POLISI NYAMONGO WAJERUHI SITA KWA MABOMU WAKIWA
MAJUMBANI KWAO.
Na Anthony Mayunga-Nyamongo.
Septemba 10,2012.
ASKARI wa mkoa wa Kipolisi Tarime na Rorya wanadaiwa
kujeruhi watu 6 wakazi wa kitongoji cha Nyabikondo kijiji cha Kewanja kwa
kuwapiga mabomu wakiwa majumbani na kazini wakati wanawatanya wavamizi wa kifusi cha mawe mgodini.
Tukio hilo limetokea septemba
9 ,majira ya saa 6 mchana mwaka huu katika kitongoji hicho,limethibitishwa na
uongozi wa kitongoji na kijiji hicho,huku kamanda wa polisi mkoa akikwepa
kulizungumzia kwa madai kuwa hakuwa na taarifa.
Ulipuaji mabomu na kuleta
madhara kumetokea wakati taifa likizizima kuhusiana na mauaji yaliyofanywa na
jeshi hilo kwa aliyekuwa mwakilishi wa Channel Ten mkoani Iringa Daud Mwangosi
septemba 2 katika kijiji cha Nyololo wakati Chadema wanafungua matawi yao.
Waliojeruhiwa wametajwa kuwa
ni Suzana Mwita Gibaye (28)ambaye aliumizwa kichwani na mguu wa kushoto,Ghati
Marwa ambaye ni mjamzito ambaye habari zinadai kuwa amelazwa katika hospitali
ya wilaya ya Tarime.
Wengine ni Esther Chacha(12) Chacha Chacha(10) na Daniel
Chacha(6) na mama yao Marwa Chacha ambao wamepanga kwa Magaiwa Ngewa wanadaiwa walipigwa mabomu na kuumizwa wakiwa nyumbani kwao ambako
anaendesha biashara ya mgahawa.
Majeruhi.
Mmoja wa majeruhi Suzana akiongea na gazeti hili kwa njia ya
simu muda mfupi baada ya kutoka zahanati
ya kampuni ya African Barrick North Mara kutibiwa alikopelekwa na askari polisi
wa kituo cha Nyamomngo kuwa walipigwa wakiwa wanaendelea na kazi kwenye mgahawa
wa Magaiwa.
“Tukiwa tunaendelea na kazi
kwenye eneo la Mrwambe tuliona polisi wanafukuzana na vijana(Intruda)
waliovamia kifusi kilichomwagwa nje na mgodi huku wanapiga mabomu ,lakwanza na
la pili hayakutufikia wakapiga la tatu nikastukia napigwa kichwani na kitu na
mguu wa kushoto damu zikaanza kuvuja nikaanguka huko”alisema.
Na kuwa mbali na yeye mama
huyo na wanae wote wakawa wamejeruhiwa vibaya ,na polisi wakaendelea kupiga
ovyo ovyo hali iliyopelekea kumwaumiza wananchi wengine wakiwa majumbani.
“Lilifika gari la pili la
polisi afisa mmoja wakawachukua watoto na mama yao mimi nilikuwa nimeanguka kwa
chini hawakuniona ,wakawapeleka zahanati ya mgodi ,mimi nilichukuliwa na boda
hadi hospitali ya Sungusungu wakaniambia niwape Pf 3,kurudi polisi wakanipeleka
zahanati ya mgodi”alidai.
Na alifungwa bendeji kichwani
na mguuni na dawa kisha akarudishwa polisi na kusaini maelezo na kuambiwa arudi
nyumbani akizidiwa arudi polisi,maelezo ambayo pia walipewa mama na watoto
wake.
Mwenyekiti wa kitongoji.
Charles Vicent mwenyekiti wa
kitongoji hicho alisema tukio hilo lilitokea wakati wakiwa kwenye kikao cha
usuluhishi kati ya koo ya Nyabasi na Wanyamongo baada ya kutokea kutoelewana
kilichohusisha Kamanda wa polisi wilaya aliyemtaja
kwa jina la Saimoni,wazee na mila na viongozi wa maeneo husika.
