Subscribe:

Ads 468x60px

UCHAGUZI AFRIKA KUSINI NA MALAWI JUKWAA LA KATIBA LATOA TAMKO



JUKWAA LA KATIBA TANZANIA
P. O. Box 78466, Plot No. 201 Block 46 Kijitonyama, Adjacent to Kijitonyama UDSM Hostels Flats,
Dar Es Salaam, TANZANIA; Tel: +255 22 2773795 Fax: +255 22 2773764 Cell: 0783 993088
E-mail: jukwaa.katiba@gmail.com,info@jukwaalakatibatz.com Web site: www.jukwaalakatibatz.com
CHAGUZI ZA AFRIKA KUSINI NA MALAWI NA
MAFUNZO MAKUU YA KIKATIBA KWA TANZANIA
TAMKO KWA UMMA KUPITIA
VYOMBO VYA HABARI
Kama sehemu ya majukumu yake ya kufuatilia masuala ya michakato
ya Katiba na utekelezaji wake nchini Tanzania na katika nchi jirani,
JUKWAA LA KATIBA TANZANIA limekuwa na utaratibu wa kupeleka
waangalizi wa uchaguzi na upigaji kura za maoni katika nchi za
Afrika. Lengo kuu limekuwa ni kutazama na kujifunza namna
ambavyo uchaguzi, kama sehemu muhimu ya utekelezaji wa katiba
za nchi husika umekuwa ukifanyika huku msisitizo ukiwa ni
kuchunguza jinsi vyombo vikuu vinavyoanzishwa kikatiba vinafanya
kazi zake katika uchaguzi. Ni wazi kuwa utendaji bora wa vyombo na
taasisi za Kikatiba ni muhimu sana katika kuufanya uchaguzi ufanyike
kwa uwazi, uhuru na haki au kinyume chake.
2
Tamko hili linafuatia uangalizi wa JUKATA katika uchaguzi
uliofanyika nchini Afrika Kusini tarehe 7/5/2014 na nchini Malawi
tarehe 20/5/2014 ambapo Jukwaa la Katiba Tanzania lilipeleka
waangalizi kadhaa kwa uchaguzi katika nchi zote hizi mbili. Mambo
makuu tuliyoyaona na mafunzo muhimu kwa Tanzania yamo katika
tamko hili kwa Umma.
UCHAMBUZI LINGANISHI WA NCHI YA MALAWI NA AFRIKA YA
KUSINI
1.1 MAZINGIRA AMBAMO UCHAGUZI UNAFANYIKA
Tuanze kwa kukiri kuwa katika nchi hizi mbili mazingira ya kisiasa,
kiuchumi na kijamii ni tofauti sana pamoja na kwamba nchi zote mbili
ni nchi za kiafrika na zote ziko Kusini mwa Afrika. Kwa mfano, wakati
hali ya kiuchumi ya Afrika Kusini ni ahueni kubwa labda kuliko nchi
nyingine yoyote ya Afrika, hali ya Kiuchumi ya Malawi mbaya sana.
Kumekuwa na mdororo wa Kiuchumi katika nchi ya Malawi kwa
miaka mingi sasa lakini hasa kuanzia mwaka 2012. Zipo fununu kuwa
hata kifo cha Rais wa Zamani wa Nchi hiyo, Dkt. Bingu wa Mutharika
ambako kulisababishwa na msongo wa mawazo na shinikizo la damu
kunaweza kuwa kulichangiwa na maandamano ya wananchi hususan
vijana kutokana na matatizo ya ajira na mengineyo kutokana na
mdororo wa uchumi. Ikumbukwe kuwa Rais Mutharika alianguka
akiwa kazini ikulu ya Malawi baada ya mjadala mrefu wa namna ya
kushughulikia matatizo ya Malawi ya ukosefu mafuta na fedha za
kigeni ambayo yalionekana kutokuwa na suluhu yoyote. Uchaguzi wa
3
Malawi umekuja wakati ambapo Malawi iko hoi na kusababisha hata
maandalizi yake kuathiriwa vibaya sana. Ziko gharama za huduma
ambazo Tume ya Uchaguzi Malawi (MEC) iliziombea kwa wafadhili
lakini kwa kuchelewa kupata fedha iliilazimu Tume kuingia mikataba
kwa kutegemea malipo yatafanywa moja kwa moja na mfadhili
husika. Hilo nalo limechangia sana katika kuathiri utendaji wa Tume
ya Uchaguzi wa Malawi kwa kuwa watumishi na watoa huduma
wengi walikuwa na malalamiko mengi ya kucheleweshewa malipo
kiasi cha kuwa na hamasa ndogo sana ukilinganisha na morali
iliyokuwepo kwa watumishi na watoa huduma wa Afrika Kusini.
