ILI kukabiliana na changamoto za
kidunia zinazochangia kuporomoka kwa
Imani ,maadili na ukiukwaji wa utawala bora kwa waumini na viongozi kanisa
Katoliki hapa nchini limeanza kujitathimini na kuweka mikakati mipya.
Akitoa semina wakati wa ibada ya
misa kwa waumini wa kanisa katoliki Parokia ya Mugumu katibu wa baraza la
maketikisa jimbo la Musoma Antony Marwa alisema hatua hiyo ya haraka imetokana
na tafiti zilizofanywa na wataalam wa kanisa na kukabidhi baraza la maaskofu Tanzania.
Alisema licha ya waumini
kuongezeka ndani ya kanisa katoliki imani inazidi kushuka kwa kuwa hawajengwi
kwa misingi mizuri na wanayumbishwa na changamoto nyingi za kidunia ikiwemo
suala la madhehebu mengine.
“Kanisa limeruhusu dunia kuingia
ndani na kuporomosha imani za waumini…watu wanaingia kanisani wamevaa nguo
zisizo na staha …waumini hawasemi,viongozi wa kanisa wako kimya…lakini waumini
wakiulizwa wanasema kanisa linaruhusu….wapi kanisa limeruhusu uchafu kama
huo?”alihoji.
Alikwenda mbali zaidi na kudai
kuwa watakao ingia kanisa na vimini,wanaume wamevaa mregezo na heleni wafukuzwe
kabla ya kuingia,na kwa wanaotoa komnio wasiwape kwa kuwa hawana sifa stahiki.
“Suala la ulevi kuna watu
wanasema kanisa linaruhusu…wapi imeandikwa kwenye biblia kuwa wamewaruhusu
kulewa…muwe watu wa kiasi….haya si maadili mema kwa viongozi wa kanisa na
waumini lazima mageuzi yafanyike ili kujenga imani ya waumini”alisema na
kushangiliwa na kanisa zima.
Akizungumzia suala la utawala
bora kanisani alielezea kuwa viongozi wanaochanguliwa na waumini kuongoza
baraza la walei wanatakiwa kuwa wawazi kwa kutoa taarifa za mapato na matumizi
kwa waumini,ikiwemo vyanzo vyao na jinsi fedha wanazochanga zinavyofanya kazi.
“Kila wakati harambee harambee
kanisani hawasemi zinazochangwa
zinafanya nini…kanisa linakwenda bila bajeti,fedha zinakusanywa kila wiki
zinaishia mifukoni benki haziendi…wekeni bajeti za kuhudumia nyumba za mapadri
na watawa na huduma za kiroho zinazobaki zipelekwe benki”alisema.
Katekista huyo alisema kukosekana
kwa mipango kwenye makanisa kumepelekea elimu ya dini haifundishwi kwa kuwa
walimu wa dini hawalipwi,wanaishi maisha magumu huku fedha zikitumiwa vibaya na
imani ikiporomoka makanisani.
“Maktekista hawathaminiwi wakati
ndio wanafundisha waumini wakabatizwa na kupata kipaimara…shukrani wanachangia
mapadri na maaskofu waliofundisha hawapati kitu…wamekata tamaa ndiyo maana
hawafundishi..wanaingiza waumini wengi wakabatizwa lakini wasiokuwa na misingi
ya imani maana hawana mafunzo…wanawafanya walimu wa dini kama kibao cha
matofali kikimaliza kazi hutupwa”alisisitiza.
Alisema maazimio hayo
yanayotokana na semina ya wiki nzima iliyoshirikisha majimbo yote Tanzania
ilifanyikia Kurasini Dar es Salaam yanatakiwa kufanyiwa kazi ili ujumbe wa
Papa mstaafu Benedict wa 16 wa kutangaza
mwaka 2013 na 14 kuwa wa imani uweze kutimia.
Mwisho.