“Kama suala la walimu halitapatiwa
ufumbuzi sasa, tofauti kwenye ufundishaji itakuwepo kwa vizazi vingi huku
ikitoa tafsiri mbaya dhidi ya jitihada za kuondoa umaskini duniani na kufikiwa
kwa maendeleo endelevu.” Dk Shukuru Kawambwa
Na Goodluck Eliona, Mwananchi
Posted Mei31
Posted Mei31
Kwa ufupi
- Mchanganuo uliofanyika katika nchi 41 zenye kipato cha chini, zaidi ya nusu ya vijana wenye umri kati ya miaka 15 na 24, hawawezi kusoma wala kuandika.
Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiahidi kuboresha elimu nchini kwa
kuhakikisha inaajiri walimu wa kutosha, imebainika kuwa asilimia 25 ya walimu
huwafundisha wanafunzi mambo yasiyo ya msingi.
Ripoti ya Shirika la Umoja wa
Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco), iliyozinduliwa Dar es Salaam
hivi karibuni, imebainisha kuwa wakati wananchi wakilalamika kuwa elimu
inayotolewa haimsaidii mwanafunzi kupata ajira nzuri, wanafunzi hawajifunzi
mambo ya msingi yatakayowasaidia kupambana na changamoto za maisha.
Akizindua ripoti hiyo, Waziri wa
Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa alisema kuwa ripoti hiyo
imeweka wazi ukubwa wa tatizo la ufundishaji, akieleza kwamba jumla ya watoto
milioni 250, duniani wanakosa mafunzo ya msingi ya kusoma, kuandika na
kuhesabu, ingawa wanaingia darasani.
“Tanzania kama sehemu ya dunia,
haijakwepa tatizo hilo. Baadhi ya watoto wetu wamekuwa wakimaliza shule za
misingi bila ya kuwa na ujuzi huo. Hii ni hali ya kushtua, inayohitaji nguvu za
pamoja za wadau wote wa elimu duniani,” alisema Kawambwa.
Alibainisha kwamba ripoti hiyo
imependekeza mpango wa elimu mwaka 2015, uzingatie ubora utakaotokana na
mipango sahihi inayotekelezeka akitaka tatizo la walimu lipatiwe ufumbuzi wa
kudumu kwa lazima ili kuwanusuru wanafunzi.
“Kama suala la walimu halitapatiwa
ufumbuzi sasa, tofauti kwenye ufundishaji itakuwepo kwa vizazi vingi huku
ikitoa tafsiri mbaya dhidi ya jitihada za kuondoa umaskini duniani na kufikiwa
kwa maendeleo endelevu,” alisema Dk Kawambwa.
Aliongeza kuwa kwa namna hali ilivyo
sasa, Serikali inalazimika kuhakikisha inaajiri walimu wenye dhamira ya kweli
ya kufundisha na kutoa elimu bora.
Ripoti ya Unesco inaeleza kuwa licha
ya kuwepo kwa mafanikio ya kuridhisha katika kipindi cha miaka kumi iliyopita,
wananchi masikini ndiyo walioathirika zaidi na tatizo la utoaji elimu mbaya
sababu ikiwa kutokuwepo kwa walimu wenye mafunzo ya kutosha.
Unesco ilisema kuwa kutokana na
matatizo ya walimu, wanafunzi 130 milioni wanaosoma shule za msingi duniani,
hawana uwezo wa kusoma hata sentensi moja, jambo linalowafanya washindwe
kujiunga na sekondari.
“Matatizo ya elimu siyo tu
yanaathiri malengo ya watoto ya baadaye, lakini pia uchumi wa Serikali hizo.
Gharama ya watoto 250 milioni kutosoma elimu ya msingi ni Dola 129 bilioni za
Marekani,(Sh 212.85 bilioni), ambayo ni asilimia kumi ya matumizi ya dunia
katika elimu,” inasema ripoti hiyo.
