Na Editor
20th August 2015
Katuni.
Katika toleo letu la jana ukurasa wa
pili, kulikuwa na habari yenye kichwa cha habari `Waandishi wa habari wapigwa
mawe.’
Tukio hili la wanahabari kupopolewa
kwa mawe, liliripotiwa kutokea katika kijiji cha Ruanda kata ya Ruanda
Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Agosti 17, mwaka huu ambako walikwenda
kutekeleza majukumu yao ya kazi.
Imeelezwa kwamba baada ya kufika
katika kijiji hicho, kundi la watu waliokadiriwa kufikia 40, walianza
kuwashambulia wanahabari hao kwa mawe.
Katika tukio hilo, Mwenyekiti wa
kijiji hicho cha Ruanda, Deogratias Haule, aliyekuwa amefuatana na wanahabari
hao, pia alishambuliwa kwa mawe na kumsababishia majeraha puani na mdomoni na
kupelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mbinga kwa matibabu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma,
Mihayo Msikhela, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo lililotokea majira ya
mchana.
Kamanda Msikhela aliwataja waandishi
wa habari waliokumbwa na mkasa huo kuwa ni Kassian Nyandindi, wa magazeti ya
kampuni ya Business Times, Aden Mbelle na Pastory Mfaume, kutoka Redio
Jogoo FM ya mjini Songea mkoani Ruvuma.
Alisema wanahabari hao walipatwa na
mkasa huo baada ya kwenda kutekeleza majukumu yao ya kikazi ya kuandika tukio
la kufungwa kufuli ofisi za kata ya Ruanda, kitendo kilichofanywa na baadhi ya
wanakijiji hicho wasiofahamika.
Kamanda Msikhela alisema baada
ya wanahabari hao kukamilisha shughuli yao iliyowapeleka, ghafla liliibuka
kundi la watu hao na kuanza kuwashambulia kwa mawe wakati wakijiandaa kurejea
mjini Songea ambapo mmoja wa waandishi hao, alirushiwa jiwe usoni.
Tukio hili siyo tu limetusikitisha
sisi wanataaluma ya habari, bali pia limetushtua na kujiuliza maswali mengi
yasiyo na majibu.
Tunasema ni tukio la kinyama na
lililokosa hata chembe ya ustaarabu.
Hatujui waliofanya unyama huu kama
wana malengo gani, lakini kwa vyovyote vile, kitendo hiki kinapaswa kulaaniwa
vikali na kila mpenda amani.
Tunaliomba Jeshi la Polisi mkoani
Ruvuma lifanye uchunguzi wa kina kuwabaini wote walioshiriki kufanya uhalifu
huu na sheria ichukue mkondo wake.
Aidha, tunalipongeza pia Jeshi la
Polisi mkoani Ruvuma kwa kumshikilia mtuhumiwa mmoja kuhusiana na tukio hili
katika hatua hizi za awali tukiamini kwamba juhudi zaidi zitafanyika
kuhakikisha kwamba wote walioshiriki kwa namna moja ama nyingine, wanapatikana
na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.
Tunaamini kwamba jamii inafahamu
fika mchango wa wanahabari katika kulisukuma mbele gurudumu la maendeleo la
Taifa letu isipokuwa watu wachache kama hao waliowapiga wanahabari, wana lao
jambo.
Tunasema tunaalani kwa nguvu zote
kitendo hiki ambacho kwa hakika tunajiridhisha kuwa kimefanywa na wachache
wenye upeo mdogo wa kuelewa majukumu ya wanahabari mbele ya jamii.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment