JESHI
la Magereza nchini limewafukuza kazi askari watatu na kumsimamisha kazi afisa
wake mmoja kwa tuhuma za kukutwa na nyara za serikali kinyume cha sheria.
Mbali
na hatua hiyo pia Mkuu wa gereza la Kiteto, Mrakibu wa Magereza Ally Sauko,
amevuliwa madaraka na kurejeshwa katika Ofisi ya Mkuu wa Magereza Mkoa wa
Manyara akisubiri hatua ya mamalaka ya kinidhamu dhidi yake kwa kutumia
madaraka vibaya.
Askari
waliofukuzwa kazi ni Sajenti Ketto Ramadhan, Koplo Silvester Dionice na Wada
Barik huku afisa aliyesimamishwa kazi ni Joseph Kimaro ambaye ni mrakibu
Msaidizi wa Magereza akifunguliwa mashtaka ya kinidhamu.
Taarifa
ya jeshi hilo kwa vyombo vya habari ilieleza kuwa uchunguzi wa awali ulibaini
ukiukwaji wa taratibu na maadili ya jeshi la Magereza na kwamba askari hao
watapelekwa mahakamani baada ya upelelezi wa Polisi kukamilika .
Askari
hao kwa kushirikiana na baadhi ya wananchi wanadaiwa kukamatwa na askari wa Kikosi
cha Kuzuia Ujangili Kanda ya Kati Julai 23 mwaka huu wakiwa na nyara za
serikali zenye thamani ya sh milioni 55.
Inadaiwa
askari hao wakiwa na gari la magereza Toyota Land Cruiser lenye namba za
usajili STK 4394 walikamatwa wakiwa wamepakia Twiga wawili, Majike mawili ya
Swala Palapala na mbuni wawili.
Watuhumiwa
walipopekuliwa katika gari walikutwa na kibali kilichoombwa na Hassan Omari
kikiwaruhusu kuwinda nyati mmoja na pundamilia wawili.
Katika
tukio hilo watuhumiwa wengine waliokamatwa ni Abubakari Ngaula, Hamza Ndachi,
Saidi Idd na Husein Gola ambao pia walikutwa na bunduki ya aina ya SR mali ya
Jeshi la Magereza pamoja na Rifle moja.
|