WASHITAKIWA WA MENO YA TEMBO WAACHIWA KISHA KUKAMATWA TENA.
“ni waliokuwa polisi kagera na mfadhili wao,kesi yao imehamishiwa
mahakama ya mkoa”
Serengeti.
WATUHUMIWA wanne wa kesi no 1/2013 ya uhujumu uchumi inayowakabili
waliokuwa askari polisi mkoa wa Kagera na mfadhili wao wamefutiwa
mashitaka na mahakama ya wilaya ya Serengeti kisha wakakamatwa na
kupelekwa Musoma kwa ajili ya kufunguliwa mashitaka mapya.
Washitakiwa hao Boniphace John Kurwa(31)mkazi wa Geita,Gerald Tuji
Kabalega(33)aliyekuwa askari polisi Bukoba,David Duma
Dalema(36)aliyekuwa askari polisi Biharamulo na Mlangirwa Emmanuel
Paulo(32)maarufu kama Mnywarwanda mkazi wa Biharamulo ambaye anadaiwa
kuwa mfadhili wa mtandao huo waliachiwa machi 25,2013 kisha kukamatwa
na kufikishwa kituo cha Polisi Mugumu.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa washitakiwa hao watafunguliwa mashitaka
upya baada ya mwendesha mashitaka wa polisi Paskael Nkenyenge
kujiondoa na kumwachia mwendesha mashitaka wa serikali ili aandae
mashitaka upya dhidi ya watuhumiwa hao na kuhamishiwa Musoma.
Uamzi huo pia unatokana na upande wa mashitaka uliokuwa unaongozwa na
polisi kushindwa kutekeleza ushauri wa Hakimu mkazi mfawidhi wa
mahakama hiyo Amon Kahimba aliyewataka warekebishe mashitaka dhidi ya
washitakiwa kwa kuwa angeweza kuwaachia ,kutokana na udhaifu wake
,hali iliyopelekea Tanapa kwa kushirikiana na Mwanasheria wa serikali
wa mkoa wa Mara kuomba wafutiwe mashitaka kisha kuwakamata upya.
Awali mwendesha mashitaka wa polisi detektivu sajenti Nkenyenge
aliiambia mahakama kuwa januari 5 mwaka huu ,muda na wakati
usiojulikana mjini Mugumu washitakiwa walikamatwa kwa kula njama
kujihusisha na biashara haramu ya nyara za serikali kinyume cha
sheria.
Aliiambia mahakama kuwa siku hiyo walipatikana na meno ya tembo
vipande 18 vyenye zito wa kilogramu 104 yenye thamani ya sh,69,750,000
mali ya serikali.
Kutokana na hati ya mashitaka kusomwa mara nne katika mahakama hiyo
bila kufafanua kila mshitakiwa alipokamatiwa,Hakimu Kahimba machi
12,mwaka huu aliomba mpelelezi wa kesi hiyo,mkuu wa upepelezi mkoa wa
Mara kurekebisha hati hiyo kwa kubainisha kosa ,muda na sehemu
waliyokamatiwa ,kwa kuiacha hivyo kunatoa mwanya kwa mahakama
kuwaachia huru.
Hata hivyo mwendesha mashitaka huyo aliendelea kuacha hati ya
mashitaka kama ilivyokuwa ,hatua ilipelekea mwendesha mashitaka wa
serikali na waendesha mashitaka wa Tanapa kuwasilisha hati ya kufutwa
kesi na kukamatwa kwa washitakiwa na kuandaliwa mashitaka mengine
ambapo watafikishwa mahakama ya mkoa iliyoko mjini Musoma wakati
wowote.
Wakati huo huo watuhumiwa hao wamepandishwa katika mahakama ya hakimu
mkazi wa mkoa wa Mara wakikabiliwa na makosa matatu ya uhujumu uchumi.
Mbele ya hakimu mkazi wa mahakama hiyo Faiser Kahamba mwendesha
mashitaka wakili wa serikali Kainunura alisema washitakiwa hao
wanakabiliwa na mashitaka matatu,ya uhujumu uchumi.
