“kati yao watoto 777 husoma wamekaa chini,kutokana na ukosefu wa
madawati.
Machi 10,2014
Serengeti:WALIMU
watano wa shule za msingi Kitarungu na Matanka kata ya Nyansurura wilayani
Serengeti wanalazimika kufundisha
wanafunzi 1005 ,moja yenye watoto 557 ina walimu 2 na nyingine yenye
watoto 448 ina walimu 3.
Mbali na upungufu wa walimu shule hizo zote mbili zina
madawati 76 ambapo wanafunzi 777 kwa shule hizo mbili husoma wamekaa chini hali
ambayo inabainisha changamoto kwa sekta ya Elimu ambayo ni miongoni mwa sekta 5
zilizokwisha zindua mikakati ya Matokeo Makubwa sasa(BRN).
Mratibu elimu kata hiyo Benard Misolo aliliambia Mwananchi
kuwa kwa hali hiyo wastaraji miujiza kwa walimu wawili kufundisha wanafunzi 557
kuanzia darasa la kwanza hadi la saba ,wakati huo Mwalimu mkuu ana majukumu ya
utawala.
“Tatizo hili ni la muda mrefu ,ofisi ina taarifa ….kupitia
uongozi wa kata na elimu toka mwaka 2007 shule ilipoanzishwa bila mafanikio…tukipata
walimu sita watasaidia kupunguza tatizo ,kwa shule ya Matanka walimu watatu
hawakidhi… wanaopata shida hapa ni watoto”alisema.
Kuhusu madawati alisema shule ya Kitarungu wanafunzi wanaosoma
wamekaa kwenye madawati ni 108,huku wanafunzi 449 wanasoma wakiwa wamekaa
chini,na shule ya Matanka wanaokalia madawati ni 120,huku 328 wanasoma wakiwa
wamekaa chini.
“Kuna upungufu mkubwa wa vyumba vya Madarasa ,maana darasa
moja watoto wanakaa kuanzia 50 hadi 120…wengi wakiwa wamekaa chini…hakuna
usikivu hapo..hayo yote ni madhila yanayowakuta walimu wawili,”alisema.
Diwani wa kata ya Nyansurura Jackson Mwita(Chadema)
aliliambia Mwananchi kuwa kata yake inahali mbaya kwa upande wa elimu kwa shule
za msingi,kwa kuwa shule zote saba hazina walimu wa kutosha.
“Tumeomba sana walimu lakini hatupewi…wanadai hakuna nyumba
za walimu…lakini hakuna kata yenye nyumba za walimu za kutosha….mjini shule
moja ina watoto 800 ina walimu 37,hakuna nyumba wamepanga….hapa watoto zaidi ya
500 walimu wawili….uwiano gani huo…harafu mwisho unalaumu watoto na
wazazi….nadhani kuna mitizamo hasi ya kisiasa,”alisema kwa masikitiko.
Mwenyekiti wa kamati ya Elimu,afya na Maji halmashauri hiyo
Daniel Kegocha amekiri kuwepo kwa upungufu huo na kuwa lilikwishatolewa agizo
idara ya elimu kupitia vikao kuwa wapeleke walimu shule zenye upungufu.
“Walimu wapya watakaporipoti mwaka huu shule zenye upungufu
zitapewa kipaumbele…si hizo hata Nyahende kata ya Kebancha bancha ina walimu
watatu wanafunzi zaidi 500…maana shule za mjini wamerundikwa walimu wengi
lazima uwiano uwepo,”alisisitiza.
Hata hivyo imebainika kuwa shule nyingi hazina nyumba za
walimu,na hata vijijini wanakosa nyumba za kupanga hali ambayo inapelekea
walimu kukimbia,ambapo mwaka 2013 walimu 80 walihama mkoa huo,wengi
wakilalamikia mazingira magumu ya kazi.
Uongozi wa idara ya elimu wilaya wamekiri kuwepo kwa
upungufu na kudai kuwa tatizo kubwa ni ukosefu wa nyumba ,hata nyumba za walimu
kupanga baadhi ya maeneo ni changamoto na kuomba jamii kujitolea kujenga nyumba
,na kutengeneza madawati ili kuboresha elimu.
Mwisho.