Subscribe:

Ads 468x60px

DAKTARI MMOJA HUTIBU WAGONJWA 25,000



ASKOFU AMOSI MUHAGACHI MWENYE TAI NYEKUNDU NA MGANGA MFAWIDHI WA NYERERE HOSPITALI TEULE YA WILAYA YA SERENGETI WAKATI WA KIKAO CHA MWISHO CHA BODI ,AMBAPO WALIJADILI NAMNA YA KUKABILIANA TATIZO LA UPUNGUFU WA MADAKTARI

Oktoba 25,2013.
Serengeti:Hospitali  Teule ya  wilaya ya  Serengeti inakabiliwa na upungufu wa kada ya udaktari na utabibu kwa asilimia 43.9,hatua ambayo inapelekea daktari mmoja kuhudumia wagonjwa 25,000 badala ya 1,500.
Hospitali hiyo inayomilikiwa na kanisa la Menonite Tanzania na huendeshwa kwa ubia na serikali inahudumia wakazi wa wilaya hiyo 360,000 na kutoka wilaya zingine za mkoa huo.
Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo Dk,Calvin Mwasha aliliambia Mwananchi kuwa wanahitaji madaktari 11 lakini wapo 4,madaktari wasaidizi wanahitajika 7 lakini yupo 1na watabibu wapo 11 badala ya 13.
“Upungufu huo ni mkubwa unawalazimu madaktari waliopo kufanya kazi zaidi ya uwezo wao….kisheria daktari anatakiwa kuhudumia wagonjwa 1,500 lakini anahudumia wagonjwa 25,000 na wanatumia masaa mengi “alisema.
Kwa upande wa uuguzi alisema hospitali hiyo inahitaji afisa muuguzi(General)14 lakini wapo 4,wauguzi wasaidizi (specialist)wanahitajika 9 lakini hakuna hata mmoja,na kada hiyo wana upungufu wa watalaam kwa asilimia 74.7
Aidha alisema kuna upungufu kwenye chumba cha maiti ,huku kitengo cha Kinywa na meno wakiwa na upungufu wa wataalam kwa asilimia 25 ili kukidhi Ikama.
“Kada ya Madawa kuna upungufu wa wataalam wa madawa(Pharmacy)ni asilimia 66.6 hasa eneo la Mteknolojia…maabara kuna upungufu asilimia 11.1,uzoezaji viungo hakuna afisa tiba kwa vitendo …kuna upungufu asilimia 75…kwa kada ya afisa afya kuna upungufu wa asilimia 100”alibainisha Mwasha.
Kwa upande wake katibu wa hospitali hiyo Dk.Musuto Chirangi alisema ili kupunguza upungufu huo wanafuatilia vibali vya ajira wizarani ili waweze kuajiri wataalam wanaohitajika,”pia tunaanza kozi ya uganga ngazi ya diploma katika chuo chetu cha Kisare mwaka 2014.”alisema.
Hata hivyo ilibainika kuwa wataalam wengi wanaacha kazi na kuajiriwa na serikalini kwa madai kuwa,ajira chini ya kanisa haina maslahi mazuri,watumishi hawapati safari ama semina kama ilivyo kwenye halmashauri na serikali kuu.
Mwisho.