Waandishi wa habari wakiwa kazini
Na Elias Msuya, Mwananchi
Posted Jumapili,Juni1 2014 saa 24:0 AM
Posted Jumapili,Juni1 2014 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Yaandaa programu maalumu ya
kuwawezesha waandishi wa habari kuripoti habari za uchunguzi wa dawa za
kulevya.
Dar es Salam. Mfuko wa Habari
Tanzania (TMF) umeanzisha programu ya uandishi wa habari za uchunguzi kuhusu
mapambano ya dawa za kulevya nchini.
Akizungumza juzi katika uzinduzi wa
programu tano zinazofadhiliwa na TMF, mwakilishi wa kitengo cha habari cha
Umoja wa Mataifa nchini, Stella Vuzo alisema programu hiyo imechaguliwa mahsusi
kutokana na tatizo la dawa za kulevya kukithiri nchini.
“Tanzania ni kati ya nchi za Afrika
zilizoathirika na matumizi na usafirishaji wa dawa za kulevya. Takwimu za
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii zinaonyesha kuwa jumla ya watumiaji 20,626
walipatiwa matibabu katika vituo vya afya kati ya mwaka 2008 hadi 2011,” alisema
Vuzo na kuongeza:
“Takwimu za Jeshi la Polisi
zinazonyesha kuwa, tangu mwaka 2010 hadi Mei 2013, jumla ya kilo 742 za
heroini, kilo 348 za cocaine, kilo 77 za bangi na kilo 16,335 za mirungi
zilikamatwa.”
Vuzo aliongeza kuwa hadi Julai 2013,
Watanzania 247 walikamatwa wakisafirisha dawa hizo katika nchi za Mauritius,
Umoja wa Falme za Kiarabu, China, Pakistan, Brazil na Afrika Kusini. “Kwa
takwimu za ndani, kati ya kesi 423 za matumizi na usafirishaji wa dawa za
kulevya ni kesi moja tu iliyoamuliwa kati ya mwaka 2005 hadi 2013. Kuna
ongezeko la vijana wanaosafirisha dawa hizo kwa matumaini ya kutajirika,”
alisema Vuzo.
Hata hivyo, Kamishna wa Kitengo cha
kupambana na dawa za kulevya cha Jeshi la Polisi, Godfrey Nzowa aliyehudhuria
hafla hiyo, alisema tatizo hilo sasa linapungua kutokana na mikakati thabiti ya
jeshi.
“Kwa sasa Jeshi la Polisi tunajivuna
kuwa tumeidhibiti biashara ya dawa za kulevya kwa kiasi kikubwa. Uthibitisho ni
kupanda bei kwa dawa hizo. Kwa sasa kilo ya cocaine inafikia hadi Sh50 milioni
na heroini hadi Sh45 milioni. Hazipatikani kirahisi kwa sababu tumedhibiti,”
alisema Nzowa na kuongeza:
“Ni kweli biashara hii inafanywa na
baadhi ya vigogo wa Serikali na wafanyabiashara wakubwa. Lakini wana mbinu kali
sana, wako tayari kwa lolote.”
Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia
Kabaka aliyekuwa mgeni rasmi wa hafla hiyo, aliwataka waandishi wa habari
kutumia kila mbinu ya taaluma yao kuibua mambo yatakayoisadia Serikali
kupambana na uhalifu.
Awali, akimkaribisha Waziri Kabaka,
Mkurugenzi wa TMF, Ernest Sungura alisema lengo la mfuko huo ni kuisaidia
Serikali kuleta maisha bora kwa Watanzania.
“Tofauti na taasisi nyingine, TMF
tunafadhili waandishi wa habari kuandika habari za vijijini zaidi kuliko mijini
tu. tunataka sauti zao nao zisikike,” alisema Sungura.
Mbali na program ya dawa kulevya, TMF pia inafadhili program
za utafutaji na uchimbaji wa mafuta, gesi na madini, Ukatili wa jinsia,
Watangazaji wanawake na Wapiga picha za televisheni.
0 comments:
Post a Comment