Subscribe:

Ads 468x60px

MFADHILI WA MTANDAO WA MTANDAO WA UWINDAJI WA TEMBO APANDISHWA KIZIMBANI

Mlangirwa Emmanuel Paulo(32)maarufu kama (Mnyarwanda}akiwa chini ya ulinzi katika mahakama ya wilaya ya Serengeti akiteta jambo na ndugu yake

 Mlangirwa Emmanuel Paulo(32)maarufu kama (Mnyarwanda)akitafakari jambo wakati akiwa mahakama ya wilaya ya serengeti ambapo ameunganishwa na waliokuwa askari polisi kutoka Biharamulo na Bukoba walionaswa na vipande 18 vya meno ya tembo Mugumu na kumtaja kama mfadhili wao.


MFADHILI WA MTANDAO WA UWINDAJI WA TEMBO  APANDISHWA KIZIMBANI.
Machi 12,2013.
SERENGETI. 

MTUHUMIWA anayedaiwa kufadhili mtandao wa uwindaji na ununuzi wa pembe za ndovu maeneo mbalimbali ya nchi  mwenye asili ya Rwanda amepandishwa katika mahakama ya wilaya ya Serengeti akiunganishwa katika kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili waliokuwa askari polisi kutoka mkoa wa Kagera.

Mtuhumiwa huyo aliyeunganishwa kesi ya uhujumu uchumi namba 1/2013 ni Mlangirwa Emmanuel Paulo(32)maarufu kama (Mnyarwanda)ambaye alitajwa na watuhumiwa wengine kwenye kesi hiyo baada ya kukamatwa na vipande 18 vya meno ya tembo kuwa  ni mfadhili wa mtandao  wa ujangili na mnunuzi wa meno ya tembo.

Mbele ya Hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama hiyo Amoni Kahimba mwendesha mashitaka wa polisi Pascal Nkenyenge aliomba kubadilidha hati ya mashitaka kwa kumwongeza mshitakiwa  wanne baada ya kukamatwa.

Katika hati hiyo awali iliwataja washitakiwa watatu ambao wamefikishwa mahakamani hapo mara tatu kuwa ni  Boniphace John Kurwa (31)mkazi wa Geita ,Gerard Tuji Kabalega(33) David Duma Delama(36)ambao walikuwa askari polisi Bukoba na  Biharamulo.

 Mwendesha mashitaka aliiambia mahakama kuwa wanakabiliwa na mashitaka ya kula njama na kufanya biasshara haramu ya nyara za serikali kinyume na kifungu namba 84(1)cha sheria ya wanyama pori namba 5 ya mwaka 2009 ,pamoja na kifungu 14(b)na 57(1)na 60(20ya kuhujumu uchumi iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

 Akisoma maelezo ya shitaka alisema januari 5 mwaka huu,muda na wakati usiojulikana mjini Mugumu washitakiwa watatu walikutwa na meno ya tembo vipande 18 vyenye uzito wa kilo 104 vyenye  thamani ya sh.67,750,000 mali ya serikali.

Washitakiwa walikana shitaka moja la kula njama ya kufanya biashara haramu ya nyara,na mashitaka mengine hawakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kuyasikiliza mpaka kibali cha Mkurugenzi wa mashitaka ambacho hakijatolewa.

.Kutokana na udhaifu wa hati ya mashitaka ilivyoandaliwa  Hakimu Kahimba amelazimika kuonya  upande wa mashitaka kuwa makini na kuagiza kufanya marekebisho katika hati ya mashitaka hayo.

Aliwataka  kufuata taratibu za kisheria kwani mashitaka yaliyoandaliwa dhidi ya washitakiwa ni dhaifu na hayatoshelezi kwani yanalenga kuifanya mahakama iweze kuwaachia washitakiwa.

“Mahakama iko hapa kutoa haki kwa pande zote ,nimekuwa wazi kueleza jambo hili mbele ya mahakama,ningeweza kukaa kimya nikaendelea kusikiliza kesi, si jambo la busara nikakaa bila kueleza mapungufu hayo,sipendi mahakama siku ya kutoa hukumu ilaumiwe kwa mambo kama haya”alisema hakimu Kahimba.

Alimwagiza mwendesha mashitaka atoe taarifa kwa mpelelezi wa kesi,mpelelezi wa mkoa(RCO),wilaya(OC CID)na wote wanaohusika kufanya marekebisho ya mashitaka .

Alibainisha kuwa mashitaka yajieleze wazi kila mtuhumiwa alikamatwa anafanya nini,wapi na muda upi kwa kila kosa badala ya maelezo ya jumla kuwa wote walikamatwa wanafanya makosa hayo.

Washitakiwa waliomba kulegezewa masharti ya dhamana ambapo walikubaliwa na hakimu kwa kuruhusu kati ya wadhamini wawili mmoja atoke Serengeti mwingine nje ya wilaya ,hata hivyo walishindwa kutimiza  masharti na kesi imeahirishwa hadi march 25 mwaka huu na washitakiwa wamerudishwa mahabusu.

Masharti mengine yaliyobaki kama yalivyo ni kuwasilisha fedha taslimu sh.31 milioni au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya kiasi hicho iliyofanyiwa uthamini na mthamini wa serikali.

Washitakiwa wawili wakazi wa mjini Mugumu bado wanaendelea kusakwa baada ya kutoroka siku ya tukio.
Mwisho.

0 comments:

Post a Comment