Na Goodluck Eliona, Mwananchi
Posted Ijumaa,Novemba15 2013
Posted Ijumaa,Novemba15 2013
Kwa ufupi
- Ripoti hiyo iliyotolewa na
idara ya nchi hiyo inayohusika na diplomasia (US Department of State,
Diplomacy in Action), pia inaitaja Tanzania kuwa ni kitovu cha njia ya
kusafirisha wanawake, watoto na wanaume ambao hutumikishwa kwenye kazi za
mashambani na biashara ya ngono.
Dar es Salaam. Marekani imetoa ripoti inayozungumzia usafirishaji wa binadamu ya mwaka
2013, huku ikiitaja Tanzania kuwa kinara wa kunyanyasa wasichana, kuwatumikisha
katika ngono na usafirishaji wa binadamu.
Ripoti hiyo iliyotolewa na idara ya nchi hiyo inayohusika na diplomasia
(US Department of State, Diplomacy in Action), pia inaitaja Tanzania kuwa ni
kitovu cha njia ya kusafirisha wanawake, watoto na wanaume ambao hutumikishwa
kwenye kazi za mashambani na biashara ya ngono.
Ripoti hiyo iliyozinduliwa Julai mwaka huu na Waziri
wa Mambo ya Nje wa Marekani, Seneta John Kerry inaweka bayana kwamba biashara
ya usafirishaji wa binadamu hufanywa na baadhi ya ndugu na marafiki ambao hutoa
ahadi kwa wahusika kwamba wanakwenda kuwasomesha au kuwatafutia ajira nzuri
mijini.
“Unyonyaji wa wasichana wadogo na utumikishaji majumbani ndilo tatizo
linaloongoza, ingawa kesi za watoto kusafirishwa kwa ajili ya biashara ya ngono
katika mpaka wa Tanzania na Kenya zinaongezeka. Pia, wasichana wananyonywa
kwenye maeneo ya utalii,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watoto kutoka Burundi na Kenya, watu wazima
kutoka Bangladesh, Nepal, Yemen na India wanatumikishwa kufanya kazi kwenye
sekta za kilimo, madini na majumbani nchini Tanzania.
“Baadhi ya raia kutoka nchi jirani huingia Tanzania kwa hiari yao,
lakini hulazimishwa kufanya kazi majumbani kabla ya kupelekwa kutumikishwa
kwenye biashara ya ngono Afrika Kusini, Ulaya na Mashariki ya Kati,” inaeleza.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angela Kairuki alimtaka mwandishi
kumtumia ripoti hiyo kwa njia ya baruapepe ili aweze kuisoma na kuitolea
maelezo.
Alipotafutwa siku ya pili, alisema kuwa ameipokea na kuikabidhi ofisi ya
Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka (DPP) ili ifanyiwe kazi na baadaye kutoa majibu.
“Ripoti niliipata nikaikabidhi ofisi ya DPP kwa kuwa wao ndio wanaoweza
kuitolea maelezo baada ya kuisoma. Maoni yangu lazima yawe ya kitaalamu siwezi
kusema bila kupata taarifa kutoka kwao,” alisema.
Lawama kwa Serikali
Ripoti hiyo inaitupia lawama Tanzania kwa kutokuwa na sheria thabiti za
kupambana na biashara haramu ya kusafirisha binadamu, huku ikitolea mfano namna
ilivyoshindwa kuwasaidia raia wake waliokuwa wakinyanyaswa nje ya nchi.
“Kamati ya Serikali ya kupambana na usafirishaji binadamu, haijachukua
hatua za kutosha katika kutekeleza mpango mkakati wa kupambana na vitendo
hivyo,” inaeleza na kuongeza:
“Serikali imeshindwa kutenga
fedha kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa usafirishaji wa binadamu kama
ambavyo inaelekezwa kwenye sheria ya kudhibiti biashara hiyo ya 2008.”Taarifa hiyo inaitaka Tanzania kuongeza nguvu katika kutekeleza sheria ya kudhibiti biashara ya kusafirisha binadamu ya 2008 kwa kuwakamata na kuwashtaki wahusika wote, lakini ikaikosoa kwa kusema inatoa adhabu ndogo kwa mtu anayebainika kufanya makosa, ikiwa ni pamoja na kumhukumu kwenda jela miaka 10, kulipa faini au vyote viwili kwa pamoja.
“Sheria hiyo haifanani na nyingine kama za mtu anayepatikana na kosa la kubaka au kufanya kosa jingine la jinai. Mamlaka imesema ina kesi nne inazozichunguza, saba zipo mahakamani toka mwaka jana, zikiwepo mbili mpya,” inasema ripoti.
Pia, Serikali ya Tanzania imelaumiwa kwa kushindwa kuripoti maendeleo ya uchunguzi wa maofisa wake waliotuhumiwa kujihusisha na biashara ya usafirishaji binadamu.
LHRC na TGNP
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema tatizo la usafirishaji wa binadamu pia linachangiwa na wasichana kuwa na tamaa ya maisha mazuri, hivyo kukubali ahadi ambazo hupewa kwamba wanapelekwa kusoma, wasifahamu wanarubuniwa.
“Wengi wanatamani kwenda ‘majuu’ wakidhani watapata elimu, lakini baadaye wanaingizwa kwenye vitendo vinavyowafedhehesha na kuwafanya wakate tamaa kabisa,” alisema.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Usu Mallya alisema katika siku za karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la vitendo vya unyanyasaji dhidi ya wasichana waliochukuliwa vijijini kwenda mijini kufanya kazi.
Alisema pamoja na tatizo hilo kuongezeka hapa nchini, hakuna tafiti za kutosha ambazo zimefanywa na wadau mbalimbali kuonyesha madhara yaliyopatikana hadi sasa.
“Katika siku za usoni kumekuwa na ongezeko kubwa la vitendo vya kunyimwa chakula, kupigwa na kufukuzwa kazi huku wasichana wengine wakitumika kwenye biashara ya ngono,” alisema na kuongeza:
“Ripoti hii isiishie kwenye makabrasha bali ifanyiwe kazi ili jamii yote ijue kuwa hili ni tatizo.”
Ripoti hiyo inabainisha kuwa watu 47,000 pekee ndio walioweza kuokolewa mwaka jana kutoka kwenye mazingira ya utumikishwaji kati ya milioni 27 waliopo katika hali hiyo duniani.
Tanzania imetajwa kuwa ni miongoni mwa nchi 44 ambazo zinajaribu
kupambana na biashara hiyo, lakini hali inazidi kuwa mbaya zaidi.