Aliyataja mashitaka hayo kuwa ni kuingia ndani ya hifadhi za
taifa,kuwinda tembo na kukutwa na vipande 18 vya meno ya
tembo,wamepandishwa mahabusu hadi aprili 18,mwaka huu kesi hiyo
itakapotajwa tena.
Mwisho.
KUFUTWA KWA MATOKEO YA WATOTO 111 SEKONDARI MANCHIRA WAZAZI WAUNDA KAMATI KUFUATILIA
KUFUTWA KWA MATOKEO YA WATOTO 111
SEKONDARI MANCHIRA WAZAZI WAUNDA KAMATI KUFUATILIA .
Machi 13,2013
SERENGETI.
WAZAZI wa watoto waliokuwa wanafunzi wa Manchira
Sekondari wilayani Serengeti waliofutiwa matokeo kwa madai kuwa majibu yalikuwa
ya mfanano wameibuka na kulitaka baraza la mitihani kupitia upya uamzi wake.
Wanafunzi 111 kati ya 114 waliohitimu kidato cha nne mwaka
jana katika shule hiyo wamefutiwa matokeo na baraza la mitihani,taarifa ambayo
inakinzana na ya awali kuwa majibu yao hayakutolewa kwa sababu hawakuwa
wamelipa fedha ya mitihani.
Kutokana na utata huo wazazi
wamelazimika kuunda kamati kwa ajili ya kufuatilia ili kujua ukweli wa taarifa
ipi ni sahihi kwa kuwa awali wazazi waliambiwa hawakulipa fedha ya mitihani
ingawa baadhi walikiri kulipa na mkuu wa shule hakuweza kutoa risti na anasakwa
na polisi.
Katika barua hiyo iliyosainiwa na
wajumbe 7 chini ya Mwenyekiti wao Daniel Washa inashangazwa na baraza la
mitihani ambalo lilituma barua kwa mkuu wa shule ikibainisha kuwa matokeo
yamezuiliwa kwa kuwa watoto hawakulipia mitihani.
“Taarifa ilitolewa januari
25,2013 kuwa baraza limetoa barua ya maelezo hayo,februari 21 katika kikao cha
wazazi walikubali kulipa sh,35,000 kwa kila mzazi …februari 22 tukawa tumekusanya sh,3,080,000
zikatumwa baraza la mitihani kupitia akaunti Na.2011100238 NMB na baada ya
kupokea pesa machi 1 mkuu wa shule alidai alipokea barua
ambayo inaonekana ilikuwa imeandaliwa mapema kuwa wamefutiwa
majibu”imesema barua.
Wazazi hao wanahoji taarifa ya
baraza la mitihani kuwa oktoba 9,2012 watahiniwa wakifanya mtihani wa Kiswahili
msimamizi alikuta Toilet Paper yenye “Notes”za somo la Kiswahili kwenye dawati
la mtahiniwa S3684/0003 na S3684/0072/0098/0105 na 0111 walikutwa na karatasi
zenye notes za somo la Biology ndani ya chumba cha mtihani,lakini
hawakuchukuliwa hatua kama wakosaji.
“Kwa kuwa watahiniwa waliofutiwa
walikuwa vyumba vitatu tofauti ,je toilet paper zingeweza kuathiri vyumba
vyote?,kama vyanzo vya baraza vimetaja majibu kufanana kwa masomo ya Physics,Biology
na Chemistry ,iweje Kiswahili somo walilokutwa na Notes
halikuhusishwa”wamehoji.
Kamati hiyo inayoundwa na Daniel
Washa Mwenyekiti,Paulo Mtatiro Chacha(katibu)na wajumbe Simioni Nyatutu,Edina
Mahemba,Damiani Thobias,Japhet Maduhu na Samwel Omar wamebainisha kuwa shule
zilizofutiwa matokeo hutajwa kupitia vyombo vya habari lakini baraza liliomba
watume fedha watoe matokeo na baada ya kufanya hivyo wakadai matokeo yamefutwa.
Na kuwa Baraza la Mitihani
halikuhusisha ngazi ya wilaya husika kuhusiana na matokeo hayo ili kubaini
udanganyifu huo badala yake limeibuka na majibu ambayo yameacha mashaka kwa
kuwa walitaka malipo,wazazi wanahoji uhalali wa kupokea fedha za matokeo ambayo
yaliyokuwa yamefutwa.
Wanaiomba serikali kupitia baraza
la Mitihani kupitia upya uamzi wake wa kuwafutia matokeo watoto 111 wa
sekondari ya Manchira ,pia Tume iliyoundwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda ifanye
uchunguzi ili kubaini ukweli kwa kutumia barua za baraza za kudai malipo ili
watoe matokeo wakati wakijua hakuna matokeo yatakayotolewa.
Ofisa elimu Sekondari wilaya ya
Serengeti William Makunja amekiri kupokea nakala ya barua hiyo iliyotumwa na
wazazi kwenda Baraza la Mitihani na kudai kama wilaya nao wanafuatilia.
Juhudi za kumpata msemaji wa
baraza la Mitihani zinaendelea ili kutoa ufafanuzi wa malalamiko hayo.
Mwisho. inaendelea
WALINZI WAWILI WA BWAWA WAUAWA KWA KUPIGWA RISASI
WALINZI
WAWILI WA BWAWA WAUAWA KWA KUPIGWA RISASI.
Machi
12,2013.
WALINZI
wawili wa bwawa la maji la Manchira lililoko Mamlaka ya mji wa Mugumu wilayani
Serengeti wameuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana na maiti kutelekezwa
njiani ikiwa ni pamoja na pikipiki waliyokuwa nayo.
Tukio hilo
limethibitishwa na polisi wilayani Serengeti na viongozi wa vijiji vya
Kebosongo na Rwamchanga linadaiwa kutokea machi 11 majira kati ya saa 2:00
usiku jilani na sekondari ya Mugumu.
Waliouawa ni
Itinde Chacha(43)mkazi wa Kebosongo na William Kamambe(40) mkazi wa Rwamchanga
ambao wote walikuwa walinzi katika bwawa hilo.
Akisimulia
mkasa huo mdogo wa marehemu Itinde,Emmanuel Chacha alisema mazingira ya mauaji
hayo ni ya kupanga kwa kuwa hakuna kitu kilichochukuliwa ,ikiwa ni pamoja na
fedha ,simu ,sime,na pikipiki waliyokuwa nayo.
“Kaka yangu
tumeachana jana usiku akaaga anaenda kazini na hata mkewe alipompigia simu kama
anarudi nyumbani alisema hatorudi kwa kuwa alikuwa anatarajia kumsindikiza
mtoto wa kaka yetu kuwahi gari asubuhi”alisema kwa masikitiko.
Alisema
machi 12,2013 asubuhi alipata taarifa ya mauaji hayo,”hili huwezi sema ni
ujambazi kama hawajachukua kitu,lazima nyuma yake kuna kitu kinaendelea
,uchunguzi wa kina unatakiwa kufanyika”alisema.
Naye
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Rwamchanga Joseph Makuru alisema kuwa
Kamambe ambaye ni ndugu yake aliaga kuwa anaenda kazini ,lakini wamepokea
taarifa ya mauaji kwa masikitiko makubwa.
“Sisi
tumetoa maelezo polisi kuhusu hilo tukio lakini polisi wanatakiwa kufanya
uchunguzi wa kina kubaini maana mauaji haya ni ya kupangwa ….wote wamepigwa
kichwani risasi inasikitisha sana”alisema.
Polisi
wanamshikilia Chacha Nyamhanga kwa
uchunguzi huku wakiendelea na upelelezi ,mtuhumiwa alifukuzwa kazi ya ulinzi bwawani hapo,hata
hivyo inadaiwa alitengeneza chuki na marehemu hao.
“Inasemekana
alifikisha malalamiko yake kwa viongozi wa halmashauri akashindwa…akaenda mpaka
kwa wazee wa mila kumshitaki Itinde kuwa amefukuzisha kazi…nako akashindwa na
akaapa lazima kieleweke na hiyo ni tarehe
8 mwezi huu”kilisema chanzo kimoja.
