Subscribe:

Ads 468x60px

Wiki ya maji bila maji inakosa mvuto,hadhi



Na Mhariri
18th March 2014

Tuko  katika maadhimisho ya wiki ya maji. Ni wiki muhimu kwa ajili ya kimiminika muhimu kwa maisha ya mwanadamu na viumbe hai wengine duniani.

Wiki hii huadhimishwa duniani kote. Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Maji inafafanua kuwa mwaka huu, kilele cha maadhimisho ya wiki hii yaliyoanza Machi 16, 2013 na kufikia mwisho Machi 22 kitafanyika kitaifa mkoani Dodoma.

NIPASHE tunaungana na Watanzania wengine kuadhimisha wiki hii. Tunaunga mkono pia jitihada zinazoendelea kufanywa kila uchao katika kupunguza tatizo la ukosefu wa maji nchini. 

Sisi tunatambua kuwa wiki hii imekuwa na historia ndefu nchini kwani huu ni mwaka wa 25 tangu ianze kuadhimishwa. Kama taarifa ya Wizara ya Maji inavyoeleza, Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa uliofanyika mwaka 1992 ulipitisha azimio lililozitaka nchi wanachama kuadhimisha kilele cha wiki hii kila ifikapo Machi 22. Hivyo, ni wiki muhimu kwa ustawi wa binadamu.

Wiki hii inatarajiwa kuwa na manufaa mengi. Inatoa fursa ya kuwapo kwa tathmini kuhusu mafanikio na changamoto zilizopo katika kuboresha utoaji wa huduma ya maji na usafi wa mazingira. Maadhimisho ya wiki hii pia hutoa nafasi kwa wadau wa maji kubadilishana uzoefu kuhusiana na sekta ya maji na mazingira.

Cha kusikitisha, licha ya kuwapo kwa umuhimu mkubwa kuhusiana na wiki hii, NIPASHE tunaona kuwa hamasa iliyopo katika kuiadhimisha bado iko chini sana.

Yapo matangazo yanatolewa kwa njia mbalimbali ili kuongeza uelewa kuhusiana na wiki hii.

Matarajio ni kuona kuwa wananchi wengi wanashiriki maadhimisho haya kwani nao ni wadau muhimu katika kuboresha sekta ya maji nchini. Pamoja na yote hayo, ukweli unabaki palepale kuwa bado maadhimisho ya wiki hii hayajawagusa watu wengi kiasi cha kukaribia walau robo tu ya umaarufu wa bidhaa yenyewe miongoni mwa Watanzania.

Sisi tunatambua kuwa zipo sababu nyingi zinazochangia kutokuwapo kwa hamasa ya kutosha kuhusiana na wiki ya maji. Hata hivyo, kubwa zaidi ni ukweli kuwa upatikanaji wa maji umeendelea kuwa wa kusuasua katika maeneo mengi nchini. Matokeo yake, wapo watu wanaendelea kuichukulia wiki hii kuwa haiko kwa ajili yao.

Hii ni kutokana na ukweli mwingine kuwa maji yameendelea kuwa sehemu ya kero za kudumu katika maeneo mengi nchini. Mijini watu wanahangaika kupata maji. Vijijini hali ni hiyo pia. Kuna kundi kubwa la Watanzania lisilokuwa na uhakika wa kupata maji safi na salama.

Kuwapo kwa mipango, mikakati na ahadi nyingi za kuvutia za kumaliza tatizo la maji kutoka kwa viongozi mbalimbali wa vyama na serikali, bado kumeendelea kuwa na ukosefu mkubwa wa bidhaa hiyo.

Takwimu za Wizara ya Maji zinaonyesha kuwapo kwa mafanikio makubwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji. Hata hivyo, takwimu hizo bado pia zinaonyesha kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanya. Kwa mfano, kufikia Desemba 2013, hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika jiji la Dar es Salaam na maeneo ya miji ya Kibaha na Bagamoyo ndiyo kwanza imefikia asilimia 68.

Aidha, miongoni mwa Watanzania wanaoishi vijijini, ni asilimia 51.09 tu ndiyo wanaopata huduma ya maji. Hali hii siyo ya nzuri hata kidogo.

Na katika baadhi ya maeneo jijini Dar es Salaam, kama Kimara na Tabata, maji yameendelea kuwa bidhaa adimu pia. Wananchi hulazimika kutumia fedha nyingi kwa ajili ya kununua maji ambayo dumu moja la lita 20 huuzwa kwa wastani wa Sh. 500. Kina mama katika maeneo ya vijijini hutembea umbali mrefu kila uchao ili kutafuta maji.

Hii maana yake ni kuwa pamoja na jitihada zinazoendelea kufanywa kupitia miradi mbalimbali inayotengewa mabilioni ya fedha katika kila mwaka wa fedha, bado nguvu zaidi zinahitajika katika kuimarisha sekta hii.

Wizara ya Maji iendelee kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha kuwa miradi ya maji inatekelezwa kwa vitendo, tena kwa kuzingatia kasi na viwango. Kwa kufanya hivyo, ni wazi kuwa ipo siku wiki ya maji itawagusa Watanzania wengi zaidi kuliko inavyoonekana sasa.