Posted Ijumaa,Mei16 2014 saa 7:57 AM
Kwa
ufupi
“Alichokizungumza
Mnyaa ni sahihi lakini hapa si mahali pake, namshauri kuwa akaulize huko
Zanzibar kwenye vikao vyao hapa sisi hatuna majibu,” alisema Werema.
Dodoma. Kwa maneno ya siku hizi ni kwamba Mwanasheria Mkuu wa
Serikali (AG), Jaji Fredrick Werema ‘amelikoroga na kulinywa mwenyewe’, baada
ya jana kutoa kauli ya kuudhi alipomtaka mbunge kutoka Zanzibar akaulize swali
lake visiwani humo, iliyosababisha baadhi ya wabunge kususia Bunge na kutoka.
Kauli
iliyoonyesha kuwagawa wabunge katika mafungu mawili; wa bara na Zanzibar,
ilimlazimu Jaji Werema baadaye kusimama bungeni na kuwaangukia akiwaomba radhi
waliokerwa na kauli yake na pia kuliomba radhi Bunge, Spika wake, Anne Makinda
na wananchi.
Kuondoka
kwa wabunge hao kulitokana na mwongozo wa Spika ulioombwa na Mbunge wa Ole
(CUF), Rajabu Mbarouk Mohamed kutokana na majibu Jaji Werema kwa mbunge wa
Mkanyageni (CUF), Habibu Mnyaa aliyekuwa ameomba ufafanuzi wakati Bunge
lilipokaa kama kamati ya kupitisha vifungu vya Makadirio ya Mapato na Matumizi
ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka 2014/15.
Mnyaa
alisema Wizara ya Katiba na Sheria ni muhimu lakini imekuwa ndiyo ya kwanza
kuvunja sheria na haki za binadamu na akataka ufafanuzi.
Hata
hivyo, aliposimama kujibu swali hilo, Jaji Werema alimwambia Mnyaa kuwa mambo
mengine akaulize Zanzibar na siyo katika Bunge la Jamhuri kwa kuwa si kila kitu
kitaulizwa ndani ya Bunge hilo.
“Alichokizungumza
Mnyaa ni sahihi lakini hapa si mahali pake, namshauri kuwa akaulize huko
Zanzibar kwenye vikao vyao hapa sisi hatuna majibu,” alisema Werema.
Mara
baada ya Bunge kurejea, Mbarouk aliomba mwongozo wa Spika akitaka ufafanuzi wa
kauli hiyo kwamba ilikuwa ya kibaguzi.
“Mheshimiwa
Spika, huu ni ubaguzi na haupaswi kufanywa na mtu msomi kama Mwanasheria Mkuu
wa Serikali,” alisema Mbarouk.
Alisema
ubaguzi huo umewabagua wabunge ambao wamekula kiapo cha kulitumikia Bunge la
Jamhuri ya Muungano na unaonyesha namna ambavyo Wazanzibari wanabaguliwa.
“Mheshimiwa
Spika, yanapofanyika mambo kama hayo na wewe mwenyewe uko hapa unaona ni sawa
na kubariki jambo hilo, huu ni ubaguzi unaoufanya wewe kwa kuwa lilifanyika
ukiona bila hata ya kukemea,” alisema Mbarouk.
Hata
hivyo, Spika alipinga na kusema: “Hakuna mwongozo wowote kwa kuwa hata wewe
umevunja sheria kwani hata nilipokuambia kaa chini umeendelea kuzungumza,
tunaendelea.... Katibu (akimtaka Katibu wa Bunge kutoa mwelekeo wa shughuli
iliyokuwa inafuata ambayo ilikuwa Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi).”
Baada
ya kauli ya Spika, wabunge wa Zanzibar walihamasishana na kuamua kutoka nje kwa
wakati mmoja na huku wenzao wa upinzani wakiendelea kutafakari cha kufanya.
Wakati huo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe alikuwa akisoma
hotuba yake.
Muda
mfupi baadaye, wabunge wa Chadema na NCCR Mageuzi nao walitoka na katika viti
vya upinzani, alibaki John Cheyo wa UDP peke yake.
Baada
ya kutoka
Akizungumza
nje ya Viwanja vya Bunge, Mbarouk alisema wametoka kwa sababu Spika na Jaji
Werema wamewadharau. “Hatutarejea ndani ya Bunge hadi hapo watakapotuomba
radhi, wasipotuomba radhi hatutarejea bungeni,” alisema Mbarouk.
Hata
hivyo, wakiwa nje ya Ukumbi wa Bunge, mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid
Mohamed aliwafuata na kuwaeleza kuwa amezungumza na Werema na amekubali kuomba
radhi kwa wabunge na Watanzania.
“Ndugu
zangu nimeongea na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, amekubali kuomba radhi,”
alisema Hamad Rashid jambo ambalo liliungwa mkono na wabunge wa CUF waliokuwa
wamekaa katika makundi katika Viwanja vya Bunge.
Hata
hivyo, wabunge hao baada ya muda wa dakika 15, walikwenda katika kikao cha
dharura kwenye Ukumbi wa Kambi ya Upinzani ambako pamoja na mambo mengine,
walijadiliana kusudio la kumuona Spika Makinda kumweleza mambo yasiyowaridhisha.
Werema
aomba radhi
Muda
mfupi kabla ya Bunge kuahirishwa, Jaji Werema alisimama na kusema: “Kwa imani
yangu, ninaamini kila binadamu ana nyongo, isipokuwa watu wawili... Yesu Kristo
na Mtume Muhammad (SAW), ndiyo pekee ambao hawakuwa na nyongo. Naomba maneno
yangu yafutwe katika kumbukumbu za Bunge hili.
“Mimi
ni Jaji kwa taaluma na kwa nafasi yangu nimekosea kwa kutoa maneno hayo.
Nimetambua kosa langu na naomba radhi... kwanza kwako Mheshimiwa Spika,
Mheshimiwa Rajab Mbarouk, Mheshimiwa Injinia Habib Mnyaa, Bunge hili na
Watanzania kwa jumla.”
KULIKOROGA
“Alichokizungumza
Mnyaa ni sahihi lakini hapa si mahali pake, namshauri kuwa akaulize huko
Zanzibar kwenye vikao vyao hapa sisi hatuna majibu.”
KULINYWA
“Mimi ni Jaji kwa taaluma na kwa
nafasi yangu nimekosea kwa kutoa maneno hayo. Nimetambua kosa langu na naomba
radhi... kwanza kwako Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rajab Mbarouk, Mheshimiwa
Injinia Habib Mnyaa, Bunge hili na Watanzania kwa jumla.”
Maswali 10 tata kuhusu dengue
“Lakini
si lazima wawe wanazaliana zaidi katika maji masafi kwa sababu wana tabia ya
kubadili tabia. Kwa mfano, anopheles wanaoeneza malaria nao walipenda maji
masafi awali, lakini kwa sasa wamebadilika wanazaliana hata kwenye maji
machafu,”.PICHA|MAKTABA
Na Waandishi Wetu, Mwananchi
Posted Ijumaa,Mei16 2014 saa 7:53 AM
Posted Ijumaa,Mei16 2014 saa 7:53 AM
Kwa
ufupi
Dk
Govela alisema suala hilo bado linahitaji utafiti zaidi kwa sababu kati ya aina
tatu za mbu wanaosababisha dengue, hakuna utafiti uliofanyika kujua tabia zao
wote.
Dar
es Salaam.Tangu ugonjwa wa homa ya dengue
uibuke mkoani Dar es Salaam na baadaye maeneo mengine ya nchi, wananchi
wamekuwa wakijiuliza maswali mengi yenye utata ambayo sasa yamepata majibu ya
wataalamu.
1.
Kwa nini mbu wengine wakiwamo wanaoambukiza malaria hawawezi kuambukiza dengue?
Mtafiti
wa tabia za mbu kutoka Taasisi ya Afya ya Ifakara (IHI), Dk Nicholaus Govela
alisema mbu anayeambukiza homa ya dengue, Aedes Egypti, hawezi kubeba vimelea
vya malaria wala yule anayeambukiza malaria hawezi kuambukiza dengue kutokana
na maumbile yao.
Dk
Govela alisema fiziolojia ya mwili wa mbu haiwezi kuruhusu Aedes Egypti kubeba
virusi vya mbu mwingine.
“Ndiyo
maana mbu hawezi kuambukiza Virusi vya Ukimwi,” alisema.
2.
Kwa nini mbu wa dengue huuma mchana?
Dk
Govela alisema suala hilo bado linahitaji utafiti zaidi kwa sababu kati ya aina
tatu za mbu wanaosababisha dengue, hakuna utafiti uliofanyika kujua tabia zao
wote.
Aina
hizo ni Aedes Egypti, Aedes Albokictus na Aedes Africaans.
Alibainisha
kuwa katika tafiti zinazofanyika, IHI iliwahi kubainika kuwa Aedes African
ambaye pia anaambukiza dengue huuma usiku.
Alisema
wengi wanamwelezea mbu huyu kwa kumlinganisha na tabia za mbu wa Japan, China
na America ya Kusini lakini inawezekana huyu aliyepo hapa ni mpya tofauti na wa
nchi za nje.
3.
Je, dawa inayopulizwa inafaa kuwaangamiza?
Dk
Govela alisema inawezekana ndiyo au hapana, lazima hili pia lifanyiwe utafiti
kwa kuwa upo uwezekano wa mbu hawa kujenga usugu wa dawa kwa kuwa wamekuwapo
nchini kwa miaka mingi.
Alipongeza
uamuzi wa Serikali wa kupuliza dawa kwenye mabasi ya mikoani lakini bado
alihoji iwapo imefikiria udhibiti kuanzia katika viwanja vya ndege na iwapo
itawezekana kuzuia watu wanaokwenda mikoani wakiwa tayari wameambukizwa.
4.
Je, kuna watu wanaougua dengue bila kuonyesha dalili?
Mtafiti
huyo alisema wapo wanaougua bila kuonyesha dalili na wanaendelea kuambukiza...
“Hawa mara nyingi hawaendi hospitali lakini wanakuwa na virusi mwilini,”
alisema.
5.
Kuna aina ngapi za virusi vya dengue?
Dk
Govela alisema zipo aina nne za virusi vinavyoambukiza dengue. Alivitaja kuwa
ni den 1, den2, den 3 na den 4. Hadi sasa, wanasayansi hawajaweza kubaini ni
virusi vya aina gani vinasababisha homa hiyo kwa Tanzania.
“Ndiyo
maana tunahitaji kufanya tafiti zaidi,” alisema.
6.
Je, juisi ya majani ya papai ni tiba ya dengue?
Ofisa
wa Taaluma na Udhibiti wa Magonjwa wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk Grace
Saguti alisema haijathibitishwa kisayansi.
Dk
Saguti alisema ili tiba ikubalike, lazima ithibitishwe na hakuna namna mbadala
ya kuiruhusu itumike kabla ya kujua madhara na faida zake. Alisema mpapai
unaongeza vitamini A na hivyo kuimarisha kinga ya mwili, lakini si kutibu
virusi vya dengue ambavyo kwa asili yake havina dawa.
7.Mbu
wa dengue wako Dar es Salaam pekee?
Mtaalamu
wa IHI alisema mbu huyo anaishi katika maeneo ya kitropiki, hivyo huenda yupo
hata katika mikoa mingine. Alisema kwa tabia, aedes africans anafanana na mbu
aina ya culex ambaye anapatikana katika mikoa mingine, hivyo hata huyo anaweza kuwapo
huko pia... “Lazima ufanyike utafiti ili tujue iwapo mbu huyo hawezi kuzaliana
katika mikoa mingine,” alisema.
8.
Kwa nini aedes hupenda maji masafi yaliyotuama?
Dk
Govela alisema ni kutokana na asili ya maumbile yao. Mbu hao huamini maji
masafi yaliyotuama huwapa joto zaidi kwa ajili ya kutaga mayai.
“Lakini
si lazima wawe wanazaliana zaidi katika maji masafi kwa sababu wana tabia ya
kubadili tabia. Kwa mfano, anopheles wanaoeneza malaria nao walipenda maji
masafi awali, lakini kwa sasa wamebadilika wanazaliana hata kwenye maji
machafu,” alisema
9.Kwa
nini wahudumu wa afya wanaathirika zaidi?
Daktari
Kiongozi na Mtaalamu wa Homa ya dengue, Mrisho Lupinda alisema nao ni binadamu
kama wengine na wanaishi maeneo hatarishi yenye mbu kama watu wengine.
10.
Kwa nini panadol pekee ndiyo inatibu dalili za dengue?
Dk
Lupinda alisema dawa nyingine za maumivu yaani Diclopar, Diclofenac na Aspirini
huingiliana na mfumo wa chembe hai nyeupe za damu na huweza kusababisha chembe
hizo kupungua mwilini. Dawa hizo huchochea kutengeneza sumu ambayo huathiri
baadhi ya ogani za mwili.
Ugonjwa
wasambaa
Homa
ya dengue imesambaa katika maeneo mbalimbali nchini na kutoka Shinyanga, Mganga
Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa, Fredrick Mlekwa amesema kumetokea kifo cha mtoto
aliyekuwa na dalili zote za ugonjwa huo.
Huko
Arusha, mkazi wa Maji ya Chai, Frank Nnko (30) amelazwa katika Hospitali ya
Mkoa ya Mount Meru akitokea Hospitali ya Wilaya ya Meru akiwa na dalili za homa
hiyo.
Zanzibar,
wagonjwa watatu wanaodhaniwa kuwa na homa ya dengue wamelazwa katika Hospitali
Kuu ya Mnazi Mmoja. Waziri wa Afya, Juma Duni Haji alisema wagonjwa hao wana
dalili za ugonjwa huo.
Mtu
mmoja amelazwa katika Hospitali ya Tumbi akiwa na dalili za dengue, akiwa na
maumivu ya kichwa na kutoka damu puani, Ofisa Habari wa Hospitali hiyo, Gerald
Chami alisema mgonjwa huyo mwenye umri wa miaka 30, alitokea Mbezi Wilaya ya
Kinondoni.
Imeandikwa
na Florence Majani, Andrew Msechu, Stella Ibengwe na Happy Lazaro, Mwinyi
Sadallah, Talib Ussi na Julieth Ngarabali.
0 comments:
Post a Comment