanja, Kibwaba Ghati (23) katika tukio la Novemba 6, wakati wananchi wanaodaiwa kuvamia mgodi, walipokurupushwa na askari wa jeshi hilo.
Mama mzazi wa Ghati, Wankrugati Malembela alisema: “Mwanangu alikuwa akichunga ng’ombe, Polisi walikuwa wakiwakimbiza wavamizi na kupiga risasi ovyo, ndipo risasi mojawapo ilipompata kwenye paji la uso na kufariki pale pale”.
Aliongeza: “Polisi waliuchukua mwili wake na kuupeleka mgodini na kuupiga picha wakisema eti alikutwa huko.”
“Tumekuwa tukifuatilia suala hili polisi lakini wanasisitiza kuwa alikutwa mgodini.Tumekwenda Barrick lakini wanatuzungusha tu,” alisema Malembela.
Polisi wajitetea
Diwani wa Kata ya Kemambo, Wilson Mangure alisema tangu 2011 hadi Januari mwaka huu, watu 69 wameuawa kwa kupigwa risasi na polisi huku mamia wengine wakijeruhiwa.
“Bado tunakusanya taarifa, lakini mauaji bado yanaendelea. Mwaka huu wameuawa watu wanne katika matukio matatu tofauti,” alisema Mangure.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya, Justus Kamugisha alikiri kuwapo kwa vifo ambavyo alisema vinatokana na mapambano na wavamizi wa mgodi.
Hata hivyo alisema mauaji hayo siyo ya mfululizo. “Hakuna mfululizo wa mauaji…, sisi kazi yetu ni kulinda raia na mali zao na kulinda mwekezaji, hatuko hapa kuua watu. Tunapambana na wavamizi ambao wanaingia mgodini kuiba dhahabu na kuharibu mali,” alisema Kamanda Kamugisha na kuongeza:
“Ungekuja hapa ningekuonyesha jinsi wanavyoharibu… kuna dhana kwa wananchi hapa Tarime kuwa dhahabu iliyoko pale ni yao. Wanavamia mgodi wanapambana na polisi. Wapo baadhi ya polisi waliojeruhiwa vibaya.”
Kwa upande wake Kamishna wa Polisi wa Mafunzo na Operesheni, Paul Chagonja ambaye ameshatembelea eneo hilo mara kadhaa, alisema mauaji yanayotokea yana sababu maalumu:
“Polisi siyo wajinga, waue watu bila sababu, haiwezekani, lazima kuwe na sababu…, huo ni mgogoro wa muda mrefu mno na ninyi waandishi wa habari mnapaswa kuwa wazalendo katika suala hilo,” anasema Chagonja na kuongeza: “Pale kuna watu wakorofi wanaopambana na polisi na kuharibu mali.”
Matukio mengine
Matukio hayo yanaendelea kutokea hadi sasa kwani Januari 6, mwaka huu, mkazi wa Kijiji cha Kewanja, Kimosi Leonard alipigwa risasi mguuni baada ya polisi kuvamia kijiji hicho kwa lengo la kukamata baadhi ya watu.
“Mimi nilikuwa napita na safari zangu tu, nikashangaa watu wanakimbia ovyo. Ndipo nilipojikuta nimepigwa risasi ya mguu,” alisema Leonard ambaye anatembea kwa kuchechemea.
Aliongeza: “Siwezi kwenda kulalamika polisi, maana ukifika huko ndiyo unaongezewa kesi nyingine ya kuvamia mgodi.”
Mwingine ni Weigama Range ambaye alisema watoto wake Fredrick (7) na Happiness (6) wamepata ulemavu baada ya kulipukiwa na mabomu ya machozi yaliyorushwa na polisi.
“Watoto wangu walikuwa wakisoma katika shule ya msingi ya Kewanja. Agosti 23, 2011 polisi walirusha mabomu hapo shuleni na wanafunzi walianza kukimbia ovyo, ndipo mtoto wangu Happiness alianguka na kupoteza fahamu. Hadi leo ana tatizo la kuanguka anguka. Fredrick naye alianguka na kung’oka meno matatu ya mbele,” alisema Weigama na kuongeza:
“Mwaka huu, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja alikuja kufanya mkutano hapa kijijini na nilimwonyesha watoto na fomu za polisi na aliahidi kunisaidia, lakini sijapata msaada wowote. Nimejaribu kufuatilia polisi na kwa mbunge wetu, lakini sijapata chochote.”
Mbunge wa Tarime, Nyambari Nyangwine alizungumzia hali ilivyo sasa: “Angalau kwa sasa hali inaendelea kuimarika, kuliko zamani hali ilikuwa mbaya zaidi. Hayo mauaji ni kweli yanatokea na lawama nazipeleka kwa Serikali. Siwalaumu Barrick kwa sababu polisi ndiyo wanaofanya mauaji.”
