Padri Alois Magabe wa kanisa Katoliki Mugumu wilayani Serengeti
Serengeti:Nchi za
Magharibi kutoa misaada yenye masharti
ya kuruhusu ushoga kwa nchi za Kiafrika ni matokeo ya kushindwa kutumia
rasilimali walizo nazo kwa ajili ya kuendesha nchi zao.
Hivi karibuni kumekuwa na mjadala kwa nchi nyingi za
Kiafrika kutokana na shinikizo la Nchi za Magharibi kuzishinikiza nchi za
kiafrika ili zipate misaada zinatakiwa kukubali ndoa za jinsia moja.
Paroko wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Fransisco wa
Asizi Mugumu wilayani Serengeti Alois Magabe hivi karibuni akihubiri wakati wa misa ya
Ekaristi Takatifu alisema utegemezi wa misaada ndiyo chanzo cha nchi hizo kutoa
masharti yanayokinzana na maagizo ya Mungu kwa nchi za Kiafrika.
“Ukristo umeanzia nchi hizo za Magharibi miaka zaidi ya elfu
mbili iliyopita….licha ya kujua masharti wanayoyatoa yanakinzana na maagizo ya
Mungu aliyeweka ndoa ya mme na mke…..leo nchi kama za Marekani na Uingereza na
washirika wao wanaziwekea masharti hayo nchi zinazotaka misaada…sababu kubwa ni
udhaifu wan chi hizi zenye rasilimali tele kutegemea misaada”alisema.
Alisema masharti kama waliyotoa kwa Uganda ni ishara tosha
kuwa hawamuogopi Mungu ,na kuzitaka nchi zingine kuungana na msimamo wa Uganda
kupinga ushoga kwa kuikataa misaada hiyo inayokweza utu wao ”misaada kama hii
hatuhitaki bora ipotelee mbali huko”alisema na kushangiliwa.
Hata hivyo aliwataka viongozi wan chi hizo kubadili mitizamo
ya kutaka kusaidiwa wakati utajiri walionao unazidi hata nchi hizo zinazotoa
misaada kwa masharti,kwa kuwa wao wana nidhamu ya kukusanya na kutumia si kama
ilivyo kwa nchi za kiafrika hakuna nidhamu ya matumizi ya mali za umma.
“Hiyo misaada yenye masharti wanayotaka kutoa kwa nchi zetu
hizi wamekusanya Afrika kiujanja ujanja wanataka kuileta kwa masharti ya
kijinga kijinga kisha wapata nafasi ya kuchota rasimali zetu”alisema.
Katika hatua nyingine alitaka serikali wilayani hapo
kuhakikisha inamaliza mgogoro wa ardhi kati ya kigango cha Nyamburi cha kanisa
Katoliki na serikali ya kijiji ambayo imeanzisha mnada kwenye eneo la kanisa
,hatua ambayo inaweza kuleta uvunjifu wa amani.
“Suala hili toka mwaka jana oktoba nimewaeleza lakini hakuna
utekelezaji…..eneo la kanisa limeporwa kwa nguvu na baadhi ya viongozi wabovu
wanaotumia nafasi zao vibaya ili kutafuta kura katika uchaguzi ujao….kwa hili
nimewaandikia polisi nao wameahidi kufuatilia,maana suala hilo linaweza
kupelekea uvunjifu wa amani”alibainisha.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment