Na Fredy Azzah, Mwananchi
Posted Novemba2 2013
Posted Novemba2 2013
Kwa ufupi
- Baadhi ya wadau hao
wakizungumza na gazeti hili jana, walisema Tanzania imeweka rekodi kwa
nchi za Afrika kwa kuwa na kiwango kidogo sana cha ufaulu cha alama F
kuanzia 0 mpaka 19.
Dar es Salaam. Siku moja baada ya Serikali kutangaza kupunguza viwango vya ufaulu kwa
mtihani ya kidato cha nne na sita, baadhi ya wasomi na wadau wa elimu wameponda
uamuzi huo na kusema una malengo ya kisiasa.
Baadhi ya wadau hao wakizungumza na gazeti hili jana, walisema Tanzania
imeweka rekodi kwa nchi za Afrika kwa kuwa na kiwango kidogo sana cha ufaulu
cha alama F kuanzia 0 mpaka 19.
Walisema, Serikali imechukua uamuzi huo kisiasa ili kuhakikisha kuwa,
wanatimiza lengo la Mpango wa Maendeleo Makubwa Sasa (BRN), ambalo ni
kuhakikisha matokeo ya ufaulu kwa Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka huu yanafikia
asilimia 60 kutoka 33 ya mwaka jana.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Herme Mosha
alisema kuwa kilichofanywa na Serikali ni kupanua wigo wa watu kufaulu.
“Wanataka watu ambao walikuwa wanapata daraja la nne wapate daraja la
tatu, daraja la tatu wapate la pili na la pili wapate la kwanza.
Hata hivyo, kwa muda wote, wadau wa elimu ambao wanataka siyo kuona tu
watu wanafaulu, wanataka elimu iliyo bora. Kwa hatua hii waliyoichukua
haitasaidia lolote katika kuongeza ubora wa elimu ambao umekuwa kilio cha muda
mrefu,” alisema Profesa Mosha.
Alisema kuwa, washikadau wengi wangependa kuona ubora wa elimu
umeongezeka na siyo kuongeza wigo wa ufaulu.
“Huku ni kujidanganya, jambo la kwanza wangetakiwa waende katika shule
mbalimbali waone ni nini walimu wanataka, tatizo lipo wapi halafu wachukue
hatua kwa sababu ukiangalia sasa ni kama kuna mgomo fulani hivi,” alisema.
Kwa upande wake Dk Kitila Mkumbo ambaye ni Mkuu wa Idara ya Saikolojia
ya Elimu na Masomo ya Mitalaa ya Shule Kuu ya Elimu katika Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam, alisema tatizo la elimu Tanzania halijawahi kuwa ni viwango vya
ufaulu.
“Wanataka tu kuona hiyo asilimia 60 waliyojipangia inafikiwa.
Walijiwekea lengo hilo wakijua kabisa kwenye elimu hakuna miujiza, lazima mtu
ufanye kazi ndiyo matokeo yaonekane,” alisema.
Alisema kiwango cha kufeli kilichowekwa kinaifanya Tanzania kuwa nchi
yenye viwango vidogo sana vya elimu kwenye bara hili.
“Burundi wenyewe mtoto akipata 50 ndiyo anakuwa amefeli, sisi huku
tumeweka mpaka 19 ndiyo tunasema amepata hiyo F, lakini bado tunaita amefaulu,
huu ni utani,” alisema.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT),
Ezekia Oluoch alisema Matumizi ya Alama za Maendeleo ya Mwanafunzi (CA) ni
suala la kupongeza.
Hata hivyo, alisema kuwa kuna matatizo ya msingi kwenye elimu na ni
lazima yafanyiwe kazi.
“Lengo lao la kushusha ufaulu ni ili ionekane kuwa BRN imefikia lengo,
watoto wamefaulu ndiyo iwe furaha yao,” alisema.
Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi Tanzania
(TAMONGSCO), Mahmoud Mringo alisema wamepokea suala hilo kwa mikono miwili.
“Zamani mtu alikuwa amapata sifuri na mwingine 33 wote tunasema wamepata
F, lakini sasa kuna utofauti kwa hiyo unaweza kuona ni namna gani uwatumie hawa
watu.
Pia suala hili linatoa mwanya mpana hata kwa Serikali na taasisi
nyingine za elimu, ikitokea kwamba watu wa C wamekosekana unaweza kuona sasa
tutumie wapi,” alisema.
Alisema kuwa, kwa sasa sera ya elimu inasema watu watakaoingia kidato
cha tano wanatakiwa wawe na C tatu, lakini mwaka huu Serikali ilichukua C moja
na D mbili wakaenda kidato cha tano.
“Yote hii ni kwa sababu hakukuwa na njia mbadala, lakini kwa sasa
kutakuwa na mianya mingi sana.
Hata hivyo, tujue kuwa, tatizo la elimu Tanzania halikuwa madaraja, hii
ilikuwa ni sehemu tu, lazima tuhakikishe tunatafuta matatizo ya msingi ya elimu
yetu tuyafanyie kazi. Tukibaki kwenye hizi alama, basi nchi yetu itakwenda
shimoni,” alisema.