NDUGU MMOJA AFA WAWILI WAJERUHIWA
WAKIDAINA SH.20,000
Serengeti:DENI la sh.20.000
limesababisha ndugu watatu wa kitongoji
cha Nyasuma kijiji cha Borenga kata ya Kisaka wilaya ya Serengeti kukatana
mapanga na mmoja kufariki huku wawili wakilazwa katika hospitali teule ya
Nyerere ddh chini ya ulinzi wakiwa na
hali mbaya.
Tukio hilo la aina yakelinadaiwa
kutokea septemba 23 majira ya saa 12:00 jioni nyumbani kwa Muhochi Hacheri
limethibitishwa na polisi na uongozi wa hospitali teule ya Nyerere ddh,na
kumtaja aliyefariki kuwa ni Julius Mwikwabe (20)aliyefariki,na majeruhi hao
kuwa ni Mwikwabe Mwikwabe(40)Magubo Mwikwabe(29).
Magubo ambaye ni mtuhumiwa akiwa
amelazwa kitanda namba 8 na kaka yake wakiuguza majeraha alisema ,alikuwa
akimdai mdogo ambaye ni marehemu
sh,20,000 baada ya kumuuzia baiskeli aina ya Swala kwa sh,40,000 na
kulipa nusu ,alipomdai ndipo kukaibuka ugomvi na kusababisha kifo na majeruhi
kwao .
“Toka mwezi mei namdai pesa hizo
akawa mkaidi…septemba 19 nilikwenda kudai akaahidi kesho yake angelipa hakulipa…septemba 23 tulipokutana akanitolea
majibu mabaya…nilimchapa fimbo nne kama mdogo wangu…akatoka kimya akaenda kunoa
panga na jioni akaja nikiwa kwa Hacheri na kufika na kunikata kwa panga mgongoni
chini ya bega la kushoto”alisema majeruhi huyo.
Alisema ndipo naye akachukua
panga alilokuwa nalo kwa nia ya kujihami,lakini mdogo wake huyo ambaye ni
marehemu alinyanyua panga amkate tena,”aliponyanyua mkono anikate nikamkata
mkono wa kushoto ukaning’inia na damu zikawa zinavuja sana..alifariki baada ya
kufika hospitalini”alisema.
Naye Mwikwabe Mwikwabe kaka
mkubwa wa familia hiyo alisema ,akiwa nyumbani kwake alipata taarifa ya ugomvi
wa wadogo zake ,”lengo likiwa ni kuwaamua…nikiwa katika pilika pilika hizo
Julius(marehemu)alinikata sehemu ya bega la kushoto kwa nyuma huku akidai ni
bahati mbaya,”alibainisha.
Alisema kitendo cha kukatwa
kilimfanya aanze kujihudumia huku wadogo zake wakiendelea kupambana na matokeo
ya ugomvi huo wamempoteza mdogo wao.
Muuguzi wa zamu wodi ya wanaume
Hellen Mosha alisema kuwa Julius alifariki muda mfupi kabla ya kupata matibabu
na chanzo kikiwa ni kuvuja damu sana kutokana na kuchelewa kufikishwa hospitalini.
Polisi wilayani hapa wamesema
watuhumiwa hao wawili wanatibiwa wakiwa chini ya ulinzi wakati uchunguzi zaidi
ukiendelea wa kubaini mhusika aweze kufikishwa mahakamania.
Mwisho.
MWIKWABE MWIKABE NA MASUBO MWIKWABE AMBAO NI MTU NA MDOGO WAKE WAKAZI WA KIJIJI CHA BORENGA KATA YA KISAKA WILAYANI SERENGETI WAKIWA WAMELAZWA WODI LA WANAUME KITANDA NAMBA 8 HOSPITALI TEULE YA NYERERE DDH KUFUATIA UGOMVI BAINA YAO ULISABABISHWA NA DENI LA SH.20.000 NA KUPELEKEA MDOGO WAO JULIUS MWIKWABE KUFARIKI .
WAMELAZWA WAKIWA WAMEFUNGWA PINGU KUTOKANA NA TUHUMA ZA MAUAJI YA MDOGO WAO