“Sijui ni
bunduki za wanyama maana wamechakazwa sana …mashimo ni makubwa sana…wote
wamepigwa sehemu moja za kichwani…ni hatari”alisema daktari.
Mwisho.
MFADHILI WA MTANDAO WA MTANDAO WA UWINDAJI WA TEMBO APANDISHWA KIZIMBANI
Mlangirwa Emmanuel Paulo(32)maarufu kama (Mnyarwanda}akiwa chini ya ulinzi katika mahakama ya wilaya ya Serengeti akiteta jambo na ndugu yake |
Mlangirwa Emmanuel Paulo(32)maarufu kama (Mnyarwanda)akitafakari jambo wakati akiwa mahakama ya wilaya ya serengeti ambapo ameunganishwa na waliokuwa askari polisi kutoka Biharamulo na Bukoba walionaswa na vipande 18 vya meno ya tembo Mugumu na kumtaja kama mfadhili wao.
MFADHILI WA MTANDAO WA UWINDAJI WA TEMBO APANDISHWA KIZIMBANI.
Machi 12,2013.
SERENGETI.
MTUHUMIWA anayedaiwa kufadhili mtandao wa uwindaji na ununuzi
wa pembe za ndovu maeneo mbalimbali ya nchi
mwenye asili ya Rwanda amepandishwa katika mahakama ya wilaya ya
Serengeti akiunganishwa katika kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili waliokuwa
askari polisi kutoka mkoa wa Kagera.
Mtuhumiwa huyo aliyeunganishwa kesi ya uhujumu uchumi namba
1/2013 ni Mlangirwa Emmanuel Paulo(32)maarufu kama (Mnyarwanda)ambaye alitajwa
na watuhumiwa wengine kwenye kesi hiyo baada ya kukamatwa na vipande 18 vya
meno ya tembo kuwa ni mfadhili wa
mtandao wa ujangili na mnunuzi wa meno
ya tembo.
Mbele ya Hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama hiyo Amoni Kahimba
mwendesha mashitaka wa polisi Pascal Nkenyenge aliomba kubadilidha hati ya
mashitaka kwa kumwongeza mshitakiwa wanne baada ya kukamatwa.
Katika hati hiyo awali iliwataja washitakiwa watatu ambao
wamefikishwa mahakamani hapo mara tatu kuwa ni Boniphace John Kurwa (31)mkazi wa Geita
,Gerard Tuji Kabalega(33) David Duma Delama(36)ambao walikuwa askari polisi
Bukoba na Biharamulo.
Mwendesha mashitaka
aliiambia mahakama kuwa wanakabiliwa na mashitaka ya kula njama na kufanya
biasshara haramu ya nyara za serikali kinyume na kifungu namba 84(1)cha sheria
ya wanyama pori namba 5 ya mwaka 2009 ,pamoja na kifungu 14(b)na 57(1)na
60(20ya kuhujumu uchumi iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Akisoma maelezo ya
shitaka alisema januari 5 mwaka huu,muda na wakati usiojulikana mjini Mugumu
washitakiwa watatu walikutwa na meno ya tembo vipande 18 vyenye uzito wa kilo
104 vyenye thamani ya sh.67,750,000 mali
ya serikali.
Washitakiwa walikana shitaka moja la kula njama ya kufanya
biashara haramu ya nyara,na mashitaka mengine hawakutakiwa kujibu lolote kwa
kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kuyasikiliza mpaka kibali cha Mkurugenzi wa
mashitaka ambacho hakijatolewa.
.Kutokana na udhaifu wa hati ya mashitaka ilivyoandaliwa Hakimu Kahimba amelazimika kuonya upande wa mashitaka kuwa makini na kuagiza
kufanya marekebisho katika hati ya mashitaka hayo.
Aliwataka kufuata
taratibu za kisheria kwani mashitaka yaliyoandaliwa dhidi ya washitakiwa ni
dhaifu na hayatoshelezi kwani yanalenga kuifanya mahakama iweze kuwaachia washitakiwa.
