Subscribe:

Ads 468x60px

visima vingi vilivyochimbwa kwa ajili ya maji mbadala kwa wakazi wa North Mara havina maji


VISIMA VINGI WALIVYOCHIMBIWA WAKAZI WA NORTH MARA HAVIJAWAHIN KUFANYA KAZI KWA KUKOSA MAJI.
Na Anthony Mayunga-Nyamongo
Septemba 3,2012.

TATIZO la ukosefu wa maji linaendelea kuwatesa wakazi wanaozunguka mgodi wa African Barrick North Mara ulioko Nyamongo wilayani Tarime ,kutokana na visima vingi vilivyochimbwa kama vyanzo mbadala kutokuwa na maji.

Mwaka 2009 kamati za bunge mara baada ya kujiridhisha kuwa maji yam to Tighite hayafai kwa matumizi kutokana na kuathiriwa na maji ya sumu yaliyovuja kutoka mgodi wa Gokona.

Uchunguzi wa blogu hii ulibaini kampuni haijachimba visima maeneo mengi kama ilivyoagizwa badala yake inasambaza maji kwa kutumia magari yake,huduma ambayo wananchi wanadai inawafanya wasichimbe visima ili wawe wanachota kwa wakati wanaotaka si kama wanavyopelekewa kwa muda maalum.

Pia visima vingi vilivyochimbwa na halmashauri havina maji ,ingawa serikali imekuwa ikijinasibu kuwa wameishachimba visima kwa wakazi wanaozunguka mgodi huo.

Uchunguzi ulibaini kuwa katika kisima kilichoko kitongoji cha Nyabikondo kijiji cha Kewanja kata ya Kewanja kilichochimbwa na halmashauri hakina maji ,hata bomba hakuna na eneo lote limegeuka kichaka.

Katika kitongoji cha Kemambo  kisima kilichochimbwa na kampuni ya African Barrick North Mara hakina maji hali ambayo inapelekea wananchi wa vitongoji hivyo kulazimika kupanga misululu kusubiri magari ya kampuni kuwasambazia maji ambayo hawajui yanakotolewa.

Pia kisima kingine katika eneo la Kenyatanka kilichochimbwa na kampuni hiyo hakifanyi kazi kwa kuwa hakina maji,hali ambayo inawapelekea wananchi kwenda kuchota maji kwenye kisima kingine kilichoko sekondari ya Ingwe na shule ya msingi Nyamongo kilichochimbwa na halmashauri ya wilaya.

Visima viwili kwa kijiji kizima ndivyo vina maji ambavyo ni kilichoshuleni na kitongoji cha Mjini kati ambacho kimechimbwa na shirika la Japani (Jaica) wengine kwenye lambo la Kewanja ambalo maji yake hayafai kwa matumizi ya kunywa wala kupikia .

Wanne Mwita mlinzi wa lambo hilo alisema kuwa maji ya lambo hilo ambalo lilikuwepo lakini kampuni imesaidia kulipanua hayafai kwa matumizi ya kunywa,wala kupikia lakini kutokana na tatizo la maji wengine huyatumia kwa kupikia na kuoga.

Hata hivyo alisema liko hatarini kuziba kwa kuwa linazidi kujaa tope kutokana na kuwa limetengezwa vibaya,hali ambayo ililalamikiwa na baadhi ya wananchi kuwa wanalazimika kutumia maji yasiyokuwa safi na salama kutokana na serikali kuwapuuza kwa kutoa taarifa za uongo.

Fanuel Sasi mkazi wa kijiji hicho alisema kuwa visima vilivyochimbwa hapakuwahi kufanywa tafiti kabla ili kujua kama kuna maji nan i salama ama eneo limeathiriwa na sumu kutoka mgodini,hata ufuatiliaji wa halmashauri haupo ndiyo maana eneo la kisima limegeuka kuwa kichaka kabla ya kutumika.

Diwani Kibasuka.
Diwani wa kata ya Kibasuka Yusuph Moya (CCM)alisema eneo lake ndilo liliathiriwa na maji ya sumu kwa kuua na viumbe hai lakini hawajahi kuchimbiwa visima.

“Wegita na Nyarwana hawana maji wanatumia vyanzo vya kienyeji,visima vimechimbwa Nyakunguru kuna vya Jaica na halmashauri ,vitongoji vipo saba vitatu vya Nyamange,Nyakunguru na Nyamuma vina maji lakini Nyakwirambe,Itandura,Nyamichare na Turuturu havina maji,hakuna maelezo tunayopewa”alisema kwa uchungu.

Mhandisi wa maji wilaya.
Vita Mkubwa mhandisi wa maji wilaya ya Tarime katika hali ambayo inaonyesha hajui walichimba visima vingapi na wapi na kama vina maji na havina alisema ,anaomba apewe muda awasiliane na wenzake ili kujua ukweli wake ndipo ataeleza.

“Niko kwenye kikao mkoani ,lakini naomba muda ili nifuatilie hilo tatizo maana nashindwa kukujibu ,vipo tulivyochimba sisi na Jaica,kama huna nafasi ya kukutana kesho tuongee nitakupigia baada ya kuwasiliana na wenzangu,”alijibu.

Mgodi.
Mmoja wa maafisa habari mgodini hapo aliyejitambulisha kwa jina la Robert alipoulizwa alidai kuwa yuko mbali na ofisi na kudai kuwa yupo Shayo na kuahidi kutoa namba yake kwa maelezo zaidi.

Hata hivyo badala ya kutoa namba yake alidai ametoa namba ya mwandishi kwa Shayo ambaye atapiga,alipotakiwa kutoa namba ya shayo aliahidi kutuma,hata hivyo alipotafutwa tena hakutaka kupokea simu ,hadi tunakwenda mitamboni Shayo hakupiga kama walivyoahidi.

Mwisho,inaendelea.

0 comments:

Post a Comment