Serengeti:
WATU wawili wamelazwa katika
hospitali ya wilaya ya Serengeti baada ya kupigwa risasi na watu wanaodaiwa
kuwa wezi wa mifugo wakati wanafuatilia nyayo.
Mganga mwandamizi katika
hospitali hiyo Dk.Tanu Waryoba amewataja majeruhi hao kuwa ni Chacha
Megera(39)na Marwa Nyakimwi(21) wote wakazi wa kijiji cha Nyahende wilayani
hapa.
Amesema Megera alipigwa risasi
mguu wa kushoto na Nyakimwi kwenye nyonga mguu wa kulia na kutokea paja la mguu
wa kushoto,na kuwa wanaendelea vizuri baada ya kupata matibabu .
Megera akiwa kitanda namba 12
wodi ya wanaume alikolazwa alisema oktoba 28 majira kati ya saa 4-5 usiku mwaka
huu kulitokea wizi wa ng’ombe 9 nyumbani kwao wakati wamelala.
“Mke wa kaka yangu Kibibi Ntare
alipotoka nje kujisaidia alibaini wizi huo…alipiga yowe kwa kushirikiana na
wanakijiji tukaanza kufuatilia nyayo tukiwa tunakimbia…kufika eneo la mto
Nyahende …tukishangaa ghafla nikapigwa risasi mguu wa kushoto”alisema.
Alisema alishindwa kuendelea na
safari hiyo kutokana na maumivu makali na kulazimika kurudishwa nyumbani na
kupelekwa hospitali kwa matibabu.
“Mimi nilipigwa risasi kwenye saa
6 usiku nikiwa miongoni mwa vijana wenzangu tuliokuwa mstari wa mbele…tukiwa
tunakwenda kwa kasi baada ya kuwepo ishara kuwa wezi hawako mbali…ghafla
nilipigwa risasi upande wa kulia wa nyonga na kutokea kushoto…niliishiwa nguvu
na kulala chini”alisema Marwa Nyakimwi.
Nyakimwi aliyelazwa kitanda namba
8 alisema ilibidi akimbizwe hospitali,huku wenzake wakisonga mbele na
kufanikiwa kurudisha ng’ombe wote 9 na kukamata watuhumiwa watatu kati ya sita
waliohusika na tukio hilo.
Hata hivyo polisi walifanikiwa
kuwaokoa watuhumiwa watatu waliokamatwa na mmoja aliyetajwa kwa jina la Mwita
Malitwa(40)amelazwa hospitali ya wilaya chini ya ulinzi wa polisi.
Polisi wanasema wanaendelea na
mahojiano na baadhi ya watuhumiwa na inasemekana watuhumiwa waliofanikiwa
kutoroka walikimbilia maeneo ya Gibaso wilayani Tarime.
Kuhusu bunduki iliyohusika
walisema ni ya kivita kwa kuwa risasi zake zilibainika ni za SMG ambazo
zinatumiwa na bunduki aina ya SRA pia.
Mwisho.