ALIYEKUTWA NA MENO YA
TEMBO AHUKUMIWA MIAKA 8 JELA.
Serengeti:MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi mfawidhi wa
wilaya ya Serengeti imemhukumu Idd Abdallah
Adamu (39 ) mkazi wa Nyakato Mwanza miaka 8 jela kwa kosa la kupatikana na meno ya tembo kilo 46 yenye thamani ya sh, 26,250,000 .
Katika kesi hiyo ya uhujumu
uchumi namba 59/2011 washitakiwa wengine kwenye shitaka hilo Lameck
James (29) mkazi wa Sirari, Kasika John(46) mkazi wa Ushashi Bunda na Mwita
John(44) mkazi wa kijiji cha Kibeyo wilaya ya Serengeti wameachiwa huru kutokana na udhaifu wa polisi
kushindwa kuwasilisha fedha sh.3,835,000 walizokutwa nazo mahakamani kama ushahidi siku ya tukio.
Hakimu Amon Kahimba wa mahakama
hiyo alisema,mshitakiwa Adamu amekumbwa na adhabu kufuatia ushahidi
uliowasilishwa mahakamani hapo kuanzia maelezo ya polisi ,mahakamani na
mashahidi kuwa vipande vinne vya meno ya tembo vilikutwa ndani ya chumba
alichokuwa amelala nyumba ya wageni ya Leopard.
Na kuwa alikiri kununua meno hayo,kwa
washitakiwa wawili kwa sh,2,400,000 na
washitakiwa Lameck James na Kasika John walikiri kununua vipande hivyo vya meno kwa mshitakiwa wanne Mwita John
kwa sh,200,000,na fedha walizokutwa nazo hotelini sh,3,835,000 hazikuwasilishwa
mahakamani kama kielelezo licha ya washitakiwa kuzidai.
“Kutokana na maelezo yote ya
ushahidi na washitakiwa ,mahakama inamhukumu Idd Abdallah miaka minane jela…na
wengine wanaachiwa huru kutokana na uzembe wa polisi..wote hawa wangehukumiwa
kama mpelelezi wa kesi na aliyekuwa Oc Cid wilayani hapo kwa sasa Mkuu wa
Operesheni Mkoani Arusha Paul Ngonyani aliyewakamata,kuwapekua,lakini hakufika
kutoa ushahidi mahakamani licha ya kuitwa na wala fedha alizowakutana nazo
hazikuwasilishwa kama ushahidi”alisema.
Alikwenda mbali hakimu huyo na
kudai kuwa kosa la kujihusisha na biashara ya meno ya tembo mazingira yake wangekutwa na mzigo au pesa,lakini wao
walikutwa na pesa katika nyumba ya kulala wageni ya Galaxy Motel ,lakini
hazikuwasilishwa mahakamani.
Aliomba jeshi la polisi nchini
liwachukulia hatua kali Paulo Ngonyani ,kwa kushindwa kufika kutoa ushahidi
kwenye kesi hiyo licha ya kuitwa mara tatu,na mpelelezi wa shitaka hilo Ditektivu
Sajenti Yona,kwa kutowasilisha fedha za
washitakiwa ambazo wamezidai na mahakama ikaagiza ziwasilishwe mahakamani..
Mapema mwendesha mashitaka
inspekta msaidizi wa Polisi Abdallah Idd aliitaka mahakama hiyo kutoa adhabu
kali kwa mshitakiwa ili liwe fundisho kwa wengine kwa kuwa makosa ya uhujumu
uchumi yamekithiri hapa nchini.
Katika utetezi wake Adamu aliomba
ahurumiwe kwa kuwa ni kosa lake la kwanza ,ana watoto 5,mke na watu
wanaomtegemea.
Februari 18,2013 katika mahakama hiyo mshitakiwa
huyo aliyehukumiwa aliyekuwa akijifanya Mmachinga anayetembeza vyombo kutoka
Mwanza aliachiwa huru na mahakama hiyo
katika kesi 184/2011 ya uhujumu uchumi baada ya kukamatwa katika nyumba
ya kulala wageni ya Silent Inn mjini Mugumu wakiwa na meno mawili ya tembo.
Katika kesi hiyo ilimhusisha
mmiliki wa nyumba hiyo Julius Mwita Marwa(43)waliachiwa na Hakimu Amon Kahimba
kwa kutumia kifungu cha sheria namba 235 cha mwenendo wa makosa ya jinai
kilichorekebishwa mwaka 2002 kwa madai kuwa upande wa mashitaka ulikuwa dhaifu.
Mwisho.