Uvamizi wa mgodi
Baadhi ya wananchi wanakiri kwamba wamekuwa wakivamia mgodi, lakini wanawakosoa polisi kwa kutumia risasi za moto kuwadhibiti.
Marwa Bina (30) ambaye alikiri kwamba aliwahi kufanya uvamizi, alisema wanalazimika kufanya hivyo kwa kuwa hawana ajira.
“Tunavamia pale ili tupate fedha za kujikimu, ila kwa sasa ulinzi umeimarishwa na hata wakikupiga risasi hupewi fidia,” alisema.
Mwingine ni Joshua Masyaga aliyekuwa mvamizi mgodini hapo ambaye alisema vijana wengi waliamini kwamba watafaidika na madini hayo hata kwa kuyaiba tu
“Mimi nilikuwa mvamizi baada tu ya kumaliza kidato cha nne 2010. Ni kweli nilipata dhahabu na kuuza lakini ni maisha ya hatari mno. Nimeshuhudia rafiki zangu wengi wakiuawa kwa risasi.
Akifafanua jinsi biashara hiyo inavyofanyika, Masyaga alisema kulikuwa na mawakala wa madini ambao huwasiliana na wafanyakazi wa mgodi wanaotoa kifusi nje.
“Kuna matajiri wanaofanya mpango na wafanyakazi wa ndani na polisi nao hushirikishwa. Mawe yakishamwagwa nje wale matajiri hutuma vijana wao kuokota na wengine huvamia tu. Hao ndiyo hupigwa risasi na polisi,” alisema na kuongeza:
“Mawe yakishapatikana tunayapeleka kwa wasafishaji ambao huyasaga na kuyawekea zebaki ili kupata dhahabu ambayo huchukuliwa na matajiri. Hata hivyo siku hizi ulinzi umeimarishwa mno, hiyo biashara imekufa.”
Majibu ya Barrick
Meneja wa Mgodi wa North Mara, Gary Chapman alisema:
“Mara nyingi watu wanaouawa ni wale wanaopambana na polisi, vinginevyo tuna uhusiano ni mzuri na wanajamii na ndiyo maana tunafanya nao mikutano kujadili maendeleo na watu wanashukuru kwa huduma zetu.”
Aliongeza: “Kuna watu wanaovamia mgodi wetu. Kwa hiyo unapozungumzia migogoro kama hiyo, siyo kwa mgodi tu bali katika jumuiya nzima.”
Naye Ofisa Uhusiano na Mawasiliano ya Umma wa ABG, Nector Foya alisema kampuni hiyo inao mfuko wa maendeleo (The ABG Maendeleo Fund) ambao hutoa huduma kwa wanajamii wanaozunguka migodi yao.
“Tuna mfuko wa maendeleo ya jamii ambao unasaidia huduma kama vile elimu, maji na afya. Tumejenga shule, hospitali na miradi ya maji katika vijiji vinavyozunguka migodi yetu, ndiyo maana tunasema tunao uhusiano mzuri na wanajamii,” alisema.
Halmashauri Tarime
Wakati kukiwa na matukio yanayozua mvutano baina ya wawekezaji na wananchi, uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime unajivuna kwa kupata faida kutoka kwenye mgodi huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Athuman Akalamu alisema tangu kampuni ya ABG ilipofika imekuwa ikijitanua, hivyo kuchukua maeneo ya vijiji vilivyo jirani, hali inayosababisha migogoro ya ardhi miongoni mwa wanavijiji kutokana na fidia iliyokuwa ikilipwa.
Alisema kutokana na migogoro hiyo, Serikali iliunda kikosi kazi kwa ajili ya kushughulikia malalamiko husika.
Kiongozi wa kikosi hicho Minja Jeremiah alisema: “Mwaka 2012 Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Steven Masele na aliyekuwa Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Charles Kitwanga walitembelea mgodi huu baada ya kampuni ya ABG kulalamika kuwa eneo lao halitoshi. Hivyo tathmini ilifanywa na kijiji cha Nyangoto kilitakiwa kutoa eneo”.
Hata hivyo alisema kutokana na hali hiyo, kuliibuka makundi matano ya watu.
“Kundi la kwanza lilipinga kabisa mpango huo, huku la pili likikubali ila kwa kulipwa kwanza fidia, la tatu lilikubali fidia lakini waliendeleza makazi yao, wengine wakakubali sehemu ya fidia na wengine walichukua fidia lakini hawakuhama.
Ndiyo maana kikosi hiki kiliundwa Aprili 2013,” alisema. Alisema tangu wakati huo, wameshafanya uthamini katika vijiji vya Kewanja na Nyakunguru na wanavijiji wameshapata kibali cha Mthamini Mkuu wa Serikali na wamelipwa fidia katika awamu nne.
Hata hivyo anasema wapo watu wapatao 4,000 waliofanyiwa tathmini lakini bado hawajalipwa.
Utatuzi wa migogoro
Katika kurejesha uhusiano mwema kati ya mgodi huo na wanajamii, Shirika la Search for Common Ground lenye makao yake makuu Dar es Salaam, sasa limejikita wilayani Tarime ili kutafuta suluhu.
Meneja Programuwa shirika hilo, Patricia Loreskar alisema kazi kubwa ya shirika hilo ni kujenga mazingira ya mawasiliano na mijadala kwenye mazingira yenye migogoro.
Naye Meneja wa mradi wilayani Tarime, Jacob Malikuza alisema njia wanazotumia ni pamoja na kufanya utafiti wa maisha ya wanajamii kabla ya kuanza kutoa mafunzo.
Kwa upande wake Mwanasheria wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Harold Sungusia anasema wamekuwa wakifuatilia mgogoro katika eneo hilo na wamefungua kesi London, Uingereza ili kuishitaki African Barrick Gold kwa ukiukwaji wa haki za binadamu.
Taarifa zaidi zinaonyesha pia kampuni ya uwakili ya Leigh Day nayo inahusika katika kesi hiyo ikiwawakilisha baadhi ya wanavijiji wanaozunguka mgodi huo, kutokana na matumizi ya nguvu kupita kiasi.
Kesi hiyo iliyofunguliwa mwishoni mwa mwaka jana, ilipingwa na ABG wakitaka iendeshwe Tanzania, lakini walishindwa katika pingamizi lao.
“Huo mgogoro tumeufuatilia sana, hadi sasa tumeshafungua kesi Uingereza.Hatukufungulia Tanzania kwa sababu mahakama zetu zinachelewesha mno kesi na mara nyingine hazitufikishi kwenye kupata haki,” alisema Sungusia.
Hata hivyo Amani Mustafa ambaye ni mwanzilishi na Mkurugenzi wa taasisi ya Haki Madini alisema ni watu wachache mno wenye uelewa na masuala ya sheria hadi kufikia kufungua kesi.
“Watu wachache sana wanaweza kupeleka kesi mahakamani. Kwanza kuna mazingira ya kutishana na kutokuaminiana. Isitoshe wengi hawaoni kama mahakama ndiyo suluhisho la mambo yao. Kwa kifupi wamepoteza imani na Serikali na mfumo mzima wa mahakama. Wanachoamini haki inapatikana mikononi mwao,” alisema Mustafa na kuongeza:
“Kuna mambo mengi mno kwenye mgodi ule; mauaji, unyanyasaji wa kijinsia, uchafuzi wa maji, kutofuatwa kwa taratibu za kazi mgodini na hata vyama vya wafanyakazi vinalalamika”.
Akizungumzia mfumo wa kushughulikia malalamiko, Mustafa alisema kutoelimika kwa wanavijiji ndiyo sababu kubwa ya kukosa haki.
“Kungetakiwa kutolewe elimu ya sheria kwa wanavijiji na mwelimishaji asilipwe na Barrick. Kwa sasa kuna ukiukwaji wa maadili na Serikali haina muda, bali imejikita kwenye ukusanyaji wa kodi kuliko kuangalia haki za watu,” alisema Mustafa.



Waandishi wa Kampuni ya Mwananchi waanza mafunzo maalum

 Afisa raslimali watu kampuni ya Mwananchi Comm.Ltd,Aika akitoa mada kwawaandishi wa habari wa kampuni hiyo wa mikoa ya kanda ya ziwa na Magharibi ,ukumbi wa g&g jijini Mwanza
 Tunataka mfikie malengo ya kampuni,anasisitiza
 msisitizo
 Tuko tayari kufikia malengo ,wanasema waandishi
 Tumekuelewa ,na tutafikia malengo ya kampuni




Tawla kutumia wanasheria 400 kutatua migogoro ya ardhi vijijini




Na Hadija Jumanne, Mwananchi

Posted  Ijumaa,Februari28  2014  saa 14:31 PM
Kwa ufupi


 Juma Nyamhanga(36)mkazi wa kijiji cha Nyamitita wilayani Serengeti akiwa hospitali Teule ya Wilaya ya Serengeti,kufuatia kukatwa mkono kutokana na mgogoro wa ardhi-picha na Mayunga Blog

  • Lengo la chama hiki ni kutoa msaada kwa watoto, wanawake na watu mbalimbali.”

