Katika kukabiliana na vitendo vya ujangili vinavyoendelea kushika
kasi ndani nan je ya mipaka ya nchi yetu, Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA)
litaendeshwa katika mfumo wa jeshi-usu katika siku chache zijazo ambapo
watumishi wake watalazimika kupitia katika mafunzo maalum ya kijeshi.
Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA aliyasema hayo mwishoni mwa wiki alipokuwa
akifunga rasmi mafunzo ya askari wapya 96 walioajiriwa na TANAPA na kuhudhuria
mafunzo ya miezi minne katika Hifadhi ya Taifa Katavi mwishoni mwa wiki.
Kijazi alisema kuwa TANAPA imeanzisha utaratibu mpya ambapo sasa
askari wanaoajiriwa na shirika kutoka katika Vyuo vya Wanyamapori vya Mweka na
Pasiansi pamoja na wale wa kutoka Jeshi la Kujenga Taifa watalazimika kupitia
mafunzo maalum yanayoandaliwa na shirika kwa ajili ya kuwawezesha waajiriwa
wapya kufahamu mazingira halisi ya utendaji kazi katika eneo la uhifadhi katika
maeneo ya Hifadhi za Taifa.