Subscribe:

Ads 468x60px

Warioba: Sikuziona nakala hati za Muungano



 Na Gaudensia Mngumi
13th April 2014
Wakati uhalali wa hati za Muungano ukiendelea kulitatiza Bunge la Katiba, Tume ya Marekebisho ya Katiba, imeeleza kuwa haikuona nakala za nyaraka hizo.

Mwenyekiti wa Tume hiyo ambayo sasa imevunjwa, Jaji Joseph Warioba, alieleza kuwa chombo hicho kiliinukuu hati hiyo kutoka kwenye vitabu vya sheria.

Alitoa maelezo hayo alipoulizwa na NIPASHE iwapo katika kutekeleza jukumu lake wajumbe waliziona na kuzipitia nakala halisi za hati za maridhiano ya Muungano.

Pia gazeti hili lilitaka kufahamu kama Tume ilikuwa na mashaka kwenye saini za viongozi waasisi na wengine walioandaa nyaraka hizo kama ilivyotokea bungeni. Jaji Warioba alisema Tume iliinukuu hati hiyo kama Sheria ya Muungano ya mwaka 1964.

Alisisitiza kuwa hiyo ni sheria hivyo hawakuhitaji nakala halisi au kivuli. Aliongeza kuwa hawakuzihitaji kwa ajili ya kuziambatanisha kwani ni moja ya sheria za nchi na kwamba kwa upande wao hati haikuwa jambo kubwa kama inavyoonekana sasa bungeni.

Jaji Warioba alipoulizwa anafikiri ni sababu zipi zinazozifanya nakala halisi za hati hizo kuwa jambo kubwa kwenye mijadala ya bunge maalumu alisema;
“Sifahamu lakini ninajua ipo sheria ya Muungano ya 1964, wanaozihitaji nakala halisi ndiyo wenye maelezo.” Kwa Tanzania hati ya Muungano ambayo awali ilikuwa amri ya rais au ‘Presidential Decrees’ iliridhiwa mwaka 1964.

SHERIA YA MUUNGANO
Kwa mujibu wa hansadi za kikao cha Bunge la Tanganyika kilichofanyika kuanzia Aprili 25 hadi Mei 12, 1964 jijini Dar es Salaam, hati hiyo iliridhiwa.

Hansadi ambayo ni rekodi za taarifa za vikao vya bunge, imeandika kuwa sheria hiyo iliwasilishwa bungeni ikiitwa ‘Muswada wa Kuthibitisha Mkataba wa Muungano kati ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.’

Kwa mujibu wa hansadi hiyo, muswada huo uliwasilishwa chini ya Katibu wa Bunge (wakati huo) Pius Msekwa na Spika, Chifu Adam Sapi Mkwawa, kwa upande wa Tanganyika. Hadi sasa sheria hiyo inajulikana kama Sheria Namba 22 ya mwaka 1964 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Kumbukumbu hizo zimeeleza kuwa sheria hiyo haikutungwa bali iliridhiwa na bunge la Tanganyika la wakati huo. Pia yapo maelezo kuwa Baraza la Mapinduzi la Zanzibar liliridhia hati za Muungano na kuwa na sheria.

UTATA BUNGENI
Wajumbe wa Bunge Maalum, John Mnyika, alitaka bunge liahirishwe mpaka wajumbe watakapopatiwa nakala halisi. Juma Haji Duni, alisema ni muujiza kuwa hati za Muungano wa nchi mbili zilizoungana hazipo kwenye ardhi ya nchi washiriki zikidaiwa zimehifadhiwa Umoja wa Mataifa nchini Marekani.

“Hili linastahili kuingizwa kwenye rekodi za maajabu ya dunia zinazoandikwa kwenye Guinness World book of Records,” aliliambia Bunge Ijumaa wiki hii.

Mjumbe mwingine Hezekiah Wenje, alisema hati za Muungano zililetwa bungeni kama kipande cha karatasi kilichofikishwa kwa wajumbe  bila kufuata utaratibu, kunaongeza wasiwasi zaidi.

Hata hivyo, wajumbe wanaotaka kuona hati hizo na kuzungumzia zaidi nyaraka hizo wanatoka kwenye  kundi la wachache wenye maoni kinzani. Wajumbe walio wengi ambao ni kundi linalowakilisha msimamo wa CCM halionyeshi mashaka kuhusu hati hizo.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI .