AKATA MIGUU NG’OMBE 27 BAADA YAJARIBIO LA
KUMUUA MAMA YAKE KUSHINDWA,
“Mtuhumiwa
aliiba kuku anayeatamia na kuuza kwa sh.7.000 akanunua gongo,alipoulizwa
akampiga mama yake aliyejiokoa kwa kumkamata nyeti kijana wake”
Septemba
21,2013
MKAZI wa kijiji cha Bwitengi kata ya
Manchira wilayani Serengeti Witiribani Thomas Barangwa (30)anatuhumiwa
kukata miguu ng’ombe 27 wenye thamani ya
zaidi ya sh,mil.5kufuatia ugomvi baina yake na mama yake aliyemtuhumu kuiba na
kuuza kuku kwa ajili ya kupata pesa ya
kununulia pombe.
Tukio hilo ambalo
limezua mjadala kutoka kwa wananchi
linadaiwa kutokea septemba 19 majira ya saa 7:00 usiku mwaka huu katika
kitongoji cha Mewara limethibitishwa na Mwenyekiti na ofisa mtendaji wa serikali ya kijiji Daud Manteni na Antony
Makuru,na kuwa mtuhumiwa ametoroka anatafutwa.
Akielezea mkasa
huo ofisa mtendaji alisema mtuhumiwa huyo aliamua kukata miguu ng’ombe hao
baada ya kumsaka mama yake mzazi NyambiseThomas Barangwa na dada yake Loyce
Thomas Barangwa waliompiga kutokana na kosa la kuiba kuku aliyekuwa ameatamia
na kumuuza kwa sh.7.000 na kwenda kunywa
pombe za kienyeji.
“Katika ugomvi huo
mtuhumiwa huyo alifanikiwa kumwangusha mama yake na kuanza kumkaba shingo…dada
yake akaingilia kati, hata hivyo mama yake alipoona amezidiwa akamkaba sehemu
za siri kwa nguvu na kumwachia…mtuhumiwa akakimbilia ndani na kuchukua silaha
na kuanza kuwasaka awakate”alisema.
Makuru alisema
mtuhumiwa alichukua panga kwa lengo la kumuua mama na dada yake ambao
walikimbia na kujificha,na wanakijiji wakijitokeza kwa wingi kutoa msaada.
“Baada ya kuwakosa
na kuona wananchi wamejitokeza kuwasaidia hasira zake zilihamia zizini na
kuanza kukata ng’ombe mmoja baada ya mwingine mali ya baba yake…waliowekeshwa na
wa kwake watatu hakuwagusa”alisema.
Baadhi ya
mashuhuda walisema kuwa mtuhumiwa aliuza kuku anayeatamia na kuwa mchezo huo
ulikuwa wa mara kwa mara na fedha zote akazitumia kwa kununua gongo,na
alipoulizwa alikuwa mkali na kuwatishia.
“Akishakunywa pombe
ni mkali sana si kwa mama yake wala majilani…na anatumia nafasi hiyo kwa kuwa
wanaishi na mama yake tu…kwa kweli tukio alilofanya ni la kipekee na halijawahi
kutokea kijijini hapa”alibainisha jilani ambaye hakutaka jina lake liandikwe.
Kutokana na tukio
hilo wafanya biashara wa bucha wanadaiwa kununua ng’ombe hao kwa bei ya chini
kwa kuwa hawakuwa na uwezekano wa kupona kutokana na jinsi walivyokuwa
wamejeruhiwa,pia wakazi wa kijiji hicho walinufaika kwa kupata nyama.
Polisi wilayani
hapa wanaendelea na msako dhidi ya mtuhumiwa na wanaomba wananchi watoe
ushirikiano ili aweze kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya dola.
Mwisho.