WATATU WAUAWA NA WANANCHI KWA
KUWATUHUMU KUHUSIKA NA WIZI-MARA
Oktoba 11,2013
WAKAZI wa Bukima wilaya ya
Butiama mkoani Mara wamewaua watu watatu kwa kuwakata kwa mapanga,kuwapiga mawe sehemu
mbalimbali za mwili baada ya kuwatuhumu kuhusika na jaribio la wizi katika kijiji cha Kwitare kata ta Makojo.
Tukio hilo limetokea oktoba 8
majira ya saa 12:00 alfajiri kijijini hapo limethibitishwa na kamanda wa polisi
mkoa wa Mara,mkuu wa wilaya hiyo na uongozi wa kijiji.
Waliouawa ni Masola Magesa
Magoti(40)mkazi wa Bukima ,Sagaya Mussa Sagaya(30)mkazi wa kijiji cha Bugoji
wilaya ya Butiama, ambaye inadaiwa alikuwa mwizi sugu na alikuwa chini ya
uangalizi wa polisi kutokana na kuhusika katika unyang’anyi wa kutumia silaha,na
Chikaka Chikaka(32)mkazi wa kijiji Tegeruka.
Mkuu wa wilaya hiyo Anjelina
Mabula amesema kutokana na kukithiri kwa matukio ya wizi na mauaji amesema
itapigwa kura ya siri kijijini hapo kubaini watu wanaijihusisha na wizi,mauaji
na wanaowahifadhi ili hatua ziweze kuchukuliwa.
Amesema sambamba na upigaji kura
za siri pia kutakuwa na madaftari ya wakazi wa kila kitongoji ,kujua wageni
wanaoingia,na kuwa kukitokea uhalifu viongozi wa eneo hilo watashughulikiwa.
Hata hivyo baadhi ya wananchi
wamesema kuwa uamzi huo ni matokeo ya kukosa imani na polisi kwa kuwa
watuhumiwa wakifikishwa kituoni huachiwa na matukio yanazidi,hivyo njia pekee
ya kukomesha uhalifu ni kuwaua.
Maelezo hayo yamepingwa na kaimu
mkuu wa polisi wilaya ya Butiama Abubakari Kunga kuwa wananchi wanapotakiwa
kwenda kutoa ushahidi hawaendi na matokeo yake watuhumiwa huachiwa.
Kauli ya wananchi kukoma imani na vyombo vya serikali yamesemwa pia na Dc wa Tarime John Henjewelle kuwa wanapoitwa kuchukua majeruhi polisi husema hawana mafuta,lakini muda huo huo wakiambiwa kuna magendo mafuta hupatikana.
Hali hiyo pia inajitokeza kwa askari wa taasisi za uhifadhi tembo wanapovamia mashamba na makazi ya watu,hudai hawana magari,risasi ama mafuta ,lakini wakiambiwa kuna jangili magari humiminika eneo hilo kwa muda mfupi.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mara
Fernandi Mtui amewataka wananchi kutojichukuliwa sheria mikononi kwa kuwa ni
kosa,badala yake wawapeleke watuhumiwa polisi na watoe ushirikiano
wanapohitaji,hata hivyo hakuna mtu anashikiliwa kutokana na tukio hilo.
Mwisho.