“Tukiwa kwenye kikao mpakani
mwa Kewanja na Nyakunguru ndipo pakatokea matukio hayo ambayo yalimlazimu Ocd
kukimbilia eneo la tukio na kuwachukua wale watoto na mama yao na kuwapeleka
mgodini wakafungiwa bendeji kisha wametelekezwa bila msaada wowote na
inasemekana gololi ziliwaumiza kichwani na vifuani ”alisema.
Alidai kuwa askari polisi
waliokuwa juu wakijua chini kuna makazi ya watu
walifyatua mabomu na kuelekeza majumbani na kuwa hili ni tukio la pili
kupiga na kujeruhiwa watu wakiwa majumbani na shuleni.
Hata hivyo mama aliyejeruhiwa
na wanae inasemekana baada ya kutoka zahanati ya mgodi kutibiwa inadaiwa
aliondoka na wanae wala haijulikani alipo ,lakini habari kutoka kwa majilani
zake zinadai kuwa huenda ameenda kwao kijiji cha Magoto kwa ajili ya matibabu
zaidi na kuwa huenda walitishwa na polisi akaogopa.
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji.
Akiongea na gazeti hili kwa
njia ya simu Mwenyekiti wa serikali ya kijiji aliyejitambulisha kwa jina la
Tanzania O’mtima alisema mmoja wa majeruhi ambaye ni mjamzito ambaye alipigwa
akiwa nyumbani kwake inasemekana amepelekwa hospitali ya wilaya ya Tarime kwa
matibabu zaidi.
Maelezo yake yanadhihirishwa
na juhudi za baadhi ya mashuhuda walioongea na gazeti hili ,ambao walikwenda
hospitali ya Sungusungu na hawakumkuta na hata walipofuatilia nyumbani kwake
waliambiwa toka alipochukuliwa siku ya tukio hajarudi nyumbani.
Mgodi.
Mmoja wa maafisa wa mahusiano
wa kampuni ya African Barrick North Mara Shayo Simion alipotakiwa kutoa
ufafanuzi wa watu wanaohudumiwa na zahanati yao,alidai ni kwa ajili ya
watumishi.
“Kama tumekuta mtu ameumia
sisi hutoa msaada wa matibabu lakini kwa ajili ya majeruhi kama hao wanapaswa
kupelekwa hospitali ya serikali,hilo wasiliana na kamanda kwa kuwa
halituhusu”alisema.
RPC.
Kamanda wa mkoa huo wa
kipolisi Justus Kamugisha alipoulizwa kuhusiana na kujeruhi watu kwa mabomu
wakiwa majumbani alidai hakuwa na taarifa ya watu kuumizwa na mabomu ila vurugu
za wananchi na askari.
“Vurugu ni kila siku tena leo
wamepiga sana gari letu kwa mawe,hapajatokea utulivu eneo hilo ,maana watu
wanajitokeza kwa wingi kutufanyia vurugu,hapa lazima maamzi magumu yachukuliwe
ama kuondoa wananchi karibu na mgodi ama kampuni kutoka wachimbe kama zamani
maana mgodi uko kwenye makazi ya watu ni hatari zaidi”alisema kamanda.
Baadhi ya mashuhuda wanadai
kuwa wananchi walilazimika kushambulia magari ya polisi kwa kile walichodai
matumizi ya nguvu ni makubwa ambayo yanasababisha madhara hata kwa wasiohusika.
Juhudi za kujua hali ya Ghati
ambaye ni mjamzito alikolazwa na hali yake zinaendelea baada ya kuwepo na usiri mkubwa
,ikizingatiwa kuwa hata majeruhi walipelekwa na polisi kutibiwa mgodini badala
ya hospitali ya serikali ili kuficha taarifa.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment