Meneja wa Kiwanda cha Bundaa, Roharl
Parmar (kushoto) akiwa na Kaimu Afisa Shughuli wa kiwanda hicho, Paul Aaron
wakati alipohojiwa na gazeti hili ofisi kwake. Na Mpigapicha Wetu.
Posted Jumatatu,Januari27 2014 saa 10:3 AM
Kwa ufupi
- Uchunguzi
uliofanywa gazeti hili ulibaini kuwa baadhi ya viwanda vya kuzalisha
mafuta vimekuwa vikinunua mbegu hizo kwa bei nafuu kwa madai ya kuzitumia
kutengenezea mashudu (chakula cha mifugo) na kuchomea
Bunda. Baadhi ya viwanda Mikoa ya
Mara na Mwanza vinadaiwa kutumia mbegu za pamba zilizooza kwa ajili ya
kuzalisha mafuta ya kula, hali ambayo inahatarisha afya za watumiaji wa mafuta
hayo.
Uchunguzi uliofanywa gazeti hili
ulibaini kuwa baadhi ya viwanda vya kuzalisha mafuta vimekuwa vikinunua mbegu
hizo kwa bei nafuu kwa madai ya kuzitumia kutengenezea mashudu (chakula cha
mifugo) na kuchomea
`boiler’ (chombo cha kuchemshia
malighafi ya mafuta), lakini zimekuwa zikitumika kinyume.
Badala yake zimekuwa zikitumika
kukamua mafuta ambayo kutokana na kuwa machafu, huchanganywa na mafuta mengine
masafi kisha kuingizwa sokoni.
Uchunguzi ulibaini kuwa mchezo huo
umekuwa ukifanyika kwa muda mrefu, kabla ya kugunduliwa na wataalamu wa Mamlaka
ya Chakula na Dawa nchini (TFDA), Kanda ya Ziwa, kutokana na kuwapo kwa
malalamiko mengi kutoka kwa walaji.
Imebainika kuwa TFDA walifanya
ukaguzi wa kushtukiza katika Viwanda vya Bundaa Oil Mill kilichoko wilayani
Bunda mkoani Mara na Brichand Oil Mill Ltd kilichopo jijini Mwanza kutokana na
kudaiwa kujihusisha na mchezo huo.
Meneja wa TFDA, Kanda ya Ziwa, Moses
Mbambe alisema: “Malalamiko ya walaji yalitusukuma kufanya msako wa kustukiza
kwenye Kiwanda cha Brichand Oil Mill Ltd…Wakakiri kuuza mbegu zilizooza kwa
Kampuni ya Bundaa Oil Mill Ltd na katika kufuatilia ndipo tulibaini ukiukwaji
huo wa sheria huo,” alisema Mbambe.
Mbambe alisema uongozi wa Brichand
Oil Mill Ltd ulisema kuwa mbegu hizo waliwapa Bundaa Oil Mill Ltd kwa madhumuni
ya kutengeneza mashudu na siyo vinginevyo, lakini TFDA katika ukaguzi wao
walibaini mbegu hizo zilitumika kwa ajili ya kuzalisha mafuta.
Mkaguzi wa Vyakula katika Mamlaka ya
Mji mdogo wa Bunda, Mafuru Madaraka alikiri kiwanda hicho kuhusika kutumia
mbegu zilizooza kutengeneza mafuta ya pamba.
“Ni kweli tulivamia tukiwa na
wataalamu wa TFDA na kukuta wakizalisha mafuta kwa kutumia mbegu
zilizooza…mafuta mengine yakiwa yameshaingia sokoni na mengine yakiwa
yamehifadhiwa stooni,” alisema Madaraka.
Alisema mbegu hizo zilichukuliwa na
kuamriwa kuteketezwa chini ya usimamizi wao na TFDA, huku uongozi wa kiwanda
hicho ukidai kuwa mbegu hizo waliuziwa na Kiwanda cha Brichand Oil Mill Ltd.
“Inaonekana ni mtandao licha ya kudai
waliwauzia mbegu zilizooza lakini kulikuwa na ndoo za Kampuni ya Brichand Oil
Mill Ltd…Ina maana mafuta yaliyokuwa yanazalishwa ilikuwa kampuni hiyo
iyachukue…Hatujui wanayaingizaje sokoni yakiwa hivyo,” alisema Madaraka.
Viongozi
wa viwanda
Meneja
wa Bundaa Oil Mill Ltd, Rohan Parmar alikiri kukamatwa wakisaga mbegu chafu na
kudai kwamba walipewa mbegu hizo na Kampuni Brichand Oil Mill Ltd.
Alipotakiwa
kufafanua sababu za kukubali kupokea mbegu chafu wakati wakijua sheria
hairuhusu alisema: “Kwanza muda huo nilikuwa Igunga sijui mambo mengi…Sisi
tumepata shida sana tumekosa mbegu sasa tumesimamisha uzalishaji ….Hayo mengine
sipendi kuyasemea.”
Baada
ya gazeti hili kumbana kwamba alikuwapo kama msimamizi wakati TFDA
walipowakamata, aling’aka akisema: “Sasa wewe unataka mambo mengi ya
nini…Walikamata mbegu wakachoma ...Sisi sasa tumefunga kiwanda…Unataka nini
tena…Mimi siwezi kusema mpaka mwanasheria wa kampuni awepo.”
Alipotakiwa
kumtaja mwanasheria ili afuatwe kutoa ufafanuzi, Maramar alikataa akisema:
“Siwezi kusema majina, wala alipo, wala namba…Wewe ‘tafuta’ sisi baada ya wiki
moja.”