“Mahakama iko hapa kutoa haki kwa pande zote ,nimekuwa wazi
kueleza jambo hili mbele ya mahakama,ningeweza kukaa kimya nikaendelea
kusikiliza kesi, si jambo la busara nikakaa bila kueleza mapungufu hayo,sipendi
mahakama siku ya kutoa hukumu ilaumiwe kwa mambo kama haya”alisema hakimu
Kahimba.
Alimwagiza mwendesha mashitaka atoe taarifa kwa mpelelezi wa
kesi,mpelelezi wa mkoa(RCO),wilaya(OC CID)na wote wanaohusika kufanya
marekebisho ya mashitaka .
Alibainisha kuwa mashitaka yajieleze wazi kila mtuhumiwa
alikamatwa anafanya nini,wapi na muda upi kwa kila kosa badala ya maelezo ya
jumla kuwa wote walikamatwa wanafanya makosa hayo.
Washitakiwa waliomba kulegezewa masharti ya dhamana ambapo
walikubaliwa na hakimu kwa kuruhusu kati ya wadhamini wawili mmoja atoke
Serengeti mwingine nje ya wilaya ,hata hivyo walishindwa kutimiza masharti na kesi imeahirishwa hadi march 25
mwaka huu na washitakiwa wamerudishwa mahabusu.
Masharti mengine yaliyobaki kama yalivyo ni kuwasilisha fedha
taslimu sh.31 milioni au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya kiasi
hicho iliyofanyiwa uthamini na mthamini wa serikali.
Washitakiwa wawili wakazi wa mjini Mugumu bado wanaendelea
kusakwa baada ya kutoroka siku ya tukio.
Mwisho.
POLISI WAKANUSHA KUKAMATA MAGAIDI WENYE SILAHA WAKIKUSUDIA KUMUUA PAROKO BUTIAMA
POLISI
WAKANUSHA KUKAMATA MAGAIDI WENYE SILAHA WAKIKUSUDIA KUUA PAROKO.
Na Anthony
Mayunga-Musoma
Machi
9,2013.
JESHI la
polisi Mkoani Mara limekanusha ujumbe unaosambazwa kwa njia ya simu kuwa limekamata magaidi wawili toka Somalia
wakiwa na bastola wilayani Butiama wakiwa na lengo la kumuua Paroko wa kanisa
Katoliki parokia ya Butiama Matheus raia wa Poland kuwa ni uongo.
Kamanda wa
polisi Mkoa wa Mara Absalom Mwakyoma alisema ujumbe huo hauna ukweli wowote na
unasambazwa na watu wenye ni uchochezi wa imani za kidini.
Alisema watu
wanaosambaza ujumbe huo wanalenga kusababisha migogoro ya kidini kati ya
wakristo na waislam kwa kuwa wanadai kuwa magaidi hao walikuwa wamejificha kwa
Shekhe mkuu wa wilaya ya Butiama kwa muda wa wiki nzima ili kutekeleza mauaji
hayo.
“Habari hizo
hazina ukweli wowote kwa kuwa jeshi la polisi halijamkamata msomali wala silaha
yoyote…huo uvumi unalenga kuwatia hofu wananchi”alisema.
Alitoa wito
kwa wananchi kutokuwa na hofu kuhusiana na watu wanaosambaza ujumbe wa
uchochezi na kuwa watoe ushirikiano kwa jeshi la polisi ili wahusika waweze
kukamatwa.
Paroko na
shehe hawakuweza kupatikana ili kuzungumzia taarifa hiyo,juhudi za kuwatafuta
zinaendelea.
Mwisho.
MAAFISA WA POLISI NA USALAMA WA TAIFA WALIOKUTWANWAKICHIMBA DHAHABU HIFADHINI WAPANDISHWA KIZIMBANI
MAAFISA WA USALAMA WALIOKUTWA WAKICHIMBA DHAHABU WAPANDISHWA
KIZIMBANI.
Na Mwandishi wetu- Machi 7,2013.
MUSOMA.
