Na Editha Majura, Mwananchi
Posted Jumapili,Marchi23 2014 saa 11:8 AM
Posted Jumapili,Marchi23 2014 saa 11:8 AM
Kwa ufupi
Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa
Mwesiga Baregu alisema alitarajia Rais Kikwete angezindua Bunge Maalumu
na siyo kutoa maagizo na vitisho kwa wajumbe.
Dodoma. Siku moja baada ya Rais
Jakaya Kikwete kuzindua Bunge na kuponda ripoti ya Tume ya Mabadiliko
ya Katiba, Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Joseph Warioba amesema jukumu
walilopewa kwa mujibu wa sheria wamelikamilisha na wanawaachia wananchi
waamue.
Akizungumza na Mwananchi jana asubuhi, Jaji
Warioba alisema alichokizungumza Rais Kikwete ni maoni yake na kwamba
hawezi kuyajadili.
“Rais Kikwete alichozungumza ni maoni yake, kwa sasa sipendi kuyazungumzia hayo, ” Jaji Warioba alieleza.
Alisema wamemaliza jukumu walilopewa na kwamba sasa jukumu lote lipo mikononi mwa Bunge.
Jaji Warioba alisema Tume yake ilikusanya maoni
kutoka kwa wananchi, mabaraza ya wilaya ya Katiba na Taasisi mbalimbali,
wakatengeneza rasimu ambayo sasa wameikabidhi kwa Bunge Maalumu la
Katiba.
Jaji Warioba pia alikataa kuzungumzia zogo
lililoibuka bungeni na kusababisha rasimu kuwasilishwa Jumatano, baada
ya kikao cha Jumanne kuvunjika.
Hali hiyo ilitokana na UKAWA kudai muda wa saa
1:30 uliokuwa umepangwa Jaji Warioba ahutubie bungeni uongezwe na kanuni
inayoelekeza Rais Jakaya Kikwete ahutubie kabla Jaji Warioba
hajawasilisha rasimu izingatiwe, baada ya kutangazwa kuwa Rais
angehutubia baada ya rasimu kuwasilishwa.
Profesa Baregu
Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa
Mwesiga Baregu alisema alitarajia Rais Kikwete angezindua Bunge Maalumu
na siyo kutoa maagizo na vitisho kwa wajumbe.
Alisema hajui lengo la Rais kufanya alichofanya
lakini ana hakika kwa kutoa ufafanuzi wa hoja zilizotokana na maoni ya
wananchi ndani ya rasimu, ameingilia kazi za Tume na hivyo amevunja
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba (Sura ya 83 toleo la mwaka 2012),
inayosema:
“21.-(b) atakayejifanya kuwa mjumbe wa Tume au
Sekretarieti; au (c) atakayeendesha programu ya elimu juu ya mabadiliko
ya katiba kinyume na masharti ya sheria hii, atakuwa ametenda kosa.
(3) atakayetiwa hatiani kwa kutenda kosa kinyume
na Sheria hii, atawajibika kulipa faini isiyopungua Sh2,000,000 (milioni
mbili) na isiyozidi Sh5,000,000 (milioni tano) au kifungo kwa muda
usiopungua mwaka mmoja na usiozidi miaka mitatu au adhabu zote mbili.
Sheria hiyo inaendelea kuelekeza, (4)
Hatua zozote zilizochukuliwa chini ya kifungu hiki hazitachukuliwa kuwa
zimefikia ukomo na zitaendelea kuwa na nguvu ya kisheria hata baada ya
Sheria hii kukoma kutumika.”
Profesa Baregu alisema sheria imezungumzia mtu yeyote, hajui kwa Rais inakuwaje.
“Sijui ameona Bunge halitoshi, haliwezi kung’amua
mambo au limepungukiwa kiasi cha kushindwa kumudu majukumu yake? Sielewi
ila amevunja sheria na amelivunjia Bunge hadhi yake kiasi kwamba hata
kazi yake inaweza isiaminike,” alieleza.
Profesa Baregu alisema Rais Kikwete amejipa jukumu la kujibu na kujadili hoja za rasimu na hivyo kuwa sehemu ya Bunge Maalumu.
Alisema wakati wabunge wanahimizwa kutumia mfumo
wa maafikiano katika kuamua mambo, Rais amewajengea msingi wa mgawanyiko
na chuki, hali itakayoathiri mpango wa kulipatia taifa Katiba
inayotokana na wananchi.
Profesa Baregu alitaja baadhi ya kauli za Rais
Kikwete ambazo zinaweza kuathiri mchakato kuwa ni kujirudia kwa kauli;
“Nyie ndiyo mnaotunga Katiba (Wabunge wa Bunge Maalumu) kazi imebaki
kwenu.” na maelekezo kwamba serikali tatu zitapatikana, lakini labda
baada ya yeye (Rais Kikwete) kuondoka madarakani.
Jaji Ramadhan
Jaji Ramadhani alisema wao Tume wamemaliza kazi
yao na kwamba sasa wanawaachia wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba na
wananchi waamue.
“Tumemaliza kazi yetu na sasa tunawaachia wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba na wananchi,” alisema.
Hata hivyo, alisema ikitokea wajumbe wa Bunge hilo
wakihitaji ufafanuzi wa jambo lolote, yeye binafsi anaahidi kutoa
ushirikiano.
Kuhusu hotuba ya Rais Kikwete bungeni juzi,
alisema yeye alikuwa Arusha akishughulika na vikao vya Mahakama ya
Kimataifa ya Haki za Binadamu na kwamba hakuwa amepata muda wa kuipitia
na kuitafakari kwa kiwango cha kuizungumzia.
“Ninasoma na kuitazama kupitia vyombo vya habari
na ninafahamu nyie wanahabari huwa mnalenga pale palipowakuna. Hivyo
nikitulia na kupata hotuba halisi aliyotoa nikaitafakari;
nitaizungumzia,” alieleza.
Rais Kikwete akizindua Bunge juzi mjini Dodoma, alisema rasimu
ya pili iliyowasilishwa bungeni na Jaji Warioba ina makosa mengi ya
kiuandishi.
Alisema ina mambo mengi, baadhi yalitakiwa kuwekwa kwenye Sheria.
“Mbolea, mbegu, pembejeo vyote vimewekwa humo,
hata umri na haki ya mtoto kupewa jina vinawekwa humo, yakiwekwa yote
kama yalivyo, serikali haitaweza kuyatekeleza itashtakiwa mahakamani
kila wakati,” alieleza.
Rais Kikwete aliwataka wajumbe wa Bunge Maalumu
kusoma neno kwa neno, mstari kwa mstari na kujiridhisha na mambo
watakayoidhinisha yaingie kwenye Katiba itakayopendekezwa.
Alisema watakachoona kinafaa kurekebishwa,
kuboreshwa au kufutwa wasisite kufanya hivyo kwa sababu inatakiwa Katiba
bora, inayotekelezeka na ambayo haitalalamikiwa kiasi cha kulazimika
kuibadilisha muda mfupi baada ya kupitishwa.
Huku akishangiliwa na baadhi ya wajumbe, alisema
wakichagua Serikali tatu watatakiwa kuondoa mambo yote yanayoweza
kukanganya utendaji wa Serikali za washirika na ile ya Muungano. Lakini
wakichagua Serikali mbili, mengi yatatekelezeka.
Rais Kikwete alisema serikali zote mbili zimeamua
kwa dhati kutumia fursa ya mchakato wa mabadiliko ya Katiba kutatua
mambo matatu kati ya sita ambayo bado hayajatatuliwa kutoka kwenye
orodha ya kero 31 za Muungano zilizoainishwa na Zanzibar.