Rais Jakaya Kikwete
akimvisha Jaji Mstaafu, Joseph Warioba nishani ya kumbukumbu ya miaka 50
ya Muungano daraja la kwanza wakati wa sherehe ya kutunuku nishani na
tuzo hizo iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaamu juzi usiku. Picha na
Salim Shao
Na Elias Msuya, Mwananchi
Posted Jumapili,Aprili27 2014 saa 10:50 AM
Posted Jumapili,Aprili27 2014 saa 10:50 AM
Kwa ufupi
Walioanza kupata tuzo na nishani
hizo ni waasisi wa Muungano wa Tanzania, Mwalimu Julius
Dar es Salaam. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji
Joseph Warioba juzi usiku alikuwa miongoni mwa viongozi na watu mashuhuri
waliotunukiwa nishani na Rais Jakaya Kikwete, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Katika maelezo ya kutoa nishani ya
kumbukumbu ya miaka 50 ya Muungano daraja la kwanza, ilielezwa kuwa Jaji
Warioba, aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliuenzi
na bado anauenzi Muungano huo.
“Katiba kipindi chako, pamoja na
nyadhifa nyingine, ulikuwa Waziri Mkuu na Makamu wa kwanza wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzani…katika kipindi hicho na hadi sasa umeendelea kuwa
mwaminifu, umeutunza, umeulinda na umeuenzi Muungano,” ilisema sehemu ya
taarifa ya kutoa nishani.
Hivi karibuni, Jaji Warioba amekuwa
akishambuliwa na baadhi ya Wajumbe wa Bunge la Maalumu la Katiba, pia baadhi ya
wanaCCM kutokana na Rasimu ya Pili ya Katiba Mpya iliyoandaliwa na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba aliyoiongoza, kupendekeza muundo wa Muungano wa Serikali
tatu.
Hata hivyo, upande mwingine wajumbe
wanaojitambulisha kama Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wamekuwa wakiunga
mkono mapendekezo ya rasimu hiyo.
Mbali na Jaji Warioba, wengine
waliopewa nishani katika daraja hilo ni Aboud Jumbe Mwinyi aliyekuwa Rais wa
Pili wa Zanzibar, Aman Karume, John Malecela, Cleopa Msuya na Dk Salmin Amour
Juma.
Wengine ni Omar Ali Juma na Idrissa
Abdul Wakil, ambao sasa ni marehemu.
Walioanza kupata tuzo na nishani
hizo ni waasisi wa Muungano wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid
Karume(wote ni marehemu) na walioendeleza ambao ni Ali Hassan Mwinyi na
Benjamin Mkapa.
Wengine waliopewa tuzo ni pamoja na
viongozi wa majeshi ya ulinzi na usalama akiwemo Mkuu wa Jenshi la Wananchi
(JWTZ), Jenerali Davis Mwamunyange na Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest
Mangu. Wakuu wa JWTZ wastaafu pia walikumbukwa akiwemo, Jenerali Mirisho
Sarakikya, Jenerali David Musuguri.
Katika nishani ya kumbukumbu ya
miaka 50 ya Muungano daraja la nne lilikuwa na Mama Maria Nyerere na Mama Fatma
Karume, Bendi ya Msondo Ngoma pia ilipewa tuzo kwa kuuenzi Muungano.
Naye Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni
za IPP, Reginald Mengi alipewa tuzo maalumu akiwa raia wa Tanzania aliyetoa
mchango muhimu katika huduma za jamii.
Wasifu
Joseph Warioba aliingia serikalini
mwaka 1966, akiwa mwanasheria wa mji wa Dar er Salaam, nafasi aliyoitumikia kwa
muda wa miaka miwili, kisha kuhamia kuwa mwanasheria wa Baraza la Jiji mpaka
mwaka 1970.
Kuanzia mwaka 1976 mpaka 1983
Warioba alitumikia taifa kwa wadhifa wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Warioba pia aliwahi kuwa Waziri wa
Sheria katika awamu ya kwanza iliyokuwa ikiongozwa na Mwalimu Julius Nyerere.
Mwaka 1984 aliteuliwa kuwa Waziri
Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, nafasi aliyoitumikia hadi mwaka 1990.
Mwaka 1996 Rais Benjamin Mkapa
alimteua kuongoza tume ya kupambana na rushwa.
Mwaka 2007 alioongoza jopo la
waangalizi kutoka nchi za Jumuiya ya Madola katika uangalizi wa uchaguzi mkuu
wa Nigeria.
Mwaka 2012 Rais wa awamu ya nne alimteua
Warioba kuongoza Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
0 comments:
Post a Comment