1.2 UHURU NA KUKUBALIKA KWA TUME ZA UCHAGUZI
Kukubalika kwa Tume ya uchaguzi katika nchi husika ni jambo
muhimu sana. Aidha, upo uhusiano kati ya imani ya wadau wa
uchaguzi na wananchi kwa Tume na kuwepo au kukosekana amani
katika uchaguzi husika. Wakati nchini Afrika Kusini kuna Tume Huru
ya uchaguzi ya Afrika Kusini (IEC) yenye uongozi na watumishi huru
Tume ya uchaguzi ya Malawi (MEC) imeonyesha udhaifu mkubwa
kuhusu namna ya uundwaji wake na kutokana na hilo uhuru wake
unaonekana kutiliwa mashaka ingawa matatizo ya kiuchaguzi
ambayo yametokea Malawi Tume imejitahidi kwa kiasi chake kuhimili
na kutatua matatizo pamoja na mashiniko toka kwa viongozi wa nchi.
Tume Huru ya uchaguzi ya Afrika ya Kusini ilionekana kutoa
maamuzi makini na ya haraka kwa hitilafu za uchaguzi zilizotokea,
kila zilipotokea. Kwa mfano, kwa kuwaondoa maafisa wake hapo
4
hapo bila kupoteza muda kwenye kituo cha kupigia kura cha Nigel –
Eastrand baada ya kuhifadhi vifaa vya kupigia kura nyumbani kwa
kada wa chama, Tume huru ya Uchaguzi ya Afrika Kusini iliweza sio
tu kukomesha vitendo kama hivyo kutfanywa na watumishi wengine
lakini pia Tume iliweza kujijengea heshima na imani kubwa toka kwa
wadau wa uchaguzi na wapiga kura. Hiyo ilikuwa tofauti sana na
Malawi, ambako Tume ya Uchaguzi ambayo ni kipande na huungwa
wakati wa uchaguzi pekee kama ilivyo nchini Tanzania ilishindwa
kushughulikia watumishi wake waliohusika na tuhuma za kutaka
kuiba karatasi za kupigia kura kabla ya siku ya upigaji kura. Katika
sakata hilo, Mkuu wa Wilaya ya Lilongwe na Mkurugenzi wa Jiji la
Lilongwe walijiuzulu nyadhifa zao kama waratibu wa uchaguzi baada
ya kuhusika na tuhuma za kuvuruga uchaguzi lakini badala ya
kuchunguzwa na kuadhibiwa na Tume, Tume iliwaomba kufikiria
kurejea kazini na kuendelea na majukumu yao kama kawaida. Katika
maeneo mengine ambako vifaa vya uchaguzi hafikuwepo bila sababu
za kuridhisha kama Area 24 (Lilongwe) na Blantyre, watumishi
walioshindwa kufikisha vifaa hivyo hawakuchukuliwa hatua zozote
kiasi cha kusababisha maandamano na vurugu za wananchi
wakitaka watendaji hao wachukuliwe hatua, bila mafanikio.
Uhuru wa Tume ya Uchaguzi ya Malawi pia ulikuwa ukitiliwa shaka
kutokana na Mwenyekiti wake, Jaji Maxon Mbendera kuwa Jaji wa
Mahakama kuu ya Malawi ambayo inaonekana kuwa upande wa
serikali zaidi. Katika Nchi ya Afrika Kusini, Mwenyekiti wa Tume Huru
ya Uchaguzi ya nchi hiyo ni Mwanasheria na Wakili huru na wa
5
kujitegemea ambaye hafungamani na chombo chochote cha kiserikali
zaidi ya Tume Huru ya Uchaguzi. Hili limesaidia sana imani kubwa ya
wadau na wananchi kwa Tume Huru ya Uchaguzi ya Afrika Kusini.
