Oktoba 26,201
KATIKA hali isiyo ya kawaida Mshitakiwa wa mauaji ya dreva
bodaboda Gwitembe Yagera (68)mbele ya Hakimu wa mahakama ya wilaya ya Serengeti
aliibuka na kudai kuwa yeye ndiye aliua lakini kwa kudanganywa na Sangoma kuwa
akipeleka damu ya mtu atakuwa atatajirika.
Mshitakiwa huyo Suguta Turuka(19)mkazi wa kijiji cha Kenokwe
wilayani hapa licha ya kuambiwa hatakiwi kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo
haina mamlaka kisheria kusikiliza kesi za mauaji aliibuka na kudai kuwa
ameyatenda hayo kutokana na kudanganywa na mshitakiwa mwenzake.
“Mheshimiwa hakimu nilifanya mauaji
hayo mwenyewe baada ya kudanganywa na mshitakiwa mwenzangu ambaye ni mganga wa
kienyeji…nilimuua Gwitembe muda mfupi baada ya kutoka kupiga ramli na kuambiwa kama nataka kuwa tajiri nilete damu ya mtu
yeyote…nikaamua kumkodi kisha nikamuua”alisema mshitakiwa na kuifanya mahakama
kubaki katika mshangao mkubwa.
“Mganga alinipa masharti mbalimbali
ikiwemo kuua na pia kupeleka maziwa ya ng’ombe yenye cream na kuchemshwa pamoja
na mafuta ya kasuku .…vikawekwa ndani ya kopo…akasema nisifungue na kuwa
nitakuta fedha nyingi siku ya kufungua….na kuwa nikikamatwa nisimtaje..hata
hivyo sikupata kitu zaidi ya kuua na kukamatwa”alisema.
Mapema Mbele ya hakimu wa mahakama
hiyo Franco Kiswaga mwendesha mashitaka wa polisi Paskael Nkenyenge aliiambia
mahakama hiyo kuwa Suguta na Marsha Severino(43)ambaye ni Sangoma anayeishi
Mugumu mjini wanashitakiwa kwa kosa la mauaji ya dreva boda boda Gwitembe
Yagera(68).
Akisoma maelezo ya shauri la mauaji
namba 27/2013 alisema washitakiwa walitenda kosa hilo oktoba 3 majira ya saa
9:00 arasili mwaka huu mpakani mwa kijiji cha Nyichoka na Kenokwe eneo lenye
vichaka vingi ambapo kuna kuna mto Nyamburu ,ambapo mshitakiwa Turuka alifanya
mauaji hayo ikiwa ni muda mfupi ametoka kupiga ramli kwa Severino.
Na kuwa mshitakiwa wa kwanza Suguta
alimkodi marehemu Gwitembe aliyekuwa anaendesha pikipiki aina ya Toyo yenye
namba za usajili T608 CKJ kwa lengo la kumpeleka nyumbani kwao Kwitete,lakini
baada ya kufika eneo hilo alimtaka asimame wajadiliane,ghafla alichomoa kisu na
kumchoma sehemu ya kifua upande wa kulia na kuanguka huku yeye akikimbia na kuacha
kisu kikining’inia.
Hakimu Kiswaga aliamru washitakiwa
warudishwe mahabusu hadi novemba 7 mwaka huu kesi hiyi itakapotajwa tena.
Mwisho.