HATIMAYE maafisa wa polisi na usalama wa Taifa waliokutwa wakichimba
dhahabu katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara wamefikishwa
katika mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Mara wakikabiliwa na
makosa 6 ya uhujumu uchumi.
Na Mwandishi wetu- Machi 7,2013.
MUSOMA.
HATIMAYE maafisa wa polisi na usalama wa Taifa waliokutwa wakichimba
dhahabu katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara wamefikishwa
katika mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Mara wakikabiliwa na
makosa 6 ya uhujumu uchumi.
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni karibu mwaka mzima toka wamekamatwa katika tukio hilo lililohusisha raia watano ambao walifikishwa mahakamani baada ya siku 2 toka wamekamatwa,huku maafisa hao wakihamishwa vituo vya kazi.
Waliofikishwa mbele ya mahakama hiyo ni SSP Paulo Cathbert
Mng’ong’o(56)aliyekuwa Ocd Serengeti,Said Mussa(44)aliyekuwa ofisa
usalama wa Taifa na dreva wa polisi E 933 koplo Frematus
Fredrick(42).
Ilidaiwa na mwendesha mashitaka wakili wa serikali Valensi Mahenga
mbele ya hakimu mkazi wa mahakama hiyo Emmanuel Loitare Ngigwana
walitenda makosa hayo machi 24,2012 katika eneo la kilima fedha ndani
ya hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Wakili huyo aliyataja makosa yanayowakabili kuwa ni kula njama kwa
lengo la kufanya kosa na kutenda kosa ,kuingia hifadhini kinyume cha
sheria.
Makosa mengine ni kukutwa na silaha ndani ya hifadhi kinyume cha
sheria ,kufanya uchimbaji wa dhahabu ndani ya hifadhi ya taifa kinyume
cha sheria,kupatikana na dhahabu ambayo haijasafishwa kinyume cha
sheria na kukutwa na zana za milipuko ndani ya hifadhi kinyume cha
sheria.
Washitakiwa wamekana mashitaka na wako nje kwa dhamana na kesi hiyo
itatajwa machi 19 mwaka huu.
Katika hatua nyingine jeshi hilo limemfukuza kazi aliyekuwa dreva wa
polisi koplo Frematus Fredrick mwenye namba E 933 huku aliyekuwa SSP
Mng’ong’o akiwa amesimamishwa kazi kutokana na cheo chake.
Katika tukio hilo maafisa hao pi a walikamatwa na raia watano
walioingia nao ndani ya hifadhi kwa ajili ya kutenda uharifu huo ambao
tayari walishafikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi mfawidhi wa
wilaya ya Serengeti.
Washitakiwa wengine ambao ni raia walifikishwa mbele ya hakimu wa
mahakama ya wilaya Amon Kahimba machi 26,2012 wakikabiliwa na makosa 5
, huku kwa upande wa maafisa hao ikidaiwa kuwa uchunguzi na taratibu
za kijeshi zilikuwa zinaendelea.
Makosa hayo ikiwa ni kuingia ndani ya hifadhi ya Taifa bila
kibali,kupatikana na silaha bila kibali,kufanya uchimbaji wa dhahabu
ndani ya hifadhi bila kibali na kupatikana namifuko 10 mawe ya madini
ya dhahabu kinyume cha sheria. Kosa lingine likiwa ni kukutwa na vifaa
vya milipuko ndani yahifadhi
.
Washitakiwa hao ni Mniko Nyamhanga Mwita (30)mkazi wa Matare,Jonas
Marwa Chacha (42)mkazi wa Mugumu mjini,Maiga James Maganjala(26)mkazi
wa Bunda .
Wengine ni Mwita William King’eti(30)mkazi wa Mugumu na Alex
Peter(29)Mwalimu wa sekondari Kambarage iliyoko mjini Mugumu
Kesi hiyo inatarajiwa kuanza kusikilizwa mwezi aprili mwaka huu baada
ya upande wa mashitaka kudai upelelezi umekamilika.
Mwisho.
Subscribe to:
Posts (Atom)