1.1. MAZINGIRA YA KIUCHAGUZI
Katika nchi zote mbili Marais walioko madarakani walikuwa
wanagombea tena kwenye chaguzi hizi zilizopita lakini tumeona kuwa
kulikuwa na utulivu zaidi Afrika Kusini kutokana na uhuru na uimara
wa Tume ya uchaguzi kwa kutoegemea upande wowote na vyombo
vingine vya kikatiba kuliko nchini Malawi ambapo Tume ya Uchaguzi
na vyombo vingine vya kikati vilijaribu kuyumbishwa sana na Rais
aliyeko madarakani, Dkt. Joyce Banda, hasa baada ya kutangaza
kufuta uchaguzi wa Malawi 2014. Matumizi mabaya ya ibara za
Katiba yalionekana wazi wakati wa kutangaza kufuta uchaguzi kwa
kutumia ibara ya 88 (2) ambayo inampa Rais Jukumu la kulinda na
kuimarisha umoja na Mshikamano wa Nchi ya Malawi. Ilishangaza
sana wengi kuwa Rais Banda alichukulia kuwa kukaribia kuanguka
kwake na Chama chake katika uchaguzi kulikuwa ni sawa na
kuvurugika kwa umoja na Mshikamano nchini humo. Jambo la
kujifunza hapa ni kwamba ipo haja ya kukemea wanasiasa
wanaojaribu kucheza na ibara na vifungu vya Katiba kwa kuvipa
tafsiri inayowasaidia kwa wakati husika. Mchezo kama wa Malawi
ungeweza kuleta vurugu hadi kupelekea machafuko na umwagaji
damu katika nchi hiyo isingekuwa uimara wa Mahakama katika
kukemea na kubatilisha kauli ya Rais la kufuta uchaguzi.
6
Kuhusiana na haki za makundi mbalimbali katika uchaguzi na
mazingira ya kuwawezesha waweze kufaidi haki yao ya kupiga kura
bila vikwazo, JUKATA tumebaini tofauti kubwa iliyopo kati ya
mazingira ya Afrika Kusini na yale ya Malawi. Wakati mazingira ndani
ya Afrika Kusini yaliandaliwa vizuri sana hadi kuwezesha watu wenye
ulemavu, wazee, vikongwe, wagonjwa, na wajawazito kuweza kupiga
kura kabla ya siku ya watu wote, hali ilikuwa tofauti huko Malawi
ambako hakukuonekana kuwa na utaratibu wa mazingira mazuri kwa
makundi maalum. Aidha, miundombinu katika vituo vya kupigia kura
ndani ya Afrika kusini iliruhusu watu wenye ulemavu kuweza kuvifikia
vituo na kupiga kura bila matatizo. Pia JUKATA tulishuhudia
watumishi na maafisa wa Independepent Electoral Commission (IEC)
wakitoa msaada na kuwapa kipaumbele watu wenye mahitaji maalum
ikiwemo wazee na wenye ulemavu hata siku ya uchaguzi kwa nchi
nzima. Tofauti na huko, vituo vya kupigia kura katika maeneo yaliyo
mengi nchini Malawi vilikuwa katika maeneo ya wazi na ambayo
hayajafunikwa kiasi kwamba watu kadhaa wenye ulemavu wa ngozi
walionwa wakiwa wamejifunika vichwa kwa shida ya kuumizwa na
jua. JUKATA tulibaini kuwa watendaji wengi wa Tume ya Uchaguzi
ya Malawi nao walikuwa wakilalamikia kuunguzwa na jua huku
wakiombea mvua isinyeshe kwa kuwa ingeathiri vibaya zoezi la
uchaguzi. Katika vituo viwili vya Lilongwe manispaa na area one,
JUKATA tulishuhudia ngazi ambazo si rafiki kwa mwenye ulemavu
zikiwa katikati ya sehemu ya kuchukuwa karatasi za kura na sehemu
ya kupigia kura. JUKATA tungependa kushauri Tume ya Taifa ya
7
uchaguzi hapa Tanzania kuanza maandalizi mapema ya sehemu
zitakazofanywa vituo vya kupigia kura ili kepuka mapungufu
yaliyojitokeza Malawi.
