Na Hadija Jumanne, Mwananchi
Posted Ijumaa,Februari28 2014 saa 14:31 PM
Posted Ijumaa,Februari28 2014 saa 14:31 PM
Kwa ufupi
Juma Nyamhanga(36)mkazi wa kijiji cha Nyamitita wilayani Serengeti akiwa hospitali Teule ya Wilaya ya Serengeti,kufuatia kukatwa mkono kutokana na mgogoro wa ardhi-picha na Mayunga Blog
- Lengo la chama hiki ni kutoa msaada kwa watoto, wanawake na watu mbalimbali.”
Kila kukicha kumekuwa na kesi za
migogoro ya ardhi, mirathi na hata kesi za wazazi kuozesha watoto wao yaani
mimba za utotoni na ndoa za utotoni na hii ni changamoto kubwa inayoikabili
nchi kwa sasa.
Utafiti uliofanywa hivi karibuni na
Chama cha waandishi wa habari wanawake (TAMWA) umeonyesha kuwa katika kipindi
cha mwaka 2012/2013 jumla ya matukio 228 ya mimba na matukio 42
ya ndoa za utotoni yaliripotiwa huko Pemba na wilaya ya kati
Unguja.
Hata hivyo, mimba na ndoa za
utotoni zimetajwa kuwa ni miongoni mwa vikwazo vinavyowapata watoto wa
kike kwamba tatizo hilo bado ni kubwa kwa baadhi ya maeneo ya Tanzania
Bara na Visiwani.
Wakati Tanzania Visiwani
hali ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto ikionekana zaidi katika Mkoa wa
Kusini Pemba na Wilaya ya Kati Unguja, upande wa Tanzania bara maeneo
yenye ukatili dhidi ya wanawake pamoja na mimba za utotoni yanaonekana katika
wilaya za Kahama, Tarime, Sengerema, Newala, Mbulu, Bunda, Nkasi, Babati,
Chunya, Dodoma, Bariadi, Busega na Singida vijijini.
Bokhe Odhiambo (31), mkazi wa Tarime
mkoani Mara, anasema vitendo vya ukatilli dhidi ya wanawake ndani ya ndoa na
mimba za utoto kwa watoto wa kike ni mambo ya kawaida na jamii wala haina
muda wa kuyakemea.
“Kupigwa au kufanyiwa vitendo vya
ukatili dhidi ya wanawake ndani ya ndoa, migogoro ya ardhi na mimba za utotoni
kwa watoto wa kike ni mambo ya kawaida tu kwenye jamii yetu licha ya wasaidizi
wa kisheria kutoa elimu,” alisema Odhiambo.
Kutokana na changamoto hiyo, Chama
cha Wanasheria Wanawake Tanzania (Tawla) kimejitosa kutoa msaada wa kisheria
katika mikoa yenye changamoto lengo likiwa ni kupunguza tatizo hilo.
Mwenyekiti wa Chama cha
Wanawake Wanasheria Tanzania (TAWLA), Aisha Bade anasema kutokana na ukubwa wa
tatizo hilo chama chake kimeamua kusambaza wasaidizi wa kisheria
400 nchi nzima lengo likiwa ni kusaidia kutatua migogoro ya ardhi na
mirathi.
Bade anasema Tawla imebaini kuwa
mikoa ya Pwani na Morogoro, Mtwara, Lindi, Arusha , Tanga, Shinyanga,
Manyara na Mwaza inaongoza kwa kuwa na migogoro ya mirathi, vitendo
vya ukatili na kuozesha watoto katika ndoa za utotoni.
Anasema kuwa mbali na mikoa hiyo pia
mikoa ya Tanga, Arusha, Dodoma inaongoza kwa kuwa na migogoro ya ardhi
pamoja na mirathi na hivyo juhudi mbalimbali zinahitajika kukabiliana na tatizo
hilo. “Tumesambaza wasaidizi wa kisheria 400 nchi nzima lengo ni kutatua
migogoro iliyopo hasa katika maeneo ya vijijini ambayo tumeona hayana msaada wa
kisheria” anasema Bade.
“Mbali na mikoa hiyo pia mikoa
ya Tanga, Arusha, Dodoma nayo ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa
kuwa na changamoto kubwa ya migogoro ya ardhi na miradhi na kwamba
juhudi za pamoja zinahitajika kushirikia katika kutatua changamoto hiyo
ili kupunguza madhara yanayoweza kutokea kutokana na tatizo hilo”anasema Beda.