Ripoti hiyo imelinukuu shirikali
lisilo la Serikali la Uwezo, linaloeleza kuwa asilimia 26 ya wanafunzi wa
darasa la tatu ndiyo wanaoweza kusoma vizuri hadithi ya Kiswahili ya darasa la
pili.
Akizungumza na gazeti hili kuhusu
takwimu hizo, Mratibu wa Uwezo-Taifa, Zaida Mgalla alisema kuwa asilimia 44 ya
wanafunzi wa darasa la tatu walifaulu jaribio la hisabati la darasa la pili,
huku asilimia 11 pekee wakifaulu kusoma hadithi ya Kiingereza.
Zaida alisema walimu wamekata tamaa
ya kufundisha kutokana na Serikali kushindwa kuwatimizia mahitaji ya msingi,
huku pia heshima yao ikishuka mbele ya jamii.
“Walimu hawaheshimiwi, wanapigwa na
wanafunzi, mtoto akipigwa na mwalimu anapiga simu polisi waje kumkamata
mwalimu. Kwa hiyo walimu wamewasusa wanafunzi na wazazi nao wapo bize na kazi,”
alisema Zaida.
Pia alisema wanafunzi hawafundishwi
mambo ya msingi kutokana na walimu kutojua kitu wanachofundisha.
Hata hivyo, Unesco imeimwagia sifa
Tanzania kwa kuongeza idadi ya wanafunzi waliomaliza shule ya msingi kati
ya mwaka 2000 na 2007, lakini ikasema kuwa asilimia 27 ya wanafunzi hao
hawakujifunza mambo ya msingi.
Vijana milioni 175 katika nchi zenye
kipato cha chini na cha wastani ambao ni sawa na robo ya vijana duniani, hawana
uwezo wa kusoma na kuandika. Katika nchi zilizopo chini ya Jangwa la Sahara,
asilimia 40 hawajui kusoma wala kuandika.
“Ripoti inathibitisha kwamba lazima
mtoto asome miaka minne ili aweze kujua kusoma na kuandika vizuri; kati ya wale
waliosoma miaka minne au chini ya hapo, asilimia 77 hawawezi kusoma sentensi,”
inasema ripoti hiyo.
Akisoma hotuba ya makadirio ya
mapato na matumizi ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa mwaka 2014/2015
bungeni, Dodoma, Dk Kawambwa alisema kuwa vyuo vya Serikali na umma
vimefanikisha upatikanaji wa walimu wapya 36,000 waliohitimu na kuajiriwa.
“Kati ya idadi hiyo, walimu wa
masomo ya sayansi na hisabati ni 2,364, ngazi ya cheti 17,928, ngazi ya
stashahada 5,416 na ngazi ya shahada 12, 994. Ofisi ya Waziri Mkuu -
Tamisemi imewaajiri na kuwapanga katika halmashauri mbalimbali nchini, hivyo
kuendelea kupunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la uhaba wa walimu ngazi
mbalimbali,” alisema.
Waziri huyo alisema kuwa baada ya
ajira ya walimu hao kufanyika, kwa sasa, taifa litabaki na upungufu wa walimu
30, 949 wa shule ya msingi na walimu 24, 596 wa sekondari katika masomo ya
sayansi na hisabati.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha
Tanzania (OUT), Emmanuel Mallya alisema kuwa walimu wanashindwa kuwafundisha
wanafunzi mambo ya msingi kutokana na kukosa ubunifu wa kutumia mifano iliyopo
kwenye jamii husika.
Pia alisema baadhi ya walimu
waliingia katika taaluma hiyo baada ya kufeli katika masomo mengine, hivyo
hawana uwezo mkubwa wa kuchambua mambo mapya na muhimu kwa wanafunzi hao.
Mallya alisema walimu hawana vifaa
vya kutosha vya kufundishia, kisha akatoa ushauri kwa mwandishi.
“Wewe tembelea shule za msingi kumi, utashangaa kugundua
kuwa wanatumia vitabu tofauti kujifunza somo moja, wakati zamani wanafunzi wote
tulikuwa tunasoma kitabu cha aina moja,”alisema.
0 comments:
Post a Comment