1.2. KASHFA KWA WAGOMBEA
Katika nchi zote mbili kulikuwa na kashfa kwa wagombea Urais
ambao walikuwa marais walioko madarakaniHuku Rais Jacob Zuma
alikabiliwa na kashfa ya Nkandla ya matumizi mabaya ya pesa za
umma kuboresha makazi binafsi, Rais Joyce Banda alikabiliwa na
kashfa ya Cashgate inayohusu uchotaji wa mabilioni ya pesa za
Malawi zinazofikia zaidi ya dola milioni 60 wakati akiwa Makamu wa
Rais wakati wa serikali ya DPP iliyoongozwa na marehemu Rais
Bingu wa Mutharika aliyefariki mwaka 2012. Rais Banda
ametuhumiwa kuendelea na uchotaji wa mabilioni hata baada ya
kushika nafasi ya urais ambayo ameshikilia kwa miaka takribani
miwili. Rais Jacob Zuma aliathiriwa kidogo sana kwa sababu katika
mfumo wa uchaguzi wa Afrika Kusini Chama ndicho kinagombea na
kupigiwa kura na sio mtu binafsi wakati Rais Joyce Banda wa Malawi
aliathirika vibaya sana hata kuelekea kupoteza nafasi ya Urais.
Haijajulikana bado kama Rais Banda ataweka kutoka nafasi ya tatu
alipo hivi sasa kwa kura theluthi moja zilizokwishahesabiwa hadi
kuibuka mshindi wa kinyang’anyiro cha Urais.
1.3. MATUMIZI YA VIFAA VYA KAMPENI SIKU YA
UCHAGUZI
8
Waangalizi wa JUKWAA LA KATIBA TANZANIA walishuhudia baadhi
ya wapiga kura wakiwa wamevaa mavazi ya kampeni siku ya
uchaguzi na hasa maeneo ya Pretoria na Johanesburg ambako
katika itongoji kama vya Yeoville, Alexandra, Soweto, Hillbrow na
Diepsloot watu kadhaa waliovalia fulana za ANC, kofia za EFF na
vikoti vya DA walionekana kwenye misitari wakielekea kwenye
vyumba vya kupigia kura wakiwa hawana wasiwasi wowote. Hata
wasimamizi wa uchaguzi na vyombo vya usalama vilionekana
kutojishughulisha kabisa na uvaaji wa mavazi yenye nembo na picha
za vyama vya Siasa hata pale mavazi hayo yalipokuwa yakigawiwa
kwa watu wengine katika vituo vya kupigia kura. Watu wengine
walikuwa wakipeperusha bendera za vyama vyao kwenye baiskeli
walizokuwa wanaendesha. Tulishuhudia na ikatolewa kwenye
vyombo vya habari pia kwamba mahali penginepo ndani ya Afrika
Kusini, vyama vikubwa vilikuwa vinagawa vifaa hivi karibu na vituo
vya kupigia kura siku ya upigaji kura bila kukemewa na yeyote.
Jambo hili linahitaji kuchunguzwa na kuona kama limeleta madhara
yoyote kwa uchaguzi wa Nchi hiyo. Itakumbukwa kuwa mavazi
yanayoashiria Kampeni ni maraufuku siku ya upigaji kura katika nchi
nyingi za Afrika ikiwemo Tanzania. Katika Malawi, jambo hili
liliheshimiwa sana na hakuna hata vazi moja lilionekana katika vituo
vya kupigia kura ambavyo vilitazamwa na waangalizi wa JUKWAA LA
KATIBA TANZANIA.