Kila kukicha kumekuwa na kesi za migogoro ya ardhi, mirathi na hata kesi za wazazi kuozesha watoto wao yaani mimba za utotoni na ndoa za utotoni na hii ni changamoto kubwa inayoikabili nchi kwa sasa.
Utafiti uliofanywa hivi karibuni na Chama cha waandishi wa habari wanawake (TAMWA) umeonyesha kuwa katika kipindi cha mwaka 2012/2013 jumla ya matukio 228 ya mimba  na matukio  42 ya  ndoa za utotoni  yaliripotiwa huko Pemba na wilaya ya kati Unguja.
Hata hivyo, mimba na ndoa za utotoni  zimetajwa kuwa ni miongoni mwa vikwazo vinavyowapata watoto wa kike  kwamba tatizo hilo bado ni kubwa kwa baadhi ya maeneo ya Tanzania Bara na Visiwani.
Wakati  Tanzania Visiwani  hali ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto ikionekana zaidi katika Mkoa wa Kusini Pemba na Wilaya ya Kati Unguja, upande wa Tanzania bara  maeneo yenye ukatili dhidi ya wanawake pamoja na mimba za utotoni yanaonekana katika wilaya za  Kahama, Tarime, Sengerema, Newala, Mbulu, Bunda, Nkasi, Babati, Chunya, Dodoma, Bariadi, Busega na Singida vijijini.
Bokhe Odhiambo (31), mkazi wa Tarime mkoani Mara, anasema vitendo vya ukatilli dhidi ya wanawake ndani ya ndoa na mimba za utoto kwa watoto wa kike ni mambo ya kawaida  na jamii wala haina muda wa kuyakemea.
“Kupigwa au kufanyiwa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake ndani ya ndoa, migogoro ya ardhi na mimba za utotoni kwa watoto wa kike ni mambo ya kawaida tu kwenye jamii yetu licha ya wasaidizi wa kisheria kutoa elimu,” alisema Odhiambo.
Kutokana na changamoto hiyo, Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (Tawla) kimejitosa kutoa msaada wa kisheria katika mikoa yenye changamoto lengo likiwa ni  kupunguza tatizo hilo.
Mwenyekiti wa  Chama cha Wanawake Wanasheria Tanzania (TAWLA), Aisha Bade anasema kutokana na ukubwa wa tatizo hilo chama chake kimeamua kusambaza  wasaidizi wa kisheria  400 nchi nzima  lengo likiwa ni kusaidia kutatua migogoro ya ardhi na mirathi.
Bade anasema Tawla imebaini kuwa mikoa ya  Pwani na Morogoro, Mtwara, Lindi, Arusha , Tanga, Shinyanga, Manyara na Mwaza  inaongoza kwa kuwa na migogoro ya  mirathi, vitendo vya ukatili na  kuozesha watoto katika  ndoa za utotoni.
Anasema kuwa mbali na mikoa hiyo pia mikoa ya  Tanga, Arusha, Dodoma inaongoza kwa kuwa na migogoro ya ardhi pamoja na mirathi na hivyo juhudi mbalimbali zinahitajika kukabiliana na tatizo hilo. “Tumesambaza wasaidizi wa kisheria 400 nchi nzima  lengo ni kutatua migogoro iliyopo hasa katika maeneo ya vijijini ambayo tumeona hayana msaada wa kisheria” anasema Bade.
“Mbali na  mikoa hiyo pia mikoa ya  Tanga, Arusha, Dodoma nayo ni miongoni mwa mikoa  inayoongoza kwa kuwa na changamoto kubwa ya  migogoro ya ardhi na miradhi na kwamba  juhudi za pamoja  zinahitajika kushirikia katika kutatua changamoto hiyo ili kupunguza madhara yanayoweza kutokea kutokana na tatizo hilo”anasema Beda.
Anasema TAWLA ilianza mafunzo ya wasaidizi wa sheria mwaka 2006 na kutokana mafunzo hayo zaidi ya wananchi 4,600 wamenufaika kwa kupata msaada wa kisheria  vijijini katika kipindi cha mwaka jana pekee.
“Lengo la TAWLA kuanzisha mradi wa mafunzo  ni kuwapatia haki wananchi ambao hawana  uwezo wa kuwa na mawakili katika kushughulikia migogoro ya ardhi na miradhi na kwamba chama chetu kiliamua kuanzisha mradi huu kutokana  na nchi kukabiliwa na uhaba wa wanasheria  na mawakili na hivyo kuwa vigumu kwa watu wa vijijini kupata msaada wa kisheria katika kutatua matatizo yao,”alisema Beda.
Pia Beda  anasema  kuwa  ripoti  inaonyesha   hadi  sasa   wasaidizi  wakisheria   wameweza  kuwafikia  watu   6,000  pamoja  na  kutoa  elimu  kuhusu   sheria  na  haki   za  binadamu.
Anasema mpaka sasa chama hicho kimeshapokea  zaidi ya kesi 700 za usuluhishi wa ndoa , migogoro ya ardhi, migogoro ya miradhi na madai mbalimbali yanayotokana na matunzo ya watoto na hivyo kuzipatia msaada wa kisheria.
 “Licha ya kusambaza wasaidizi wa kisheria vijijini  bado nchi inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa wataalamu hao  kutokana na mahitaji kuwa makubwa kuliko idadi ya wataalamu wa masuala ya kisheria,”anasema.
Nasieku  Kisambu, ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Tawla, anasema licha ya kupeleka wasaidizi hao wa kisheria vijijini bado kuna changamoto ya uhaba wa wasaidizi wa kisheria nchini kutokana na mahitaji yaliyopo.
Kisambu anataja  mikoa yenye  wasaidizi wa kisheria kuwa ni Dodoma yenye wasaidizi 98, Morogoro 12, Katavi 73, Dar es Salaam 22, Pwani 8, Arusha 154 na Tanga  wasaidizi 45 ambao watatoa huduma hiyo kwa jamii bila gharama yoyote.
Kisambu anasema maeneo  yatakayonufaika na huduma hiyo ni yale ya vijiji ambayo jamii imeshindwa kupata haki  zao stahiki kutokana na kukosa msada wa kisheria na uhaba wa fedha kwa ajili ya kutafuta mawakili katika kusimamia kesi zao.
“Lengo la kuwepo kwa chama hiki  ni kutoa msaada wa kisheria kwa watoto, wanawake  na watu wenye matatizo mbalimbali ambayo ni migogoro ya ardhi na  mirathi”anasema Kisambu.
Kisambu anasema kutokana na uelewa mdogo wa masuala ya elimu juu ya unyanyasaji na ukatili kumekuwa na matukio ya mara kwa mara wanayofanyiwa wanawake na watoto lakini kupitia  wasaidizi wa kisheria wataweza  kutatua migogoro iliyopo nchini.
“Mikoa kama Morogoro, Mtwara, Lindi, Arusha , Tanga, Shinyanga, Manyara na Mwaza  inaongoza kwa kuwa na migogoro ya  mirathi, vitendo vya Ukatili na  kuozesha watoto katika  ndoa za utotoni na hali hii ya kuoza watoto wadogo inatokana na wazazi kutokuwa na uwezo wa kuwaendeleza watoto wao kielimu nan a badala yake huona kuwa badala ya mtoto kupata mimba akiwa nyumbani baada ya kumaliza darasa la saba ni bora aolewe ili kuondoa aibu”anasema Kisambu na kuongeza .
“Mwamko mdogo kwa baadhi ya jamii juu ya umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike unaendelea kukwamisha maendeleo ya wanawake na kuupa kipaumbele mfumo dume ambao kwa miaka mingi unapigwa vita na mataifa yote ulimwenguni” alisema Kisambu.
Kwanini migogoro ya ardhi.
Kaimu  Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na nyumba ya wilaya nchini, Jane Kapongo anasema ufinyu wa bajeti ya serikali  kwa wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya makazi ni moja kati ya changamoto inayochangia kuendelea kwa migogoro ya ardhi nchini.
Kapongo anasema katika  kipindi cha mwaka 2012 na 2013 watu  58393 waliopata hati baada ya kupimwa viwanja vyao  nchi nzima na kwamba  jukumu la wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ni kusimamia  sera  na kuweka miongozo ya matumizi ya ardhi pamoja na  kutatua migogoro.
Anasema  hadi Desemba mwaka 2011  wizara hiyo ilikuwa  imepokea asilimia 27.8 ya fedha zilizoidhinishwa kwa mwaka wa fedha 2011/12 hivyo kushindwa utekelezajiwa majukunu yake kwa ufanisi.
“Halmashauri nyingi hazitengewi bajeti  na hali hii inasababisha migogoro kutokana na  kiasi kidogo kinachotolewa katika bajeti  hakikidhi ulipaji wa fidia kwa wananchi, kushindikana upimaji viwanja, uendelezaji miji hushindwa kufanyika kwa sababu ya uhaba wa fedha na hatimaye  kusababisha migogoro”Anasema  Kapongo.
