Rais Jakaya Kikwete
Na Mwandishi Wetu Mwananchi
Posted Mei3 2014 saa 9:40 AM
Posted Mei3 2014 saa 9:40 AM
Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete ameunda Tume ya Uchunguzi, kuhusu
vitendo vilivyotokana na Uendeshaji wa Operesheni Tokomeza.
Taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi
Balozi Ombeni Sefue ilisema, Rais ameunda Tume hiyo kwa mujibu wa kifungu cha
tatu cha Sheria ya Uchunguzi Sura ya 32.
Kutokana na hatua yake ya kuunda
Tume hiyo, Rais Kikwete amemteua Jaji na Balozi Mstaafu Hamisi Msumi kuwa
Mwenyekiti wa Tume hiyo.
Vilevile, Rais Kikwete amewateua
Jaji Mstaafu Stephen Ihema na Jaji Mstaafu Vincent Lyimo kuwa Makamishna. Rais
pia amemteua Frederick Manyanda, Wakili wa Serikali katika Ofisi ya Mwanasheria
Mkuu wa Serikali kuwa Katibu wa Tume hiyo.
Hatua ya Rais Kikwete kuunda tume
hiyo inakuja baada ya Operesheni Tokomeza Ujangili kusitishwa na Bunge kutokana
ukiukwaji wa sheria na haki za binadamu wakati wa utekelezaji wake.
Operesheni hiyo iliayoanza Oktoba
2013 na kusitishwa Nobemba 4 mwaka jana, ndiyo iliyowang’oa mawaziri wanne kwa
kushindwa kusimamia vizuri utekelezaji wake.
Mawaziri hao ni Waziri wa Ulinzi na
Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Dk. Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki na
Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David Mathayo.
Taarifa ya Balozi Sefue inasema kuwa
uteuzi huu ulianza jana, na kutaja majukumu ya tume hiyo kuwa ni pamoja na
kuchunguza na kubaini Operesheni Tokomeza ilivyoendeshwa.
Majukumu mengine ni kuchunguza na
kubaini iwapo Sheria, Kanuni, Taratibu na Hadidu za Rejea zilifuatwa na watu
waliotekeleza Operesheni Tokomeza na kuchunguza na kubaini iwapo yupo mtu
yeyote aliyekiuka Sheria, Taratibu na Hadidu za Rejea wakati wa Operesheni
Tokomeza.
Kuchunguza na kubaini kama wapo watu
wowote waliokiuka Sheria yoyote wakati wa utekelezaji wa Operesheni Tokomeza na
kupima kama hatua zilizochukuliwa dhidi yao au mali zao zilikuwa stahiki.
Kupendekeza hatua zozote zinazopaswa
kuchukuliwa dhidi ya mtu yeyote atakayebainika kukiuka Sheria, Taratibu na Hadidu
za Rejea za Operesheni Tokomeza.
Kupendekeza mambo ya kuzingatiwa
wakati wa kuandaa na kutekeleza operesheni nyingine siku zijazo ili kuepuka
kasoro.
0 comments:
Post a Comment