Mwanasheria Mkuu mstaafu wa Serikali
ya Kenya, Seneta Amos Wako akizungumza jana, wakati wa Semina ya Bunge Maalumu
la Katiba. Picha na Salim Shao
Na Habel Chidawali na Editha
Majura, Mwananchi
Posted Ijumaa,Marchi21 2014 saa 9:11 AM
Posted Ijumaa,Marchi21 2014 saa 9:11 AM
Kwa ufupi
- Awataka Wajumbe wa Bunge la Katiba watunge Katiba inayotokana na maoni na matakwa ya wananchi ili kuepusha migogoro.
Dodoma. Mwanasheria Mkuu (AG) mstaafu wa Kenya, Amos Wako amewataka
wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutokupuuza maoni ya wananchi katika kutunga
Katiba ya nchi vinginevyo watazua mgogoro.
Wako, ambaye kwa sasa ni Seneta wa
Busia ya Mashariki nchini Kenya, alitoa ushauri huo jana katika semina kwa
wajumbe wa Bunge la Katiba kuhusu uzoefu wa namna nchi hiyo ilivyopitia
misukosuko ya kuipata Katiba mpya.
Wako ambaye kwa miaka 21 alikuwa
katika wadhifa wa AG, alisema matukio mengi yaliyosababisha Kenya kutokupata
Katiba yao kwa wakati, yalitokana na kutokuwashirikisha wananchi moja kwa moja
katika mchakato.
Katika hotuba yake iliyodumu kwa saa
2: 11, mwanasheria huyo aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Katiba ya Kenya
alionya pia kuwa Katiba inayotengenezwa hapa nchini isiwe ya kunukuu kutoka
katika mataifa mengine kwa sababu mahitaji yanatofautiana kwa kila nchi.
“Katiba isiwe ya mazungumzo kutoka
kwa viongozi pale Dar es Salaam, kwani itakuwa ni mali ya watu wachache na
ambayo lazima itapingwa, hata sisi tulianza hivyo lakini tulishindwa vibaya,”
alionya Wako.
Aliimwagia sifa Rasimu ya Katiba
iliyowasilishwa bungeni Jumanne iliyopita, kwamba kwa mtindo ilivyowasilishwa
inaonekana kuwajali na kuwapa nafasi zaidi wananchi wa hali ya chini.
“Pamoja na hayo, lakini Katiba hii
ikiingiliwa zaidi na kutekwa na wanasiasa au kikundi cha watu wachache kwa
masilahi yao, inaweza kuharibika kama ilivyotokea kwetu Kenya ambako Kanu
walikuwa wakipinga kila kitu wakatufanya tuingie katika mgogoro.”
Alisema kuwa mitazamo ya wanasiasa
huwa ni tatizo na hatari katika kutafuta Katiba mpya na dawa pekee na ya maana
ni kutoa nafasi kwa wananchi waamue wenyewe.
“Mfumo uliowekwa katika mchakato wa
kuunda Katiba mpya nchini kwenu, kwamba Rasimu ya mwisho ya Katiba itoke bungeni
na kupelekwa moja kwa moja kwa wananchi ni mzuri, ni muhimu maoni ya wananchi
ya awali yazingatiwe,” alisisitiza.
Kwa mujibu wa mwanasheria huyo,
Bunge Maalumu limeaminika kufanya kazi hiyo ili kuwasaidia wananchi kufikia
malengo yao.
Uzoefu wa Kenya
Akizungumzia uzoefu wa Kenya katika
kupata Katiba mpya alisema walianza kwa kukabiliana na changamoto kubwa ya
ukabila ambayo kila jamii ilikuwa haiamini kundi jingine katika kutafuta usawa,
jambo alilosema ni tofauti na Tanzania.
SHARE THIS STORY
Related Stories
“Mwaka 1991 nilipoteuliwa kuwa
Mwanasheria Mkuu, niliulizwa ningetaka nini zaidi ambacho nitawafanyia Wakenya,
nikajibu kuwa ningependa kuwa na Katiba mpya yenye kutoa haki na uhuru wa kweli
kwa Wakenya,” alisema.
Alisimulia kisa chake kwamba
kutokana na ahadi hiyo, alikwenda Uswisi ambako alijifungia peke yake chumbani
na kuandika Rasimu ya Katiba ndani ya siku 10, kisha akarejea Kenya na
kuwaambia alichokifanya lakini akakataliwa na wengi akiwamo aliyekuwa Rais wa
Kenya, Daniel Arap Moi.
Alisema mwaka 1995, Rais Moi
alitangaza kuteua kamati ya wataalamu watakaoandaa upatikanaji wa Katiba na
katika mchakato huo walialikwa wataalamu watatu kutoka Ufaransa, Uganda
na Zambia.
“Changamoto tuliyoipata kwa wakati
huo ni kwamba, tuliambiwa kuwa tusiposhirikisha vyama vya kijamii na taasisi
nyingine, wataweza kuipindua Serikali, hapo nataka kuonyesha namna gani makundi
ya kijamii yalivyo ya muhimu zaidi,” aliongeza.
Hofu ya Kanu
Alisema kuwa Kanu bado iliendelea
kuwa na hofu juu ya uchaguzi kutokana na jinsi mambo yalivyoanza kuwa motomoto
baada ya tangazo la kuingia katika mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, lakini
tofauti na matazamio yao, Rais Moi aliibuka na ushindi mkubwa.
Baada ya hatua hiyo, alisema
wanasiasa kutoka katika chama hicho kilichokuwa madarakani walisema hakukuwa na
haja ya kuwa na Katiba mpya, bali wafanye maboresho kidogo kitendo kilichoibua
hisia kali kutoka vyama vya upinzani.
Kingine ni Kanu kukataa kuingiza
uwiano katika uchaguzi wa wabunge kwa madai ya wingi wao katika Bunge, jambo
lililopingwa na wengi na kusababisha kuunda umoja uliojulikana kama Ufungamano.
Mwafaka katika Katiba
Kuhusu mwafaka alisema ulifika
wakati ambao kila Mkenya aliona ipo haja ya kuwa na Katiba bila ya kujali
maeneo wala mazingira anayotoka, ndipo wakakubaliana kukaa pamoja katika eneo
la Boma na wakati huu walishiriki wabunge wote na wajumbe watatu kutoka kila
wilaya na suala la mgawanyo wa majimbo likaibuka.
Rasimu yakataliwa
Pamoja na mambo yote, kosa lilikuwa
jinsi walivyoipitisha kwa AG (yeye mwenyewe) ambapo alitakiwa kurekebisha
katika maeneo 13, kisha akaipeleka bungeni, jambo lililoibua hasira za watu
wakaamua kuipinga kwa makusudi.
“Huo ulikuwa ni mvutano wa
kuonyeshana mabavu kwa wanasiasa na makundi mengine, kikubwa kilikuwa katika
muundo wa majimbo na mgawanyo wa madaraka katika kuzalisha majimbo, ili kuwepo
na seneta na gavana kabla ya wabunge,” alisema.
Anasema kuwa mamlaka zinatakiwa kuanzia
ngazi ya mwanzo hadi katika ngazi ya Taifa likiwemo suala la kuangalia mgawanyo
wa mapato ili kuondoa manung’uniko.
Ushauri Katiba ya Tanzania
“Katiba Mpya ambayo inatakiwa ni ile
ambayo inaihusisha jamii moja kwa moja, tume yenu imefanya kazi nzuri na
mpangilio uliofanywa na Rais kutanguliza maoni ya wananchi na kisha wao kuwa wa
mwisho kuamua ni mpango mzuri ambao hata mimi nimeupenda,” alisema Wako.
Alirudia maneno kuwa lazima maoni na matakwa ya wananchi yaangaliwe kwa umakini
mkubwa kabla ya kuwarudishia ambapo watakwenda kuamua kwa busara bila ya
malumbano.
Maswali ya wabunge
Mbunge wa Kongwa, Job Ndugai
alimuuliza Wako kuhusu namna walivyokubaliana katika kugatua madaraka na njia
bora ya kugawana rasilimali na katika majibu yake, Wako alisema kinachoweza
kuondoa malalamiko hayo ni uamuzi wa wananchi katika Katiba ambayo inakwenda
kutungwa itakayoeleza namna ya kugawana rasilimali za nchi kwa usawa.
Profesa Abdallah Safari aliuliza kwa
nini Wako alitumia lugha ya Kiingereza katika hotuba yake, huku akijua kuwa
Katiba ya Kenya katika ibara ya 8 imetamka wazi kuwa Kiswahili ndiyo lugha ya
taifa hilo.
Wako aliomba radhi kuwa bado
hajakijua Kiswahili vizuri kutokana na mazoea, na akasema alipochaguliwa
alikwenda Zanzibar kujifunza Kiswahili kwa mwezi mmoja huku akiwataka watu
kutumia lugha hiyo inayokuwa kwa kasi barani Afrika.