Anasema   jukumu la kupima na kugawa viwanja  linafanywa na  mamlaka za serikali za mitaa ambazo ni Halmashauri za wilaya, Miji, Manispaa na Majiji hivyo wizara  imekuwa ikijikita katika kusimamia sera na kuweka miongozo ya matumizi ya ardhi  na utatuzi wa  migogoro inayoibuka kila  mara.
Kapongo anataja  baadhi ya migogoro mikubwa ya ardhi iliyopo nchini kuwa ni migogoro kati ya jamii za wakulima na wafugaji,  wanavijiji na wawekezaji, migogoro ya mipaka baina ya mamlaka mbalimali na wamiliki wawili katika kiwanja kimoja.
“Migogoro mingine ni Uvamizi wa mashamba na viwanja,  wananchi kutoridhika na fidia inayolipwa wakati wa utwaaji ardhi na hali hiyo inatokana na elimu duni kwa jamii kuhusiana na  sheria, kanunia na taratibu za utawala wa ardhi”anasema Kapongo.
Anafafanua zaidi kuwa ukosefu wa uadilifu  kwa baadhi ya watendaji katika sekta  ya ardhi, upungufu wa watendaji na  vitendea kazi pamoja na utunzaji hafifu ya kumbukumbu ni moja kati ya sababu  inayochangia migogoro ya ardhi nchini.
Jinsi ya utatuzi wa migogoro ya ardhi unavyofanyika:
Kaimu Mkurugenzi wa Tawla, Nasieku Kisambu anasema sheria  ya mahakama za ardhi ya mwaka 2002 imeweka utaratibu na muundo mpya wa utatuzi wa migogoro ya ardhi nchini.
Miongoni mwa utatuzi huo ni kuwa na baraza la ardhi la kijiji ambalo jukumu lake ni  kusuluhisha migogoro ya ardhi inayotokea hapo kijiji.
Vile vile katika utatuzi huo wa migogoro ya ardhi lazima kuwe na baraza la ardhi la kata na baraza la ardhi  na nyumba la wilaya ambalo limeundwa na waziri anayehusika na masuala ya ardhi.
“Mabaraza haya yanatakiwa kuwepo katika ngazi zote za wilaya ili kuhakikisha huduma stahiki kwa wananchi inatolewa na kwamba kazi ya baraza hili ni kusikiliza  rufaa kutoka baraza la kata, kusikiliza mashauri mbalimbali ya ardhi kwa mujibu wa sheria  za ardhi pamoja na kusimia utekelezaji wa maamuzi yake”anasema Kisambu.
Nini kifanyike?
Kapongo anasema serikali iongeze banjeti kwa wizara hiyo ili kuwepo na wataalamu watakao weza kuwafikia wananchi wa vijijini na kutatua migogoro pamoja na kuwepo kwa  uadilifu  kwa baadhi ya watendaji katika sekta  ya ardhi na kuongeza  watendaji na  vitendea kazi katika maeneo husika.
Vile vile kutolewe elimu itakayosaidia kupunguza changamoto hiyo kwani migogoro mingi ya ardhi inatokana na kutoridhika na fidia inayolipwa wakati wa utwaaji ardhi na hali hiyo inatokana na elimu duni kwa jamii kuhusiana na  sheria, kanunia na taratibu za utawala wa ardhi.
Vile vile kwa upande wa ukatili, Beda anasema  licha ya kuwepokwa sheria zinazobidhitihali hiyo bado kuna changamoto ya uhaba wa wasaidizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali ya nchi.




MJAMZITO WA MIEZI 9 AKATWA MGUU KISHA KUWEKEWA TINDIKALI






Anna Sabai aliyefanyiwa ukatili na mmewe,
Na Anthony Mayunga-Mwananchi.
machi,2014.
Serengeti:“NI zaidi ya miezi sita toka nifanyiwe ukatili na mme wangu na mama mkwe….nahangaika kuuguza mguu niliokatwa panga  kisha nikawekea maji ya betri … sijui kama utapona… kichanga nacho kinasumbua ,jamani nimekosa nini mimi kwa Mungu”
Ni maneno yenye kutia simanzi na ambayo yanaamsha kilio ya Anna Sabai(20)mkazi wa kitongoji cha Manyata kijiji cha Nyamakendo kata ya Mbalibali wilayani Serengeti,ambaye anapasa sauti akiuliza ,wako wapi watetezi wa akina mama ,maana kwa hali aliyonayo anahitaji msaada.
Ukatili aliofanyiwa Anna mama wa watoto wawili katika ndoa yake yenye migogoro na mmewe Hamisi Sabai (20)unazidi kuuweka mkoa wa Mara kwenye taswira mbaya  ,kwa matukio ya ukatili wa wanawake.
