TEMBO WAVAMIA KIJIJI NA KUUA NG’OMBE
Oktoba 7,2013
HOFU imetanda kwa wakazi wa kijiji cha Makundusi kata ya
Natta wilayani Serengeti kufuatia kundi kubwa la tembo kuvamia kijijini na
kusababisha kifo cha ng’ombe na uharibifu wa mazao.
Tukio hilo limethibitishwa na uongozi wa kijiji na ofisi ya
wanyama pori wilaya kuwa limetokea oktoba 3 majira ya saa 8 arasili mwaka huu
katika eneo la Makundusi ambapo inadaiwa tembo hao wamepiga kambi kwa zaidi ya
siku mbili.
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho Juma Porini alisema
kuwa siku ya tukio tembo kati 30-40
waliokuwa wamepiga kambi jilani na kijiji hicho walivamia kundi la ng’ombe na
kuchanga nyika wakati wanachunga.
“Wachungaji wakakimbia ..ng’ombe nao wakaanza kukimbia,lakini
kuna tembo mmoja ambaye amekatika mkia ambaye inadaiwa mwaka jana na mwaka huu
ameua ng’ombe alianza kufukuza ng’ombe na kufanikiwa kumnasa mmoja kwa
mkonga”alisema.
Alisema kuwa baada ya kumnasa alimbamiza kwenye mti kisha
akaanza kumkanyaga na
kumtoboa toboa hadi akafa,kisha akaanza kutafuta wengine
lakini wakawa wamekimbia.
“Mara baada ya mauaji hayo wakaondoka na kukaa jilani na
mpaka wa kijiji..jioni wanarudi kijijini na kuharibu mazao,kwa ujumla wananchi
walikuwa wamejitahidi kulima mahindi lakini kwa hali ilivyo hawataambua
kitu,maana wanyama hawa wameamua kupiga kambi kabisa”alisema.
Alisema walilazimika kutoa taarifa ofisi ya wanyama pori
wilaya ambao walisema hawana gari,na kuomba msaada kwa hifadhi ya
Jamii(WMA)ambao nao hawakufika,hata kampuni ya Singita Grumeti Reserves
hawakufika kwa wakati.
Na kuwa hata walipofika walidai hawana risasi hali inayotia
shaka utendaji wake,kwa kuwa halmashauri ilipewa gari na kampuni ya Singita
Grumeti Reserves kwa ajili ya kukabiliana na tatizo la tembo,pia kila mwaka wanalipwa
sh.mil.200 na kampuni hiyo,ambazo hazijasaidia idara zaidi ya madiwani kulipana
posho za vikao.
Mjumbe wa serikali ya kijiji hicho Peter Magari alisema
wananchi wana hofu kubwa ya kupoteza maisha kwa kuwa mbinu walizokuwa wanatumia
kufukuza tembo sasa hazina maana kwa kuwa tembo wanaonekana wamezizoea.
“Tumekuwa tukitumia tochi kubwa kwa kukusanyana na mwanga
unakuwa mkali huku tunapiga kelele,tembo wanakimbia …lakini kwa sasa badala ya
kukimbia wanatufukuza hii inaonyesha wazi wameishazoea …kama hali ni hivyo
inatishia usalama wetu”alisema.
Alisema tembo huyo mwaka 2012 aliua ng’ombe wawili mali ya
Charles Machera na Mwanzoni mwa mwaka huu ameua ng’ombe mmoja na tukio hilo ni
tatu anafanya madhara hayo.
Kaimu afisa wanyamapori wilaya Cathbert Boma alikiri kupata
taarifa na kuwa hawakuwa na gari na kudai kuwa wameishaweka utaratibu kwa
askari wa idara hiyo walioko Grumeti wanatakiwa kutaarifiwa.
“Tatizo la tembo kuvamia maeneo ya vijiji linazidi kuongezeka
kwa kuwa wanapokuwa wanawindwa ndani hukimbilia nje…kwa hiyo tatizo hili
linasumbua sana maeneo mbalimbali “alisema.
Hivi karibu Tembo alivunja uzio na kumuua Faru aitwaye
Limpopo aliyekuwa amehifadhiwa katika eneo la Kijiji hicho na kampuni ya
Singita Grumeti Reserves.
Mwisho.