Mtandao
wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) umelaani vikali vitendo na matamshi
yaliyolenga kuichafua
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi Mtendaji wa THRDC, Onesmo Olengurumwa, kuchafuliwa au kudhalilishwa kwa Tume hiyo, ni sawa na kumdhalilisha Mtanzania aliyetoa maoni yake kwa chombo halali cha kisheria katika mchakato wa katiba.
“Awali, Tume ilipaswa kuwa sehemu ya Bunge. Ila kwa kuwa hawakufuata matakwa ya watawala, sheria ilibadilishwa na kuweka ukomo wa Tume,” alisema.
Alisema Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, sura ya 83 toleo la mwaka 2014, kifungu cha 31(1) imewekwa bayana kuwa Tume itavunjwa na Rais kwa amri iliyochapishwa kwenye Gazeti la Serikali, lakini cha ajabu utaratibu huu haukuzingatiwa.
“Lakini pia tukitambua haki ya kupata habari na ushiriki wa wananchi katika mambo ya msingi ya kitaifa...tunaalaani vikali kitendo cha Wizara ya Sheria kuchukua uamuzi wa kuifunga tovuti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba,” alisema.
Alisema tovuti hiyo imefungwa wakati wananchi wanaitegemea sana kufanya marejeo na kupata taarifa mbalimbali kuhusu uandaaji wa katiba nchini.
Olengurumwa alisema siyo sahihi kusema kuwa kwa kuwa Tume imevunjwa, basi hata na taarifa muhimu zake nazo zifungiwe.
Alisema viongozi na watawala wameonya wazi wazi ushabiki wa kisiasa, maslahi binafsi, dharau kwa wananchi na chuki dhidi ya Tume ya Warioba kwa kitendo cha kuwanyima wananchi na wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kupata taarifa za mchakato wa katiba, hasa ukusanyaji wa maoni.
Olengurumwa alisema kitendo hicho kinapingana na sera za uwazi, ukweli na uwajibikaji na katiba ya nchi.
Alishauri utata juu ya tovuti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba utatuliwe kwa kuwaeleza wanachi ukweli kwamba imefungwa au ilikohamishiwa na kama ikiwezekana irudishwe ili kuwapa haki ya kupata habari za maandalizi ya rasimu wananchi.