Kwa nini analalama?
Agosti mosi ,2013 ikiwa ni tarehe ambayo wakazi wa wilaya hiyo humiminika mnadani ,akiwa ni mjamzito wa miezi  9,akihesabu siku tu kwa ajili ya kujifungua, aliamriwa na mme wake kwenda kuchunga ng’ombe,bila kujali hali aliyokuwa nayo.
“Kwa kweli nilikuwa na hali mbaya sana…nikiwa machungani nilikaa chini ya kivuli huku ng’ombe wanachunga….hali ilivyozidi kuwa mbaya nikalala usingizi hapo….alipokuja mme wangu akakuta nimelala…akaanza kunishambulia kwa kipigo ,akidai kuwa nilikuwa na mwanamme …mapenzi yamenoga hadi nikasinzia na kuacha ng’ombe wanachunga wenyewe”anasema kwa masikitiko.
Anasema pamoja na kujieleza na kwa kuzingatia hali yake,walipofika nyumbani mama mke wake Bhoke Sabai alizidi kumchochea kijana wake kuwa  nilikuwa na mwanaume ,natakiwa kupewa kipigo ili nikome.
“Pamoja na kuwa wakati ananipiga sikuwa najitetea kujibu mapigo….lakini akaona aache fimbo akachukua panga na kunikata mguu wa kushoto …niliumia sana ,huku ujauzito…nikawa natamani kufa,maana hali ilikuwa mbaya…sina msaada,kisha nikafungiwa ndani ili watu wasijue  ,wala hakuna kwenda kutibiwa,”anabainisha huku akitokwa machozi.
Ili kuzuia damu isitoke amwagiwa tindikali.
Anna huku amebeba mtoto wake kutembea kwake kwa shida anasema,ili watu wasije kujua unyama aliotendewa walileta maji ya betri na kumwagia kwenye kidonda,”hakika maumivu yalikuwa zaidi ya uchungu wa kujifungua,nilifikia hatua kama ningepata kitu cha kujimaliza ningekufa….huku nasumbuliwa na mimba …naumizwa hivi…jamani wanaharakati wanaotetea wanawake wako wapi…maana nitakatwa mguu hivihivi”anasema na kuibua simanzi.
Matokeo yake mguu ukaoza ,kwa kuwa alikaa ndani muda mrefu ,ndugu zake hawaambiwi,huku mama mkwe wake akimkejeri kila wakati,na kuwa hajaona watu wenye roho ya kikatili kama hao,kwa kuwa walilenga kumuua bila kosa.
Aokolewa na Mama yake mzazi.
Anasema kuwa akiwa amekata tamaa kwa kuwa alikuwa anafungiwa ndani mara kwa mara majilani wasijue,lakini kuna wakati alilazimika kumlilia Mungu,kwa nini afe bila ndugu zake kumwona,ndipo bila kutarajia alistua mama yake mzazi Mnanka Chacha(48)akifika hapo  baada ya kutaarifiwa na majilani.
“Nilipomwona Mama nikasema basi sasa hata kama nikifa …niko mikono salama,huenda maiti yangu itapewa heshima kama binadamu…maana kama ningefia mkononi mwa hao  huenda maiti ingetupwa kama mbwa….nilijisikia ahueni kwa kumuona mama”anabainisha.
Afikishwa hospitali kwa matibabu.
Anasema kwa kupitia polisi mama yake alimfikisha hospitali Teule ya Nyerere kwa ajili ya matibabu ,madaktari walipomwona walimwambia kuwa hawana uwezo tena wa kumtibu kwa hali aliyonayo wakamwandikia barua kwenda hospitali ya rufaa ya Bugando.
Akosa pesa .
Kutokana na ukata wake na mama yake ,alishindwa kwenda Bugando na kuamua kurudi nyumbani kwake kwa ajili ya kutafuta wasamaria wema ili aweze kwenda Bugando kwa ajili ya matibabu.
Mme achana barua ya rufaa.
Katika kuhakikisha juhudi za kupelekwa hospitali hazizai matunda ,akiamini kuwa mme wake alikuwa ameishajirudi alimpa barua ya rufaa ili watafute fedha za matibabu,lakini yeye akaichana,akawa hana jinsi ya kufanya.
“Alichana barua ya rufaa…ikawa sina namna yoyote ya kwenda kutibiwa hospitali ya rufaa ya Bugando….ikabidi nikae tu nyumbani nikiangalia mguu wangu unaoza….kwa kweli nahitaji msaada kwa watu wanaoguswa maana kula yangu hata ya mtoto ni ya shida…siweze kwenda zaidi ya hapa”anasema.
Anabainisha kuwa alichana barua huku akilalama kuwa nimetoa siri polisi na kwa watu wengine hivyo ili kunikomoa akaona aichane ili kupoteza ushahidi.
Ajifungua mtoto wa kiume.
Agosti 24,2013 ikiwa ni siku 24 toka amefanyiwa ukatili na mme wake alijifungua mtoto wake wa pili wa kiume ambaye anazunguka naye katika hali aliyonayo,na kama si  msaada wa wasamaria  wema  kumpeleka dispensari ya Machochwe huenda angepata shida zaidi,lakini mme wake hakuwa na mpango wowote.
“Hakuna matumizi mme wangu anayotoa  kwangu na kwa mtoto….dada kwa kuona hali hiyo amenichukua niko kwake mtaa wa bomani mjini Mugumu na mwanangu huyu…maana yule wa kwanza alifariki”anabainisha.
Anawaomba wanawake wanaofanyiwa ukatili wafike polisi kutoa taarifa kwa kuwa kwa tatizo lake amebaini kuwa askari wa dawati la jinsia akimtaja kwa jina la Sijali amekuwa kama ndugu,anamnunulia dawa na amehangaika naye kwa muda mrefu bila kuchoka.
Diwati la jinsia wajitosa kuwasaka watuhumiwa.
Katibu wa dawati la jinsia polisi wilaya ya Serengeti Sajenti Sijali Nyambuche anasema kwa muda mrefu wamekuwa wakiwasaka watuhumiwa ,lakini wanakosa ushirikiano kutoka kwa jamii ikiwemo baadhi ya viongozi.
“Tukajifanya kusahau,nao wakajisahau wakaendelea na maisha ikiwemo kilimo cha tumbaku,na tukafanikiwa kuwakamata kirahisi ,mama na mtoto kwa tuhuma za kujeruhi”anasema Sijali.
Anasema wamefungulia jalada namba MUG/DAW/IR/30/2014 kwa tuhuma za kusababisha dhara .
Afanyiwa uchunguzi tena.
Katibu wa dawati analazimika kumfikisha hospitali ili kujua hatima ya mguu huo, kama unatibika ama kukatwa.
Daktari adai misuli ilivurugwa.
Dk.Richard wa hospitali teule ya Nyerere anasema baada ya kupiga picha ya Xray wamebaini kuwa mishipa haikukatwa wakati wa shambulio hilo,bali kuna misuli iliyoharibiwa ,kutokana na hali hiyo mguu huo utakuwa kama mwenye ugonjwa wa matende.
“Ni bora akabaki hivyo,akawa anapata dawa inapotokea maumivu…kwa kuwa vidole havichezi vimeisha kufa ganzi …maana zaidi ya hapo ni kukata mguu atapata ulemavu na maumivu mapya….nashauri anapokuwa anahisi hali tofauti aje apate dawa kuliko kukatwa mguu”anashauri Dk.
Mme ajifanya amezimia asitoe maelezo.
Sabai katika hali ya kushangaza baada ya kukamatwa na kulala mahabusu na mama yake anapotakiwa kutoa maelezo ,ghafla anaanguka na kujifanya amezimia,hata hivyo haikumsadia alipozinduka akatoa maelezo huku akidai kuwa mke wake alilala na mwanamme mwingine  ambaye hakumtaja na kuacha ng’ombe wanazunguka.
Lakini anakana kuwa hakumwekea maji ya betri kwenye kidonda,huku akishindwa kueleza kwa nini alimkata na kushindwa kumpeleka hospitali,na kuchana barua ya rufaa kwenda Bugando kwa matibabu.
Mama yake alidai yeye hakuhusika na ukatili huo.
Wanaharakati.
Mratibu wa kitengo cha kuzuia ukatili wa kijinsia kupitia CCT wilayani Serengeti,Sophia Mchonvu,anasema matukio ya ukatili wa kijinsia yameshika kasi wilayani hapo,na kuomba vyombo husika kutoa adhabu kali ili liwe fundisho .
Matukio mengine.
Mwaka 2000 Kadogo Waya alipigwa na mme wake kutokana na wivu wa mapenzi kisha akamwagia tindikali na miguu ikaoza na kupelekea kukatwa miguu yote,hivi karibu mkazi mmoja wa kijiji cha Bisarara wilayani hapa alimjeruhi vibaya mke wake na kung’ata mtoto kisa kikiwa ni kugoma kwenda kuchunga ng’ombe usiku ndani ya hifadhi ya Taifa ya Serengeti,n
Mawasiliano kwa atakayeguswa,0759891849,0787239480,au 0684518319 Katibu wa dawati la jinsia.
Mwisho.

VINARA WA AFYA