MKURUGENZI Mkuu wa Hifadhi za Taifa nchini,
(TANAPA), Allan Kijazi, amewataka wapagazi wanaosaidia kubeba mizigo ya
watalii kwenye Mlima Kilimanjaro kuhakikisha wanatunza mazingira ya
mlima huo kwani ukiharibika na wao wataathirika kwa kukosa ajira.
Aidha, alisema atawasiliana na wadau wa
utalii ili kuona namna ya kuboresha utendaji wao kwa kuwatafutia ziara ya
mafunzo kwenye moja ya nchi zenye milima mirefu.
Aliyasema hayo jana wakati akifungua kongamano
la kwanza la Chama Cha Wapagazi nchini (TPO) lililofanyika kwenye ukumbi wa
YMCA ambalo lilikuwa likijadili changamoto wanazokabiliana nazo na namna ya
kuzitatua.
Kijazi alisema kuwa kwenye kongamano lao
hilo mbali ya kujadili changamoto zinazowakabili ni vema wakaangalia namna
ya kuutunza mlima huo ambao unawapatia ajira.
“Kuna malalamiko yanakuja kuwa wakati
mwingine nyie mnaacha taka huko mlimani kwa kushindwa kuzikusanya vizuri,
ni vema mkautunza mlima huu kwani ukipoteza sifa na hadhi yake wageni
wataacha kuja na nyie mtakosa ajira,” alisisitiza mkurugenzi mkuu huyo wa
Tanapa.
Aliwataka viongozi wa TPO kujenga mfumo wa
kufuatilia mienendo ya wanachama wao ili kuona kama wanafuata taratibu na
maadili waliyojiwekea, kwani kuna wakati yanaibuka malalamiko kuwa kuna
baadhi ya wapagazi si waaminifu na wengine hawazingatii uvaaji sahihi,
jambo linalohatarisha usalama wa afya zao.
Kijazi alisema kuwa anaangalia uwezekano
wa kukutana na wadau wa utalii wanaoendesha shughuli kwenye mlima huo
wakiwemo Chama cha Waongoza Watalii kwenye mlima huo, KIATO, na Wizara ya
Maliasili na Utalii ili waweze kuona namna sheria zilizowekwa hasa kwenye
udhibiti wa uzito wa mizigo zitakavyosimamiwa kwa ukaribu zaidi.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Bodi ya
Ushauri, TPO, Richard Kessy, alisema changamoto kubwa zinazowakabili
wapagazi ni kampuni za uwakala wa utalii kubebeshwa mizigo mizito
zaidi ya kiwango kilichowekwa na Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA)
ambacho ni kilogramu 20.
“Wapagazi wakiwa huko mlimani kuna wengine
wanapewa chakula mara moja kwa siku, wengine wanapewa mara mbili lakini
kidogo sana ukinganisha na kazi ngumu ya kubeba mizigo yao na ya watalii
wanayoifanya,” alisema Kessy.
Naye Mwenyekiti wa TPO, Philip Mbise,
alisema kuwa wana wanachama 2,820, ambapo kongamano hilo la siku moja
limehudhuriwa na wapagazi 250 kutoka mikoa ya Kilimanjaro na Arusha.
|