- Amina Juma
- Habari zilizothibitishwa na baadhi ya waombolezaji waliokuwa nyumbani kwa marehemu Visiga, Kibaha zinasema baadhi ya wanandugu walimkana Amina siku chache baada ya kutangazwa vifo hivyo.
Amina ambaye inadaiwa kuwa alikuwa akiishi na
Fortunatus Msofe aliyekuwa askari katika Kambi ya Msangani, 36KJ Pwani
alisema jana: “Kumekuwa na mzozo wa hali ya juu na ndiyo maana
tumeshindwa hata kufika Uwanja wa Ndege kuupokea mwili na hata kesho
(leo) sidhani kama nitakwenda... kuna mtafaruku mkubwa wa kifamilia.”
Baada ya kutimuliwa, Amina ambaye hawakuwahi
kupata mtoto na marehemu Msofe, alilazimika kuondoka kwenye nyumba hiyo
na kwenda Mlandizi kwa wazazi wake.
“Nimeishi na Msofe kwa miaka mitatu, akiwa kambini
mimi niko hapa na wakati mwingine alikuwa analala huku... lakini leo
wamenitimua,” alisema huku akilia.
Habari zilizothibitishwa na baadhi ya waombolezaji
waliokuwa nyumbani kwa marehemu Visiga, Kibaha zinasema baadhi ya
wanandugu walimkana Amina siku chache baada ya kutangazwa vifo hivyo.
Ilidaiwa kwamba Amina alitimuliwa katika nyumba
hiyo Ijumaa iliyopita, saa saba mchana baada ya ndugu watatu wa marehemu
kufika hapo wakitokea Tanga.
Walipofika inadaiwa kuwa walitangaza kusitishwa msiba huo katika nyumba hiyo na kutangaza kutomtambua mke huyo.
Watu hao waliwaeleza waombolezaji kuwa walitumwa
na baba mzazi wa marehemu, Willbad Msofe kutoka Kange, Tanga kufika
Kibaha kusitisha msiba uliokuwa ukiendelea nyumbani kwa mtoto wake huyo.
Inadaiwa pia kuwa katika msafara huo, alikuwapo mdogo wa marehemu ambaye aliwahi kuishi kwa miaka miwili na Amina hapo Visiga.
Ilidaiwa kuwa walipofika nyumbani hapo walionana
na mfiwa, Amina na wazazi wake ambao pamoja na majirani na watu wengine
wengi, walikuwa wakimfariji binti yao huyo.
Mmoja wa waombolezaji alisema baada ya salamu
wanandugu hao walianza kuulizia mali za marehemu na walikuwa wakimuuliza
Amina ambaye aliwaleza kila kitu kilipo na baada ya hapo ndipo
walipomweleza kuwa wametumwa na baba wa marehemu kuwa watu hawatakiwi
kuomboleza kwenye eneo hilo kwani msiba upo Tanga tu ambako ndiko iliko
familia yake.
Alipoulizwa baba wa marehemu, Mzee Msofe alisema:
“Mimi ndiye niliyeagiza nyumba ifungwe na ukweli ninamfahamu Amina,
lakini simtambui kama mkewe kwa kuwa hawajafunga ndoa... Hata wewe si
unayafahamu haya? Uchumba si ndoa na ukifunga ndoa ndipo unatambulika
rasmi,” alisema.
Akiwa kwa wazazi wake Mlandizi jana, Amina alisema:
“Namwachia Mungu maana hayo yote nashangaa
yanatokea wakati huu mume wangu ‘Fortu’ amekufa, mbona kipindi chote cha
miaka mitatu iliyopita familia ya Tanga dada zake na mdogo wake
tuliishi nao vizuri kwangu nilipokuwa na marehemu? Nimeishi na ndugu
wote lakini hawakuwahi kuhoji, hata nilipokwenda na mume wangu Kange
baba na mama Msofe nilikaa nao zaidi ya wiki na hawakunikana, ila
nashangaa,” alisema na kulia kwa uchungu.
Akizungumzia kitendo hicho, baba yake Amina, Juma
Juma alisema: “Nimeshangaa hizi taarifa. Tulikuwa tunajiandaa kupokea
msiba wa mwanetu, lakini leo yanakuja mengine kwa kweli imetushangaza
sana.”
“Nasubiri baada ya kumzika marehemu, nitazungumza
nao... Kinachonishangaza ni kwamba walituandikia barua ya kumposa binti
yangu na tukawajibu na gharama zilikuwa Sh1.2 milioni... Tutazungumza,
ngoja hili lipite kwanza,” alisema mzee Juma.
Maisha ya Amina na ‘Fortu’
Akisimulia maisha yao, Amina alisema: “Tulianza
kuishi Mbezi Luis mwaka 2010 katika nyumba ya kupanga na nikamshawishi
tununue kiwanja na kwa kuwa mimi ni mwenyeji wa Kibaha, niliwatumia
marafiki wa familia yangu Mlandizi wakatafutia eneo na mwaka 2011
tulipata na tukaanza ujenzi.
“Tukiwa Mbezi, tulianza kufyatua matofali kisha
ujenzi ukaanza Visiga mwaka 2012 mwanzoni na Septemba mwaka huo
tulihamia kwenye nyumba yetu na hapo ndiyo ilikuwa makazi yetu hadi
marehemu anaondoka kwenda Darfur.
“Wakati wote huo ‘Fortu’ alikuwa keshaniposa na
hata barua zote za posa zipo na tulikuwa tukisubiri utaratibu wa kijeshi
marehemu kukamilisha miaka sita ya kukaa kambini kisheria ndipo
aruhusiwe kuoa.
“Fortu alikamilisha miaka hiyo mwaka 2012 mwishoni
na wakati akijiandaa kwa kufunga ndoa ndipo ikatokea safari ya Darfur
mwanzoni mwa mwaka huu na tukakubaliana tusitishe kwanza akirudi
tukamilishe, lakini haikuwa.... Halafu wananifukuza wanasema hawanijui,”
alieleza huku akiangua kilio