MTOTO KELVIN MARWA WA MIAKA MIWILI AMELAZWA KTK HOSPITALI TEULE YA NYERERE WILAYA YA SERENGETI AKIWA NA MAMA YAKE JACKLINE ANAYEMUUGUZA MAJERAHA YA KUCHOMWA MOTO NA JILANI YAO KUTOKANA NA WIVU WA KULALIA GODORO WAKATI YEYE ANALALIA JAMVI
Serengeti:
WIVU wa kukosa godoro
umempelekea mwanamke mmoja wa
mtaa wa uwanja wa mbuzi mjini Mugumu wilayani Serengeti kuchoma godoro la
jilani yake na kumuunguza vibaya mtoto
wakati amelala.
Tukio hilo la aina yake
limethibitishwa na polisi wilayani hapa na kumtaja mtuhumiwa kuwa ni Esther Juma linadaiwa kutokea oktoba 30 majira ya saa 1:00 asubuhi ambapo
mtoto huyo aliyetajwa kwa jina la Kelvin Marwa(2)ameungua sehemu mbalimbali za
mwili na amelazwa hospitali ya wilaya kwa matibabu.
Akisimulia mkasa huo mama mzazi
wa mtoto huyo akiwa hospitalini
Jackiline Godfrey(20)alisema wamekuwa na ugomvi na mtuhumiwa ambaye ni
jilani yake baada ya kuwa amenunua godoro na yeye analalia jamvi,na siku hiyo akaamua kuchoma godoro na kumuunguza
mwanae.
“Nilitoka saa 12:00 alfajiri kuwahi
kibaruani stendi kwenye mgahawa ninakofanya kazi…nikaacha mwanangu
amelala…hurudi mapema kumwandalia chai ama uji…nikiwa kazini majira ya saa 1:00
asubuhi nilifuatwa na mtoto wa
jilani..akasema Kelvin ameungulia ndani---niliishiwa nguvughafla…kwenda
nikakuta majilani wamebomoa mlango na mtoto ameungua vibaya”alisema huku
akifuta machozi.
Alisema mbali na mtoto kuungua
pia nguo na vitu vingine viliungua vyote
kutokana na unyama huo uliofanywa na jilani yake ambaye amekuwa akimwapia
kumkomesha kwa yeye kununua godoro na kumwacha yeye akilalia jamvi.
Baadhi ya mashuhuda walisema
walimwona mtuhumiwa akitoka ndani ya chumba kilichoungua akikimbia ,ghafla
wakaona moshi na sauti ya mtoto ikisikika akilia kwa sauti kali ,katika
kufuatilia wakabaini mtoto anaungua wakabomoa mlango na kumnusuru mtoto huyo.
“Kilichomsadia mtoto baada ya
kuanza kuungua alijivuta hadi kwenye kona na kuacha godoro linaungua….kwa kweli
ni unyama mkubwa sana aliokuwa anaufanya huyo mwanamke….kulalia jamvi
kunampelekea kutaka kumuua huyo mtoto…kwa kweli kama polisi wasingewahi
angeuawa”alisema shuhuda.
Balozi wa nyumba 10 eneo hilo
Janet Samwel alisema baada ya kukamatwa kwa mtuhumiwa alianza kupigwa na kama
si polisi kufika eneo hilo mapema huenda angeuawa kwa kuwa wananchi walikuwa na
hasira kali dhidi ya ukatili huo.
Mratibu wa dawati la jinsia la
polisi wilaya WP 5665 D/S Sijali Nyambuche alisema walilazimika kufika haraka
eneo la tukio baada ya kupata taarifa za tukio ,wakabaini kuwa huenda kukatokea
maafa kwa mtuhumiwa kutokana na mazingira ya tukio na hasira za wananchi.
“Kama tusingewahi ingekuwa mbaya
zaidi…tulimnusuru mtuhumiwa na tunamshikilia ..taratibu zikikamilika
atafikishwa mahakamani wakati wowote”alisema.
Muuguzi wa zamu wodi ya watoto
Mwangwa Samson alisema mtoto huyo ameungua makalio,miguu na sehemu za siri kwa
asilimia 30 na kuwa hawezi kukaa kutokana na majeraha aliyopata,na juhudi za
madaktari na waganga zinaendelea kuhakikisha anapona.
Mwisho.