KUFUTWA KWA MATOKEO YA WATOTO 111
SEKONDARI MANCHIRA WAZAZI WAUNDA KAMATI KUFUATILIA .
Machi 13,2013
SERENGETI.
WAZAZI wa watoto waliokuwa wanafunzi wa Manchira
Sekondari wilayani Serengeti waliofutiwa matokeo kwa madai kuwa majibu yalikuwa
ya mfanano wameibuka na kulitaka baraza la mitihani kupitia upya uamzi wake.
Wanafunzi 111 kati ya 114 waliohitimu kidato cha nne mwaka
jana katika shule hiyo wamefutiwa matokeo na baraza la mitihani,taarifa ambayo
inakinzana na ya awali kuwa majibu yao hayakutolewa kwa sababu hawakuwa
wamelipa fedha ya mitihani.
Kutokana na utata huo wazazi
wamelazimika kuunda kamati kwa ajili ya kufuatilia ili kujua ukweli wa taarifa
ipi ni sahihi kwa kuwa awali wazazi waliambiwa hawakulipa fedha ya mitihani
ingawa baadhi walikiri kulipa na mkuu wa shule hakuweza kutoa risti na anasakwa
na polisi.
Katika barua hiyo iliyosainiwa na
wajumbe 7 chini ya Mwenyekiti wao Daniel Washa inashangazwa na baraza la
mitihani ambalo lilituma barua kwa mkuu wa shule ikibainisha kuwa matokeo
yamezuiliwa kwa kuwa watoto hawakulipia mitihani.
“Taarifa ilitolewa januari
25,2013 kuwa baraza limetoa barua ya maelezo hayo,februari 21 katika kikao cha
wazazi walikubali kulipa sh,35,000 kwa kila mzazi …februari 22 tukawa tumekusanya sh,3,080,000
zikatumwa baraza la mitihani kupitia akaunti Na.2011100238 NMB na baada ya
kupokea pesa machi 1 mkuu wa shule alidai alipokea barua
ambayo inaonekana ilikuwa imeandaliwa mapema kuwa wamefutiwa
majibu”imesema barua.
Wazazi hao wanahoji taarifa ya
baraza la mitihani kuwa oktoba 9,2012 watahiniwa wakifanya mtihani wa Kiswahili
msimamizi alikuta Toilet Paper yenye “Notes”za somo la Kiswahili kwenye dawati
la mtahiniwa S3684/0003 na S3684/0072/0098/0105 na 0111 walikutwa na karatasi
zenye notes za somo la Biology ndani ya chumba cha mtihani,lakini
hawakuchukuliwa hatua kama wakosaji.
“Kwa kuwa watahiniwa waliofutiwa
walikuwa vyumba vitatu tofauti ,je toilet paper zingeweza kuathiri vyumba
vyote?,kama vyanzo vya baraza vimetaja majibu kufanana kwa masomo ya Physics,Biology
na Chemistry ,iweje Kiswahili somo walilokutwa na Notes
halikuhusishwa”wamehoji.
Kamati hiyo inayoundwa na Daniel
Washa Mwenyekiti,Paulo Mtatiro Chacha(katibu)na wajumbe Simioni Nyatutu,Edina
Mahemba,Damiani Thobias,Japhet Maduhu na Samwel Omar wamebainisha kuwa shule
zilizofutiwa matokeo hutajwa kupitia vyombo vya habari lakini baraza liliomba
watume fedha watoe matokeo na baada ya kufanya hivyo wakadai matokeo yamefutwa.
Na kuwa Baraza la Mitihani
halikuhusisha ngazi ya wilaya husika kuhusiana na matokeo hayo ili kubaini
udanganyifu huo badala yake limeibuka na majibu ambayo yameacha mashaka kwa
kuwa walitaka malipo,wazazi wanahoji uhalali wa kupokea fedha za matokeo ambayo
yaliyokuwa yamefutwa.
Wanaiomba serikali kupitia baraza
la Mitihani kupitia upya uamzi wake wa kuwafutia matokeo watoto 111 wa
sekondari ya Manchira ,pia Tume iliyoundwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda ifanye
uchunguzi ili kubaini ukweli kwa kutumia barua za baraza za kudai malipo ili
watoe matokeo wakati wakijua hakuna matokeo yatakayotolewa.
Ofisa elimu Sekondari wilaya ya
Serengeti William Makunja amekiri kupokea nakala ya barua hiyo iliyotumwa na
wazazi kwenda Baraza la Mitihani na kudai kama wilaya nao wanafuatilia.
Juhudi za kumpata msemaji wa
baraza la Mitihani zinaendelea ili kutoa ufafanuzi wa malalamiko hayo.
Mwisho. inaendelea
0 comments:
Post a Comment