Jitihada
za gazeti hili ziliwezesha kupatikana kwa Mwanasheria wa Kampuni, Denis Masami
ambaye alipoulizwa kuhusu uzalishaji wa mafuta kwa kutumia mbegu zilizooza
aliomba apewe nafasi ya kufuatilia kwa kuwa wakati wanakamatwa na TFDA alikuwa
bado hajaajiriwa.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi wa Brichand Oil Mill Ltd, Mohammed Sharif alikiri kiwanda
chake kuwauzia Bundaa Oil Mill Ltd, mbegu chafu lakini kwa kwa ajili ya
kusafisha `Boiler’.
“Walichukua
kwa makubaliano kuwa wanakwenda kusafisha mashudu ili yawe meupe badala ya
mafuta…Maana wana mtambo usio wa kawaida una uwezo wa kuchanganya mbegu
zilizooza na safi ukasaga bila matatizo…Mitambo mingine haiwezi kufanya hivyo,”
alisema.
Wasemavyo
wananchi
Uchunguzi
umebaini kuwa baadhi ya wananchi walilalamikia mafuta yanayotokana na mbegu
hizo, lakini kwa upande mwingine yalikuwa yakipendwa na wakaanga samaki
kutokana na kuuzwa kwa bei rahisi ikilinganishwa na mafuta ya aina nyingine.
Mkazi
wa Kijiji cha Migungani, Bunda ambao Kichere Gikaro (60 alisema kulikuwa na
malalamiko mengi kutoka kwa watumiaji wa mafuta yalitoka katika Kiwanda cha
Bundaa Oil Mill Ltd.
“Hapa
kwetu sisi ndio tulitakiwa kuwa wateja wakubwa kwa kuwa kiwanda kiko
hapa……lakini kutokana na malalamiko ya watumiaji wengi kuhusu ubora wake,
tulilazimika kwenda kununua mafuta mengine mjini, malalamiko
aya
yaliwafikia watu wa afya, lakini hatukupata majibu,” alisema Gikaro.
Muuzaji
wa mafuta katika Soko Kuu la Bunda Mjini aliyejitambulisha kwa jina la Nashon
alikiri kwamba alikuwa na wakati mgumu kuuza mafuta hayo kutokana na
kulalamikiwa kwamba yalikuwa na uchafu pia harufu mbaya.
“Ilikuwa
shida kweli maana licha ya kwamba bei yake iko chini lakini soko lake ni gumu
sana, kama unavyojua sisi wafanyabiashara tunataka unaponunua mali basi itoke
ili pesa yako izunguke,” alisema Nashon.
Naye
Sundi Juma ambaye ni muuza samaki stendi Kuu ya Bunda, alisema yeye anayapenda
mafuta hayo kutokana na ukweli kwamba ni mazito hivyo hayaishi haraka anapokuwa
akikaanga samaki wake.
“Kwanza
mafuta haya ni bei ni nafuu…Ni mazito, ukinunua kidogo unakaanga samaki
wengi…unatumia gharama ndogo, ingawa wateja wanalalamika harufu hasa samaki
wakila lakini kwetu ni nafuu…Maana mafuta mengine bei iko juu na ni
mepesi,”alisema Juma.
Alisema
bei ya mafuta hayo yanayozalishwa na Bundaa Oil Mill Ltd ni Sh 1,400 kwa lita
moja, ikilinganishwa na mafuta aya aina nyingine ambayo yanauzwa Sh2,000 kwa
kiasi hicho.
“Ukinunua
mafuta ya bei kubwa unalazimika kuuza samaki pia kwa bei kubwa, wakaanga samaki
hatuko tayari kununua mafuta ya bei ya juu…Kwa kuwa ukinunua wewe mwenzio
anachukua ya bei ya chini, anauza samaki bei nzuri, wako wanabaki,” alisema.
Juma
alikiri kuwapo kwa watu wanaolalamika kujisikia vibaya hasa wanapokuwa
wanakaanga samaki kutokana na mvuke unaotokana na mafuta hayo kubadili hali ya
hewa na kuwa nzito.
Madhara
kiafya
Mmoja
wa maofisa wa TFDA, Kanda ya Ziwa ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe kutokana
na kutokuwa msemaji wa taasisi hiyo, alisema miongoni mwa madhara yanayoweza
kumpata mtumiaji ni saratani.
“Uzalishaji
wa mafuta hayo hutumia kemikali aina ya caustic soda ambayo kisheria lazima
isimamiwe na mtaalamu, lakini hata mkemia hawakuwa naye…Wanazalisha mafuta kwa
mbegu zilizooza…Wanawalisha watu vitu visivyo stahiki…madhara yake ni makubwa
kiafya,”alisema.
Mfamasia
na mmiliki wa zahanati binafsi wilayani Serengeti Mkoa wa Mara, Thomas Burito
alisema madhara kwa watumiaji wa mafuta hayo ni makubwa kwa kuwa husababisha
mishipa kuziba na matokeo yake ni watumiaji kuugua saratani na figo.
“Matumizi ya mafuta kama hayo
ni hatari kwa maisha ya walaji, kiafya wanaathirika polepole na wengi hupata
kansa, ugonjwa ya moyo, figo na hayo ni magonjwa hatari na mwisho kama
hakuchukua hatua haraka ni vifo,” alisema Burito.
Ofisa Afya wa Wilaya Bunda, Fadhili
Kinyogoli alisema matatizo ya kuzalisha mali zisizo na kiwango na kuziingiza
sokoni ni kubwa kutokana na wananchi ambao ni walaji kutokutoa taarifa kwa
wakati ili hatua ziweze kuchukuliwa.