Subscribe:

Ads 468x60px

Mabadiliko makubwa mitihani ya sekondari


Posted  Ijumaa,Novemba1  2013 

Kwa ufupi
Akifafanua zaidi juu ya alama za Maendeleo ya Mwanafunzi (CA), alisema kuwa Sera ya Elimu ya mwaka 1995 inayotumika mpaka sasa inataka alama hizo ziwe 50 na zile za mtihani wa mwisho ziwe 50.

Dar es Salaam. Zikiwa zimebaki siku tatu kwa wanafunzi wa kidato cha nne kuanza mtihani wa kumaliza ngazi hiyo ya elimu, Serikali imepunguza alama za ufaulu kwa mtihani huo pamoja na ule wa Kidato cha Sita.
Pia imetangaza kuwa, mtihani wa taifa wa kidato cha nne na sita utakuwa na alama 60 za ufaulu, huku alama 40 zilizobaki zitatokana na zile za maendeleo ya mwanafunzi shuleni (CA).
Katika mfumo huo mpya, wizara hiyo pia imefuta daraja la sifuri na badala yake kutakuwa na daraja la tano.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome alitangaza uamuzi huo wa Serikali jana kwa kueleza utekelezaji wa utaratibu huo utaanza kwenye mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne mwaka huu.
“Hatua hii imechukuliwa kutokana na changamoto zilizojitokeza kuanzia mwaka 2011. Tangu wakati huo kumekuwa na mabadiliko mbalimbali ambayo yamekuwa yakifanyika,” alisema Profesa Mchome.
Alisema kuwa, alama zilizokuwa zikitumiwa awali na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) katika kupanga matokeo hayo, kwa kidato cha nne ni A=80-100, B=65-79, C=50-64, D=35-49, F= 0-34 kwa upande wa kidato cha sita A=80-100, B=75-79, C=65-74, D=55-64, E=45-54, S=40-44 na F= 0-39.
Alisema mfumo mpya, umehusisha alama za kidato cha nne na cha sita na kuwa kuanzia sasa A=75-100, B+=60-74, B=50-59, C=40-49, D=30-39, E=20-29 na F=0-19.
“Alama A itakuwa ni ufaulu uliojipambanua, B+ itakuwa ni ufaulu bora sana, B ufaulu mzuri sana, C ufaulu mzuri, D ufaulu hafifu, E ufaulu hafifu sana na F ufaulu usioridhisha kabisa,” alisema Profesa Mchome.
Alisema pia kuwa, wamebadilisha mfumo wa madaraja ambao awali kulikuwa na daraja la kwanza, la pili, la tatu, la nne na sifuri.
“Lile la sifuri tumeliondoa, badala yake kutakuwa na daraja la tano, lengo ni kuweka mlolongo mzuri zaidi,” alisema.
Alisema, alama hizo zitakuwa ni mgando (fixed grade range).
Profesa Mchome alisema kuwa, utaratibu wa sasa wa kupanga matokeo hayo kwa madaraja, utabadilika muda wowote kuanzia sasa na kwamba utakaokuwa ukitumika ni ule wa wastani wa alama katika ufaulu (Grade Point Average ‘GPA’).
Mfumo huu kwa sasa unatumika kwenye ngazi za vyuo. “Huu mfumo wa madaraja unaotumika sasa ni wa mpito tu, mwakani ama hata kabla ya hapo tunaweza kuanza kutumia mfumo wa GPA,” alisema.
Akifafanua zaidi juu ya alama za Maendeleo ya Mwanafunzi (CA), alisema kuwa Sera ya Elimu ya mwaka 1995 inayotumika mpaka sasa inataka alama hizo ziwe 50 na zile za mtihani wa mwisho ziwe 50.
Kwa upande wa Zanzibar, alisema CA ilikuwa alama 40 na mtihani wa mwisho alama 60, ingawa alisema utaratibu huo haukuwahi kutumika kwa Zanzibar wala Bara.
Aliongeza kuwa hali hiyo ilisababishwa na kutokuwa na utaratibu wa kupata alama sahihi alizopata mwanafunzi shuleni kwani walimu wengi wamekuwa wakituma alama za uongo kwa kuwaongezea wanafunzi alama.
Alisema, utaratibu mpya wa kupata CA itakuwa ni mtihani wa kidato cha pili utachangia alama 15 mitihani ya mihula miwili ya kidato cha tatu kila muhula utachangia alama tano, Mtihani wa Kanda wa kidato cha nne alama 10 huku kazi mradi (project) zikitoa alama tano.
“CA zitatumika pia kwa watahiniwa wa kujitegemea, zile CA zao ambazo walimaliza nazo kidato cha nne hazitatupwa, wakitaka kurudia mtihani hizo alama zao zitajumlishwa kwenye mtihani wa mwisho.
Hata hivyo, alisema kuwa, kwa kuwa tayari shule nyingi zimeshawasilisha CA Baraza la Mitihani, alama 40 kwa mwaka huu zitapatikana tu kwa kuangalia alama hizo zilizopelekwa na shule ambazo hupatikana kwa kuangalia mitihani ya mihula kuanzia ule wa kidato cha kwanza. Kwa wale waliofanya mtihani wa QT (Qualifying Test), alama zao hizo za QT zitachukuliwa 40 kuongezwa kwenye mtihani wa kidato cha nne,” alisema Profesa Mchome.
Alisema kuwa, mfumo huo mpya hautabadilika mara kwa mara na kuwa, utamaliza mzunguko mmoja ambao ni wa miaka minne.

Kidato cha nne kuanza mitihani
Katika hatua nyingine Profesa Mchome alisema, Novemba nne wanafunzi wa Kidato cha nne nchi nzima wataanza mitihani yao ya mwisho ambayo wataimaliza Novemba 21.
“Mitihani hiyo imetanguliwa na ile ya vitendo ya masomo ya Food and Nutrition iliyofanyika Oktoba 7, mpaka 24 mwaka 2013,” alisema.
Alisema kuwa, watahiniwa walioandikishwa kufanya mtihani huo ni 427,906 ambao kati yao 367,399 ni watahiniwa wa shule na 60,507 ni watahiniwa wa kujitegemea.
Alisema kuwa, kati ya watahiniwa wa shule 367,399 wavulana ni 198,257 sawa na asilimia 53.96 na wasichana ni 169,142 sawa na asilimia 46.04.
Alisema kuwa, kati ya watahiniwa 60,507 wa kujitegemea walioandikishwa, wanaume ni 30,456 sawa na asilimia 50.33 na wasichana ni 30,051 sawa na asilimia 49.67.
Alisema kuwa, watakaofanya Mtihani wa Maarifa (QT) walioandikishwa ni 18,214, kati yao wavulana ni 7,222 sawa na asilimia 39.65 na wasichana ni 10,992 sawa na asilimia 60.35 .
Wadau
Kwa upande wake, Meneja wa Idara ya Habari na Utetezi, Nyanda Shuli alisema anaipongeza wizara kwa kuamua kutumia CA ingawa alisema ni lazima kuwe na mfumo wa kuhakikisha alama hizo zinaonyesha uwezo halisi wa mwanafunzi.
Kuhusu kushusha kiwango cha ufaulu, alisema kuwa Serikali inapaswa kutoa sababu iliyoifanya kuchukua hatua hiyo.
“Kama wanahofia jinsi matokeo ya mwaka jana yalivyokuwa siyo sahihi, dawa ni kufundisha kwa makini zaidi,” alisema Nyanda.
Dk Joyce Ndalichako
Katika mahojiano, ambayo Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Joyce Ndalichako, aliwahi kufanya na gazeti hili, alisema ni vigumu kutumia alama za Maendeleo ya Mwanafunzi (CA) kwani kwa kiasi kikubwa walimu hudanganya.
“Wafanyakazi wa baraza ni wachache, hatuwezi kwenda kila mahali ili tuhakikishe alama hizo, mwaka 2011 wale wanafunzi walioandika vitu visivyoeleweka kwenye mitihani yao ya mwisho, kwenye CA walikuwa wana mpaka alama 75.
Tulipowauliza walimu wengine walisema hawakuwa na walimu waajiriwa wa Serikali na waliokuwa wanawatumia ni wale waliomaliza kidato cha sita kwa hiyo hawajui kupanga hizo alama, wengine walisema mitihani hiyo haina usimamizi makini,” alisema Dk Ndalichako