Anasema TAWLA ilianza mafunzo ya
wasaidizi wa sheria mwaka 2006 na kutokana mafunzo hayo zaidi ya wananchi 4,600
wamenufaika kwa kupata msaada wa kisheria vijijini katika kipindi cha
mwaka jana pekee.
“Lengo la TAWLA kuanzisha mradi wa
mafunzo ni kuwapatia haki wananchi ambao hawana uwezo wa kuwa na
mawakili katika kushughulikia migogoro ya ardhi na miradhi na kwamba chama
chetu kiliamua kuanzisha mradi huu kutokana na nchi kukabiliwa na uhaba
wa wanasheria na mawakili na hivyo kuwa vigumu kwa watu wa vijijini
kupata msaada wa kisheria katika kutatua matatizo yao,”alisema Beda.Pia Beda anasema kuwa ripoti inaonyesha hadi sasa wasaidizi wakisheria wameweza kuwafikia watu 6,000 pamoja na kutoa elimu kuhusu sheria na haki za binadamu.
Anasema mpaka sasa chama hicho kimeshapokea zaidi ya kesi 700 za usuluhishi wa ndoa , migogoro ya ardhi, migogoro ya miradhi na madai mbalimbali yanayotokana na matunzo ya watoto na hivyo kuzipatia msaada wa kisheria.
“Licha ya kusambaza wasaidizi wa kisheria vijijini bado nchi inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa wataalamu hao kutokana na mahitaji kuwa makubwa kuliko idadi ya wataalamu wa masuala ya kisheria,”anasema.
Nasieku Kisambu, ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Tawla, anasema licha ya kupeleka wasaidizi hao wa kisheria vijijini bado kuna changamoto ya uhaba wa wasaidizi wa kisheria nchini kutokana na mahitaji yaliyopo.
Kisambu anataja mikoa yenye wasaidizi wa kisheria kuwa ni Dodoma yenye wasaidizi 98, Morogoro 12, Katavi 73, Dar es Salaam 22, Pwani 8, Arusha 154 na Tanga wasaidizi 45 ambao watatoa huduma hiyo kwa jamii bila gharama yoyote.
Kisambu anasema maeneo yatakayonufaika na huduma hiyo ni yale ya vijiji ambayo jamii imeshindwa kupata haki zao stahiki kutokana na kukosa msada wa kisheria na uhaba wa fedha kwa ajili ya kutafuta mawakili katika kusimamia kesi zao.
“Lengo la kuwepo kwa chama hiki ni kutoa msaada wa kisheria kwa watoto, wanawake na watu wenye matatizo mbalimbali ambayo ni migogoro ya ardhi na mirathi”anasema Kisambu.
Kisambu anasema kutokana na uelewa mdogo wa masuala ya elimu juu ya unyanyasaji na ukatili kumekuwa na matukio ya mara kwa mara wanayofanyiwa wanawake na watoto lakini kupitia wasaidizi wa kisheria wataweza kutatua migogoro iliyopo nchini.
“Mikoa kama Morogoro, Mtwara, Lindi, Arusha , Tanga, Shinyanga, Manyara na Mwaza inaongoza kwa kuwa na migogoro ya mirathi, vitendo vya Ukatili na kuozesha watoto katika ndoa za utotoni na hali hii ya kuoza watoto wadogo inatokana na wazazi kutokuwa na uwezo wa kuwaendeleza watoto wao kielimu nan a badala yake huona kuwa badala ya mtoto kupata mimba akiwa nyumbani baada ya kumaliza darasa la saba ni bora aolewe ili kuondoa aibu”anasema Kisambu na kuongeza .
“Mwamko mdogo kwa baadhi ya jamii juu ya umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike unaendelea kukwamisha maendeleo ya wanawake na kuupa kipaumbele mfumo dume ambao kwa miaka mingi unapigwa vita na mataifa yote ulimwenguni” alisema Kisambu.
Kwanini migogoro ya ardhi.
Kaimu Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na nyumba ya wilaya nchini, Jane Kapongo anasema ufinyu wa bajeti ya serikali kwa wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya makazi ni moja kati ya changamoto inayochangia kuendelea kwa migogoro ya ardhi nchini.
Kapongo anasema katika kipindi cha mwaka 2012 na 2013 watu 58393 waliopata hati baada ya kupimwa viwanja vyao nchi nzima na kwamba jukumu la wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ni kusimamia sera na kuweka miongozo ya matumizi ya ardhi pamoja na kutatua migogoro.
Anasema hadi Desemba mwaka 2011 wizara hiyo ilikuwa imepokea asilimia 27.8 ya fedha zilizoidhinishwa kwa mwaka wa fedha 2011/12 hivyo kushindwa utekelezajiwa majukunu yake kwa ufanisi.
“Halmashauri nyingi hazitengewi bajeti na hali hii inasababisha migogoro kutokana na kiasi kidogo kinachotolewa katika bajeti hakikidhi ulipaji wa fidia kwa wananchi, kushindikana upimaji viwanja, uendelezaji miji hushindwa kufanyika kwa sababu ya uhaba wa fedha na hatimaye kusababisha migogoro”Anasema Kapongo.
Anasema jukumu la kupima na kugawa viwanja linafanywa na mamlaka za serikali za mitaa ambazo ni Halmashauri za wilaya, Miji, Manispaa na Majiji hivyo wizara imekuwa ikijikita katika kusimamia sera na kuweka miongozo ya matumizi ya ardhi na utatuzi wa migogoro inayoibuka kila mara.
Kapongo anataja baadhi ya migogoro mikubwa ya ardhi iliyopo nchini kuwa ni migogoro kati ya jamii za wakulima na wafugaji, wanavijiji na wawekezaji, migogoro ya mipaka baina ya mamlaka mbalimali na wamiliki wawili katika kiwanja kimoja.
“Migogoro mingine ni Uvamizi wa mashamba na viwanja, wananchi kutoridhika na fidia inayolipwa wakati wa utwaaji ardhi na hali hiyo inatokana na elimu duni kwa jamii kuhusiana na sheria, kanunia na taratibu za utawala wa ardhi”anasema Kapongo.
Anafafanua zaidi kuwa ukosefu wa uadilifu kwa baadhi ya watendaji katika sekta ya ardhi, upungufu wa watendaji na vitendea kazi pamoja na utunzaji hafifu ya kumbukumbu ni moja kati ya sababu inayochangia migogoro ya ardhi nchini.
Jinsi ya utatuzi wa migogoro ya ardhi unavyofanyika:
Kaimu Mkurugenzi wa Tawla, Nasieku Kisambu anasema sheria ya mahakama za ardhi ya mwaka 2002 imeweka utaratibu na muundo mpya wa utatuzi wa migogoro ya ardhi nchini.
Miongoni mwa utatuzi huo ni kuwa na baraza la ardhi la kijiji ambalo jukumu lake ni kusuluhisha migogoro ya ardhi inayotokea hapo kijiji.
Vile vile katika utatuzi huo wa migogoro ya ardhi lazima kuwe na baraza la ardhi la kata na baraza la ardhi na nyumba la wilaya ambalo limeundwa na waziri anayehusika na masuala ya ardhi.
“Mabaraza haya yanatakiwa kuwepo
katika ngazi zote za wilaya ili kuhakikisha huduma stahiki kwa wananchi
inatolewa na kwamba kazi ya baraza hili ni kusikiliza rufaa kutoka baraza
la kata, kusikiliza mashauri mbalimbali ya ardhi kwa mujibu wa sheria za
ardhi pamoja na kusimia utekelezaji wa maamuzi yake”anasema Kisambu.
Nini kifanyike?
Kapongo anasema serikali iongeze
banjeti kwa wizara hiyo ili kuwepo na wataalamu watakao weza kuwafikia wananchi
wa vijijini na kutatua migogoro pamoja na kuwepo kwa uadilifu kwa
baadhi ya watendaji katika sekta ya ardhi na kuongeza watendaji
na vitendea kazi katika maeneo husika.
Vile vile kutolewe elimu
itakayosaidia kupunguza changamoto hiyo kwani migogoro mingi ya ardhi inatokana
na kutoridhika na fidia inayolipwa wakati wa utwaaji ardhi na hali hiyo
inatokana na elimu duni kwa jamii kuhusiana na sheria, kanunia na
taratibu za utawala wa ardhi.
Vile vile kwa upande wa ukatili,
Beda anasema licha ya kuwepokwa sheria zinazobidhitihali hiyo bado kuna
changamoto ya uhaba wa wasaidizi wa kisheria katika maeneo mbalimbali ya nchi.