Na Mwandishi Wetu, Mwananchi
Posted Jumatatu,Marchi17 2014 saa 10:28 AM
Posted Jumatatu,Marchi17 2014 saa 10:28 AM
Kwa ufupi
Waandishi wa habari wametakiwa
kutumia kalamu zao kuijenga Tanzania na kujiepusha na upotoshaji unaoweza
kuivuruga nchi.
Dodoma. Waandishi wa habari
wametakiwa kutumia kalamu zao kuijenga Tanzania na kujiepusha na upotoshaji
unaoweza kuivuruga nchi.
Wito huo ulitolewa jana na Makamu
Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samia Suluhu Hassan wakati akizungumza na
waandishi wa habari katika semina iliyoitishwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki
za Binadamu (THRDC).
Semina hiyo ya siku moja ililenga
kuwakumbusha waandishi wa habari umuhimu wa kufuatilia na kuibua mambo muhimu
yanayoendelea ndani ya Bunge la Katiba.
“Nawaomba mjikite katika kuandika
habari ambazo zitalenga kuweka mustakabali mzuri wa nchi yetu kuliko kuweka
makombora ambayo hayana msingi wowote,” alisema Samia.
Alisema kalamu za waandishi wa
habari zinaweza kuibua mambo mazito ambayo yakienda kwa mwelekeo mzuri,
yatakuwa yanajenga nchi lakini yakipotoshwa itakuwa hatari zaidi.
Aliwakumbusha waandishi kuwa
Watanzania wengi hivi sasa macho na masikio yao yameelekezwa Dodoma ambako
Bunge linaendelea na mjadala wa Katiba, hivyo kila kinachofanyika
wanakifuatilia kwa umakini mkubwa.
Samia, ambaye pia ni Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), alisema anakerwa na uandishi unaolenga
zaidi mambo ya Muungano na kuacha mengine muhimu ndani ya rasimu.
Suala la waandishi kuripoti shughuli
za Bunge la Katiba liliibua mjadala, hasa baada ya baadhi ya wajumbe kutaka
waandishi wasihudhurie vikao vya kamti za bunge hilo, nia ambayo ilihitimishwa
kwa wajumbe kupitisha kanuni inayozuia waandishi kuhudhuria vikao vya kamati.
Vyombo mbalimbali vya habari
vimepinga kanuni hiyo vikieleza kuwa inafinya uhuru wa habari.