TANZANIAYATILIANASAINI NA THAILAND MKATABA
WA KULINDA MALIASILI NA KUKOMESHA
UJANGILI,
Julai 31,2013.
Serengeti:SERIKALI ya Tanzania
imetiliana saini mkataba wa maelewano wa
miaka mitatu wa ushirikiano wa kulinda na kuendeleza maliasili na Utalii na
Jamhuri ya Kifalme ya watu wa Thailand.
Mkataba huo umesainiwa na Waziri
wa Maliasili na Utalii balozi Khamisi Kagasheki kwa niaba ya serikali ya
Tanzania na Naibu Waziri Mkuu wa
Thailand Plodprasop Suraswad aliyeambatana na Waziri Mkuu wa Thailand
Yingluck Shinawatra kwenye ukumbi wa Four Session Safari Hotel Ltd iliyoko hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Akizungumzia manufaa ya mkataba
huo Waziri Kagasheki amesema hatua hiyo itasaidia taifa kuongeza mapato kupitia
sekta ya Maliasili kwa kuongeza watalii kutoka milioni moja kwa sasa kama
ilivyo kwa nchi ya Thailand pamoja na raslimali chache wanapata watalii hadi
milioni 22 kwa mwaka.
“Tunataka mchango wa maliasili katika pato la Taifa utoke asilimia 17 …hali hiyo ikienda sambamba na kuongeza pato
la wananchi….maana Thailand kupitia utalii pato la Mwananchi ni dola 5,000 kwa
mwaka …na ndio mpango wa taifa wa
20-25”alisema.
Waziri wa uwezeshaji na Uwekezaji
Dk,Mary Nagu amesema mkataba huo
unafungua fursa za uwekezaji ambao utainua pato la taifa katika sekta ya
utalii,pia kilimo na madini.
“Tanzania tuna fursa nyingi
lakini hatujafanya vizuri kwa ajili ya kujipatia mapato….tuna maliasili nzuri
na kubwa tunawazidi Kenya …lakini wao wana vitanda 11,000 wakati sisi
tunavitanda 6,000 sasa tunakusudia kukuza kwa kasi sekta hii kwa kushirikiana
na nchi ambazo zinamwelekeo na zinazofanya vizuri”alisema.
Alisema ili kuhakikisha
watanzania wananufaika na uwekezaji kama huo ,kwa upande wa madini serikali
haitauza madini ghafi bali kuyatengeneza na kuwa vito ili yaongezewe thamani
,na watanzania wakipewa fursa ya kwanza kwa kuangalia watakavyonufaika.
Alisema ziara hiyo imekuja siku
chache baada ya viongozi wa mataifa ya China,Marekani na Uingereza kutiliana
mikataba ya kimaendeleo na taifa la Tanzania..
Mkurugenzi wa Wanyamapori
Tanzania Profesa Alexander Songorwa
alisema ,wanategemea kuimarisha utalii na kupunguza tatizo la ujangili kwa kuwa
nchi hizo zote zitahusika katika masuala ya ulinzi na usimamizi.
“Soko la meno ya Tembo kutoka
Tanzania ni kubwa nchini Thailand na China …kwa mkataba huu sasa nao
watashiriki kukabiliana na vitendo hivyo vya uharifu,na hiyo nafasi itatusaidia
sisi kudhibiti hali hiyo…maana ujangili wa tembo ni changamoto kubwa kwa
uhifadhi hapa Tanzania”alisema.
Mapema Mhifadhi Mkuu wa hifadhi
ya Taifa ya Serengeti William Mwakilema akitoa taarifa ya hifadhi hiyo alisema
mbali na kuwa kivutio kikubwa kwa wageni,bali wanakabiliwa nanchangamoto za
askari wachache wa ulinzi wa wanyama pori,nyumba za askari ,maji ,barabara za
ndani na jamii zinazowazunguka .
Kwa upande wa falme za Thailand
walisema ,Raslimali za Tanzania zikilindwa na kusimamiwa vema zitasaidia kuinua
uchumi kwa kasi kubwa,kwa kuwa wana vitu ambavyo havipo katika maeneo
mengine,lakini hawajafanya vizuri.
Mwisho.
SAINI YA MAKUBALIANO
WAZIRI MKUU WA THAILAND YINGLUCK SHANAWATRA AKIANGALIA MCHORO WA MZUNGUKO WA NYUMBU
WANAKABIDHIANA MKATABA WA MAELEWANO