Subscribe:

Ads 468x60px

mwanafunzi atuhumiwa kwa kuua kwa mshare familia yake yakimbia kwa kuhofu kuuawa


MWANAFUNZI WA SEKONDARI ATUHUMIWA KUUA KWA MSHARE,
Na Anthony Mayunga-Serengeti.
Oktoba 27,2012.


MWANAFUNZI wa kidato cha tatu katika sekondari ya Busawe kata ya Majimoto wilayani Serengeti mkoani Mara Peter Lucas Wambura(17)anasakwa na polisi kwa tuhuma za kumpiga mshare kifuani Chacha Damiani Mangali(18) na kufa papo hapo.

Tukio hilo linalodaiwa kutokea oktoba 26,majira ya saa 2 mwaka huu  usiku nyumbani kwa marehemu Mangali limethibitishwa na uongozi wa kitongoji na polisi linahusishwa na wivu wa kimapenzi.

Mwenyekiti wa kitongoji hicho Daud Mgendi aliliambia Mwananchi Jumapili kuwa mtuhumiwa huyo ambaye ni jilani yake na marehemu alimpiga mshare kifuani na kufa papo hapo wakati anafungua mlango atoke nje ya nyumba yake.

“Sababu hazijajulikana kuwa ni vijana waliokuwa wanalingana huenda wamegongana kwa wanawake ,maana inaonekana marehemu alifungua mlango akidhani ni mambo ya kawaida ndipo akapigwa mshare kifuani na kupiga kelele kisha akakata roho”alisema Mwenyekiti.

Alisema mara baada ya kutenda unyama huo mtuhumiwa aligeuka kama kichaa na kitishia usalama wa wananchi kwa kuwa alikuwa na upinde na mishare mingi ,na kutokana na giza walishindwa kumdhibiti na kutokomea kusiko julikana.

“Kumdhibiti ilikuwa vigumu kwa kuwa alionekana kuwa kama kichaa na kutishia watu kwa kurusha mishare ovyo na kutokana na giza kila mtu aliamua kuchukua tahadhari kwa kuwa hakuwa katika hali ya kawaida”alisema.

Baba mzazi wa marehemu Damiani Mangali akiongea na gazeti hili kwa njia ya simu alisema kuwa kijana wake alikuwa hajaoa na wanahisi huenda wamegongana kwa wanawake kwa kuwa hakuna madai mengine ambayo ameyasikia.

“Kama ingekuwa deni tungesikia lakini kwa matatizo ya wanawake mara nyingi huwa siri zao maana wote walikuwa vijana na majilani,nilipigiwa simu na kaka yake na marehemu kuhusiana na tukio hilo,tunaendelea kufuatilia chanzo lakini inauma kifo cha ghafla namna hii bila hata kuwaeleza sababu”alisema.

Polisi wilayani hapa waanaendelea na uchunguzi ikiwa ni pamoja na kumsaka mtuhumiwa ,ambapo wameomba wananchi watoe ushirikiano wa chanzo na alikojificha kwa kuwa anaweza kusababisha madhara makubwa zaidi.

Hivi karibuni mwanafunzi mmoja wa  kidato cha pili Mugumu  sekondari  wilayani wilayani hapa  Mwang’omba Kegocha(16)amefikishwa katika mahakama ya wilaya  kwa tuhuma ya kumchoma kisu Chacha Pasta(29)

Tukio ambalo linadaiwa lilitokea wakati wanacheza kamali ambapo mtuhumiwa inadaiwa alikuwa ana mdai marehemu  ths 5,000  na katika kudaiana wakakorishana ndipo akamchoma kisu ubavuni na kufa papo hapo.
Mwisho.


FAMILIA YA MWANAFUNZI ANAYETUHUMIWA KUUA KWA MSHARE YATOWEKA KIJIJINI
KWA HOFU YA KUUAWA.
NaAnthony Mayunga-Serengeti
Oktoba 28,2012.
FAMILIA ya mwanafunzi wa kidato cha tatu sekondari ya Busawe wilayani
Serengeti Peter Lucas Wambura(17)anayesakwa  na polisi kwa tuhuma za
kumpiga mshare kifuani Chacha Damiani Mangali(18)imetoweka kijijini
hapo na malizao zikiwemo kuku kwa hofu ya kuuawa.

Kutoweka kwao kunadaiwa kutokea oktoba 27,usiku mwaka huu baada ya
kubaini kuwa Mangali ameaga dunia kufuatia  kupigwa mshare wa sumu
kifuani na mtuhumiwa akimtuhumu kuwa na uhusiano wa mapenzi na mdogo
wake anayesoma kidato cha pili sekondari ya Busawe.

Kwa mjibu wa habari kutoka kijijini hapo zilizothibitishwa na kamanda
wa tarafa hiyo Inspekta Abdallah Idd ambaye alikuwa eneo la tukio
zinadai kuwa familia hiyo ilitokomea kusikojulikana wakiwa wamebeba
kila kitu ikiwemo kuku.

Hofu yao ikiwa wananchi wangeweza kuwadhulu kwa kitendo kilichofanywa
na kijana wao ,tukio ambalo linadaiwa kushuhudiwa na mama wa mtuhumiwa
akimpongeza kijana wake kwa kumchoma mshare Mangali kwa kuwa alikuwa
alikuwa anachangia kuharibu mwenendo wa mtoto wake kimasomo.

Inadaiwa kuwa siku ya tukio marehemu Mangali alikwenda kwao na
mtuhumiwa kwa lengo la kukutana na mpenzi wake huyo,tukio lililomuudhi
mtuhumiwa na kuchukulia kama dharau kwa familia kwa kuwa walikuwa
wameishamkata uhusiano wa mapenzi na binti huyo kwa kuwa ni
mwanafunzi.

“Walipigana kwanza hapo nje kwa kuwa wote walikuwa kama wanalingana
,mtuhumiwa baada ya kuona amezidiwa nguvu aliingia ndani na kutoka na
upinde na mshare mwenzake akidhani ana tania ndipo akamchoma kifuani
,lakini akafanikiwa kuuchomoa na kutoa taarifa kwao kwa kuwa ni
majilani”alisema mmoja wa wanafamilia jina limehifadhiwa.

Hata hivyo familia ya marehemu ilimwita mama wa mtuhumiwa ambaye
alisema alichokuwa anatafuta amekipata,wakati wanajiandaa kwenda
hospitali aliaga dunia kwa kile kinachodaiwa alizidiwa na sumu yam
share huo.

Hata hivyo jamii imesema itamnasa mtuhumiwa na familia hiyo kwa kuwa
hawataweza kukwepa zaidi ya kuchelewa kukamatwa,kwa kuwa tukio hilo ni
la kusikitisha na ambalo liliibua hisia kali za watu.

Habari za uhakika zinadai kuwa kutoroka kwa familia hiyo kulitokana na
hisia za kuweza kuuawa kwa kuwa si watu wa jamii hiyo na ukoo wa
aliyeuawa ni mkubwa ,huenda wakawa wamekimbilia maeneo mengine huku
mtuhumiwa akawa hakuambatana nao.

Mwenyekiti wa kitongoji hicho Daud Mgendi aliliambia Mwananchi kuwa
tukio hilo lilitokea oktoba 26,majira ya saa 2 usiku mwaka huu
nyumbani kwa marehemu likihusishwa na migogoro ya mapenzi.
 

MUUZA UREMBO ANUSURIKA KUUAWA BAADA YA KUKUTWA AKIMPAKA RANGI ZA KUCHA MKE WA BODABODA.
Na Anthony Mayunga-Mara
Oktoba 29,2012.

BODA BODA wa baiskeli mtaa wa Nyasho C,Manispaa ya Musoma anashikiliwa na jeshi la polisi kwa kujeruhi watu watatu waliokuwa wanamzuia asimkate kwa panga  muuza urembo baada ya kumkuta akimpaka mke wake rangi ya kucha.

Tukio hilo limetokea oktoba 27 majira ya saa 6 mchana mwaka huu katika maeneo ya Nyansho C’katika manispaa hiyo limethibitishwa na kamanda wa polisi wa mkoa wa Mara Absalom Mwakyoma.

Kamanda huyo amemtaja mtuhumiwa anayeshikiliwa kuwa  ni Chacha Wandiba Masincha(25)ambaye ni boda boda wa baiskeli ambaye aliwajeruhi kwa kuwakata na panga watu watatu ambao walifikishwa hospitali kwa matibabu  wakatibiwa na kuruhusiwa.

“Mtuhumiwa alimkuta muuza urembo ambaye aliombwa na mke wa mtuhumiwa Anita Chacha(19)akitaka kumpaka rangi mke wake alichukua panga kwa lengo la kumkata ndipo watu wakajitokeza kusaidia asilete madhara “alisema kamanda.

Alisema katika purukushani hizo watu watatu waliokatwa  ni Nyairabu Mwita(22)mkulima na mkazi wa Nyasho C’,Kichonge Wandiba(19)mkulima mkazi wa eneo hilo na Marwa Wambura(20)ambaye ni boda boda eneo hilo.

“Majeruhi wametibiwa katika kituo cha afya Nyasho na kuruhusiwa kuondoka kwa kuwa hali zao hazikuwa mbaya ,lakini mtuhumiwa tunaye na tunategemea kumfikisha mahakamani taratibu zikikamilika”alibainisha kamanda Mwakyoma.

Hata hivyo muuza urembo alikimbia na kuacha mali zake ambazo ziliharibiwa na mtuhumiwa ambaye alionekana kupandwa na hasira kwa kile kilichobainika kuwa ni wivu wa kimapenzi dhidi ya mkewe.

Baadhi ya mashuhuda walidai kuwa tatizo ni wivu wa kimapenzi na kutoaminiana kati yake na mkewe kwa kuwa mfumo wa wanawake kupakwa rangi ni la kawaida siku hizi.

Mwisho.

0 comments:

Post a Comment