Subscribe:

Ads 468x60px

Lipumba: Haki za binadamu zimepuuzwa katika rasimu



Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba,Profesa Ibrahim Lipumba.
Na Jacqueline Massano
18th March 2014


Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Profesa Ibrahim Lipumba, amesema anashangazwa kuona Rasimu ya Katiba Mpya, kutokuwa na vipengele vya kutosha kuhusu haki za binadamu.

Alisema Tanzania imejijengea tabia ya kutesa binadamu, hata kwa haki zinazolindwa na sheria.

Profesa  Lipumba ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), alitoa kauli hiyo juzi kwenye semina ya wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba iliyoandaliwa na Mtandao wa Kutetea Haki za Binadamu.

Alisema wajumbe wote wanatakiwa kuungana kuhakikisha Katiba ijayo inalinda haki za watetezi wa haki za binadamu.

“Hili ni letu sote maana wengi wetu tumeathiriwa na kasumba ya utawala wetu kuvunja haki za binadamu hata kwa zile zinazolindwa na sheria, hebu tuwezeshe ibara itakayolinda haki za kundi hili la jamii kuwekwa ndani ya Katiba ijayo,” alisema

Alisema Katiba ijayo inatarajiwa kupatikana na maoni ya wananchi ambao watakuwa na jukumu ya kuilinda, na iwapo ikitokea ikavunjwa mhusika atadhibitiwa kwa nguvu za walioiunda.

Profesa Lipumba alitoa mfano wa kanuni za Bunge Maalum la Katiba ambazo zimetungwa na wajumbe wa bunge hilo, kwa mamlaka waliyopewa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2012, sura ya 83.

 “Kwa mfano sisi (Bunge Maalum), tumepoteza muda kutunga kanuni, tukapambana na kuhakikisha tunapata mwenyekiti tuliyeamini anafaa…lakini amekalia kiti kwa siku moja tu…akavunja kanuni zetu tulizojiwekea, ” alisema.
CHANZO: NIPASHE