Subscribe:

Ads 468x60px

Warioba: Matusi, uongo vinaniumiza






Jaji Joseph Warioba 
Na Goodluck Eliona, Mwananchi

Posted  Aprili26  2014  saa 9:0 AM
Kwa ufupi
  • Warioba amesema ingawa haelewi kwa nini wanaomshambulia wameamua kutumia lugha za matusi dhidi yake binafsi, hatajutia kuchaguliwa kuiongoza tume hiyo kwa kuwa ilikusudia kuwaletea maendeleo wananchi wote kwa kuwapatia Katiba wanayoitaka.
Dar es Salaam. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba amesema baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wametumia vibaya Bunge hilo kwa kumshambulia na kumsingizia mambo ya uongo kwa makusudi, akisema matusi yanayotolewa dhidi yake yanamuumiza.
Aidha, Warioba amesema ingawa haelewi kwa nini wanaomshambulia wameamua kutumia lugha za matusi dhidi yake binafsi, hatajutia kuchaguliwa kuiongoza tume hiyo kwa kuwa ilikusudia kuwaletea maendeleo wananchi wote kwa kuwapatia Katiba wanayoitaka.
Kauli hiyo ya Jaji Warioba imekuja wakati baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba na viongozi wa CCM wakiikosoa Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba kwa maneno makali,huku wakimshutumu na kumkejeli yeye na baadhi ya wajumbe wa tume aliyoiongoza.
Akizungumza kwa mifano katika mahojiano na gazeti hili jana, Warioba alisema kuwa anawashashangaa wajumbe hao na viongozi wa CCM kwa kuacha kuijadili Rasimu ya Katiba, badala yake wanamkosoa yeye na kumsingizia maneno yasiyo ya kweli.
“Bulembo (Abdallah Bulembo mjumbe wa Bunge na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM) amenitukana, amenitukana… amesema niliwahi kupokea rushwa huku akijua kabisa kuwa ni uongo. Yeye ni kiongozi wa Kamati Kuu ya CCM, anasema uongo akijua ni uongo. Kwanza mimi simjui wala sijawahi kumwona huyu mtu naambiwa tu anatoka Mara,” alisema Jaji Warioba kwa sauti ya upole iliyoashiria kuumizwa.
Aliongeza kwamba siyo mara ya kwanza kwa Bulembo kumshambulia kwa lugha za matusi, kwani aliwahi kufanya hivyo tena kwenye moja ya mikutano ya CCM mkoani Tanga.
“Alifanya hivyo Tanga, anachokifanya siyo kitu cha mzaha kwa sababu anafahamu kilichotokea,” alisema.
Akizungumzia kauli aliyoitoa Waziri Hawa Ghasia wakati akichangia mjadala wa Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba aliyemtaka Jaji Warioba kufunga mdomo kutokana na kazi yake ya kuwasilisha Rasimu kumalizika, Jaji Warioba alisema: “Wao wanataka waseme uongo, mtu mwingine asiseme kitu.”
Warioba alieleza kuwa tangu lugha za matusi na kejeli zilipoanza kutolewa dhidi yake, baadhi ya watu walimshauri kwenda mahakamani kufungua kesi, lakini alikataa kwa kile alichodai kuliheshimu Bunge.
Alisema Bunge ndiyo lenye mamlaka ya kufuatilia na kudhibiti kauli zinazotolewa bungeni, kama wahusika hawafanyi hivyo hawezi kuchukua hatua yoyote.
“Kama kinga ya Bunge inatumika vibaya unafikiri mimi nitafanya nini? Sina nia ya kuchukua hatua, watu walipendekeza niende mahakamani, kuna wanasheria walisema hata nisipokwenda, wao watakwenda mahakamani nikawazuia,” alisema Warioba ambaye pia ni Waziri Mkuu mstaafu.
Akisimulia kuhusu uchaguzi wa ubunge wa mwaka 1995 ambapo aligombea na kutuhumiwa kupokea rushwa na kufungiwa kwa miaka minne, Warioba alisema taarifa hizo siyo sahihi kwa kuwa aliyepokea rushwa ni aliyekuwa mgombea kwa tiketi ya NCCR Mageuzi (wakati huo), Stephen Wassira ambaye sasa yuko CCM na ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu.
Uchaguzi ule ulikuwa umejaa sana rushwa, tukaenda mahakamani, Wassira akafungiwa asigombee,” alisema.
Akizungumzia maadhimisho ya sherehe za miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Warioba alisema: “Mimi ni muumini wa muungano, kwa miaka 50 taifa limekaa kwa amani, mshikamano na umoja. Ni kweli tumekuwa na matatizo lakini yanaweza kutafutiwa ufumbuz



Warioba atunukiwa nishani iliyotukuka




 


Rais Jakaya Kikwete  akimvisha  Jaji Mstaafu, Joseph Warioba nishani ya kumbukumbu ya miaka 50 ya Muungano daraja la kwanza  wakati wa sherehe ya kutunuku nishani na tuzo hizo iliyofanyika Ikulu jijini  Dar es Salaamu juzi usiku. Picha na Salim Shao 
Na Elias Msuya, Mwananchi

Posted  Jumapili,Aprili27  2014  saa 10:50 AM
Kwa ufupi
Walioanza kupata tuzo na nishani hizo ni waasisi wa Muungano wa Tanzania, Mwalimu Julius


Dar es Salaam. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba juzi usiku alikuwa miongoni mwa viongozi na watu mashuhuri waliotunukiwa nishani na Rais Jakaya Kikwete, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Katika maelezo ya kutoa nishani ya kumbukumbu ya miaka 50 ya Muungano daraja la kwanza, ilielezwa kuwa Jaji Warioba, aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliuenzi na bado anauenzi Muungano huo.
“Katiba kipindi chako, pamoja na nyadhifa nyingine, ulikuwa Waziri Mkuu na Makamu wa kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani…katika kipindi hicho na hadi sasa umeendelea kuwa mwaminifu, umeutunza, umeulinda na umeuenzi Muungano,” ilisema sehemu ya taarifa ya kutoa nishani.
Hivi karibuni, Jaji Warioba amekuwa akishambuliwa na baadhi ya Wajumbe wa Bunge la Maalumu la Katiba, pia baadhi ya wanaCCM kutokana na Rasimu ya Pili ya Katiba Mpya iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba aliyoiongoza, kupendekeza muundo wa Muungano wa Serikali tatu.
Hata hivyo, upande mwingine wajumbe wanaojitambulisha kama Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wamekuwa wakiunga mkono mapendekezo ya rasimu hiyo.
Mbali na Jaji Warioba, wengine waliopewa nishani katika daraja hilo ni Aboud Jumbe Mwinyi aliyekuwa Rais wa Pili wa Zanzibar, Aman Karume, John Malecela, Cleopa Msuya na Dk Salmin Amour Juma.
Wengine ni Omar Ali Juma na Idrissa Abdul Wakil, ambao sasa ni marehemu.
Walioanza kupata tuzo na nishani hizo ni waasisi wa Muungano wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Karume(wote ni marehemu) na walioendeleza ambao ni Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa.
Wengine waliopewa tuzo ni pamoja na viongozi wa majeshi ya ulinzi na usalama akiwemo Mkuu wa Jenshi la Wananchi (JWTZ), Jenerali Davis Mwamunyange na Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu. Wakuu wa JWTZ wastaafu pia walikumbukwa akiwemo, Jenerali Mirisho Sarakikya, Jenerali David Musuguri.
Katika nishani ya kumbukumbu ya miaka 50 ya Muungano daraja la nne lilikuwa na Mama Maria Nyerere na Mama Fatma Karume, Bendi ya Msondo Ngoma pia ilipewa tuzo kwa kuuenzi Muungano.
Naye Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni za IPP, Reginald Mengi alipewa tuzo maalumu akiwa raia wa Tanzania aliyetoa mchango muhimu katika huduma za jamii.
Wasifu
Joseph Warioba aliingia serikalini mwaka 1966, akiwa mwanasheria wa mji wa Dar er Salaam, nafasi aliyoitumikia kwa muda wa miaka miwili, kisha kuhamia kuwa mwanasheria wa Baraza la Jiji mpaka mwaka 1970.
Kuanzia mwaka 1976 mpaka 1983 Warioba alitumikia taifa kwa wadhifa wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Warioba pia aliwahi kuwa Waziri wa Sheria katika awamu ya kwanza iliyokuwa ikiongozwa na Mwalimu Julius Nyerere.
Mwaka 1984 aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, nafasi aliyoitumikia hadi mwaka 1990.
Mwaka 1996 Rais Benjamin Mkapa alimteua kuongoza tume ya kupambana na rushwa.
Mwaka 2007 alioongoza jopo la waangalizi kutoka nchi za Jumuiya ya Madola katika uangalizi wa uchaguzi mkuu wa Nigeria.
Mwaka 2012 Rais wa awamu ya nne alimteua Warioba kuongoza Tume ya Mabadiliko ya Katiba.