1.4. HAMASA YA WAPIGA KURA
9
Hamasa ya wapiga kura nchini Afrika Kusini ilikuwa kubwa sana
kama ilivyokuwa pia Malawi. Kabla ya siku ya kupiga kura baadhi ya
maeneo kama Mpumalanga wananchi waliohojiwa walisema
hawatatoka kwenda kupiga kura kwa sababu serikali inawatembelea
kipindi cha kupiga kura tu nabaada ya hapo serikali inapotea. Wapiga
kura walionekana wakilalamikia ukosefu wa huduma muhimu kama
maji na umeme na pengo linalozidi kuongezeka kati ya masikini na
matajiri wan chi hiyo. Machafuko pia yalionekana sehemu za
Alexandra na baadhi ya maeneo huko Kwa Zulu Batal (KZN). Hata
hivyo, ilipofika siku ya kupiga kura, wananchi wa marika na rangi
mbalimbali (wazungu, wahindi, wenye asili ya mchanganyikohalfcaste
na waafrika) walionekana kwenye mistari ya kupigia kura
kwa wingi wa kutosha. Takwimu za mwisho za mwitikio wa wapiga
kura katika uchaguzi wa Afrika Kusini imeonesha kuwa asilimia 73%
ya wananchi milioni zadi ya 25 waliojiandikisha Afrika Kusini
waliweza kupiga kura. Hamasa ya wapiga kura pia ilikuwa kubwa
sana nchini Malawi kuashiria kuwa wananchi walitaka kufanya
mabadiliko katika uongozi wa nchi. Vijana wa Malawi walionekana
kuwa ndio wenye hamasa zaidi ya kutaka kupiga kura, wengi wakiwa
wanapiga kura kwa mara ya kwanza. Ingawa takwimu halisi za
mwitikio wa wapiga kura (turn out) katika uchaguzi wa Malawi
hazijatoka, inakadiriwa kuwa zaidi ya ailimia 80 ya Wamalawi milioni
7.5 walijitokeza kupiga kura katika uchaguzi wa tarehe 20 Mei 2014.
Huu ni mwitikio mkubwa sana ikilinganishwa na Tanzania ambako
katika uchaguzi wa mwaka 2010 ni asilimia 42 tu ya watanzania
milioni 20 walio katika daftari la kudumu la wapiga kura waliweza
10
kupiga kura. JUKWAA LA KATIBA TANZANIA tumebaini kubwa
mwitikio mkubwa wa wapiga kura Afrika Kusini na Malawi
kumechangiwa na elimu kubwa nay a mapema ya uraia na
uhamasishaji wa wapiga kura iliyofanywa katika nchi hizo.
Ilitushangaza na kutufurahisha kuwa kazi ya uhamasishaji wa wapiga
kura kujiandikisha ilifanywa hata na vyama vya siasa ndani ya Afrika
Kusini kitu ambacho si utamaduni wa vyama vya Siasa nchini
Tanzania.
2.0. MAFUNZO KWA TANZANIA
2.1. UIMARA WA TAASISI ZINAZOSIMAMIA UCHAGUZI NA
ULINZI NA USALAMA WA TAIFA
Kutokana na hali iliyojitokeza nchini Malawi ambapo Rais aliyeko
madarakani alikuwa anagombea na hamasa ya wananchi ilikuwa juu
kuashiria kutaka mabadiliko ya uongozi, Rais aliyeko madarakani alipoona
dalili za kushindwa akaanza kutoa amri ovyo kwa taasisi na vyombo
mbalimbali muhimu vya usimamizi wa uchaguzi na ulinzi wananchi.Somo
hapa kwa Tanzania ni kuwa lazima vyombo hivi visukwe katika namna
ambayo havitapendelea mtu yeyote na kusikiliza amri wakati wa uchaguzi.
Vyombo hivi ni pamoja na Tume ya Taifa ya uchaguzi (NEC), Jeshi la
Polisi, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Vyombo vya habari vya
umma yaani Televisheni na Redio ya Taifa (TBC) na Idara ya Usalama wa
Taifa. Hii itasaidia kulinda usalama wa Raia, mali zao na Taifa kwa ujumla
kuliko kulinda chama na kikundi cha watu au hata kuishia kumlinda mtu
mmoja anayegombea Urais. Aidha, nafasi ya mahakama katika sio tu
11
kusikiliza na kutolea uamuzi mashauri yahusuyo uchaguzi kwa haraka
lakini pia kutoa tafsiri juu ya maamuzi ya vyombo na wanasiasa
imejidhihirisha wazi ndani ya Afrika Kusini lakini hasa Malawi. Nafasi ya
vyombo vingine kama Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
nayo imeonekana kuathiri uchaguzi katika nchi mbili tulizoangalia uchaguzi
wake mwezi Mei, 2014. JUKATA tunapendekeza kuwa mahakama zetu
lazima zifanye jitihada ya kuwa huru na kujiweka katika nafasi ya kuepuka
upendeleo kuelekea, wakati na baada ya uchaguzi.
2.2. ELIMU YA URAIA NA ELIMU YA MPIGA KURA NI MUHIMU
Elimu ya uraia ni muhimu sana ifanywe Tanzania muda wote na serikali
itoe ruzuku kwa vyombo vya habari hata vya binafsi ili kusambaza elimu hii
muhimu kwa upana zaidi na kufika kila pembe ya nchi ili kuwa na wapiga
kura na wananchi wenye uelewa wa kutosha kwa ajili ya kulinda maslahi
na usalama wa Taifa ili kuepusha fujo na vurugu katika nchi. Ni wito wetu
kwa wadau wa uchaguzi nchini kuwa Elimu ya Uraia na elimu ya Mpiga
kura lazima ianze angalau mwaka mmoja kabla ya uchaguzi na sio
kufanyika ndani ya miezi sita (6) kabla ya siku ya kupiga kura.
2.3 UANDIKISHAJI NA UHAKIKI WA MARA KWA MARA WA WAPIGA
KURA KATIKA DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA
JUKWAA LA KATIBA TANZANIA linapenda kukumbusha tume ya uchaguzi
kuanza kurekebisha daftari la wapiga kura. Sheria ya Uchaguzi Na. 1 ya
mwaka 1985 (kama ilivyorekebishwa) inatutaka kuhakiki daftari la wapiga
kura angalau mara mbili ndani ya miaka mitano. Jambo hili halijawahi
kutekelezwa na huo ni uvunjaji wa sheria. Kama tulivyokumbushia mwaka
12
jana kwamba Zanzibar wamesha rekebisha daftari lao, tunapenda
kuchukua fursa hii kuuliza -je daftari la Jamhuri ya Muungano wa
Tananialinasubiri nini? Hii ndio inapelekea urekebishaji wa haraka haraka
na wananchi wengine wanakosa haki zao za msingi za kupiga kura kwa
kushindwa kuingia kwenye daftari la kudumu la wapiga kura. Tatizo liko
wapi?
Mwisho, tunapenda kushauri pia kuwa siku ya kupiga kura Tanzania
ifanywe kuwa siku ya katikati ya wiki na itangazwe kuwa siku ya
mapumziko ili kuruhusu watu wa Kada mbalimbali kupata fursa ya kupiga
kura. Aidha, inapendekezwa kuwa Mchakato unaendelea wa Katiba
uachwe ukamilike ipasavyo ili usuke vema vyombo vikuu vya uwajibikaji
vya kikatiba. Katiba ya Afrika Kusini inaweza kutoa mfano mwema kwa
Tanzania kupitia sura ya tisa (9) ambayo imeweka taasisi imara za Kikatiba
ambazo haziko tayari kutetereka hata wakati wa uchaguzi. Taarifa kamili ya
uangalizi wa JUKWAA LA KATIBA TANZANIA kwa uchaguzi wa Afrika
Kusini na Malawi itakabidhiwa kwa baadhi ya wadau wa uchaguzi nchini
kwa kuanza na Tume ya Taifa ya Uchaguzi hapa Tanzania na Tume ya
Uchaguzi Zanzibar.
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika!
Ahsanteni sana kwa usikivu.
Deus M.Kibamba
Mwenyekiti

0 comments:

Post a Comment