Subscribe:

Ads 468x60px

kituo cha utalii cha seronera watalii wakipata maelezo mbalimbali ya vivutio vilivyomo ndani ya hifadhi ya taifa ya serengeti

wafanyakazi wa World Vision kutoka mikoa mbalimbali wakiwa kwenye utalii wa ndani katika hifadhi ya taifa ya serengeti,hata hivyo basi lao la kampuni ya Mohammed Trans nusura lianguke baada ya kushindwa kukata kona

hapo ni kituo cha utalii seronera

pigia kura hifadhi ya taifa ya serengeti,bonde la Ngorongoro na Mlima Kilimanjaro

nyumbu wakirejea hifadhi ya taifa ya serengeti ambako ni kwao,wakitokea masai mara

pigia kura vivutio vya Tanzania ambavyo ni hifadhiya Taifa ya Serengeti yenye nyumbu wanaohama,bonde la Ngorongoro ambalo wanyama wafugwao,wanyama pori na wananchi wanaishi pamoja na mlima kilimanjaro ambao barafu yake haiyeyuki hata pawe na joto,andika vote@sevennaturalwonders.org

wanaharakati watakiwa kuandamana kupinga mauaji ya wananchi mgodi wa nyamongo


WANAHARAKATI WATAKIWA KUANDAMANA KUPINGA MAUAJI NYAMONGO.
Na Anthony Mayunga-Nyamongo.
Septemba 11,2012.

SIKU moja tu baada ya polisi kujeruhi watu 6 kwa mabomu ya machozi wakiwa majumbani kwaoWanaharakati na mashirika ya  kiraia wilayani Tarime wameombwa  kufanya maandamano ya hiari kupinga mauaji na vitendo vya kikatili vinavyofanywa na askari polisi wanaolinda mgodi wa African Barrick Gold North Mara.

Wito huo wakati waandishi wa habari hapa Tanzania wakiandamana kimya kimya kulaani mauaji ya kikatili ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa Channel ten mjini Iringa katika kijiji cha Nyololo na raia wasiokuwa na hatia yanayofanywa na polisi.

Mtafiti kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu(LHRC)Onesmo Ole ngurumwa akiongea na gazeti hili alisema zaidi ya watu 30 wameuawa na jeshi la polisi katika mgodi wa African Barrick North Mara kwa kipindi cha kuanzia 2009-sasa.

“Matukio hayakomi kila wakati wananchi wanauawa ,inabidi wanaharakati na mashirika ya kiraia mkoani Mara kuunganisha nguvu na kufanya maandamano ya amani ili kupinga mauaji na ukatili wanaofanyiwa wananchi hao ambao hawajawekewa mazingira mazuri”alisema.

Ole ngurumwa ambaye ni mfuatiliaji wa karibu wa mauaji yanayotokea Nyamongo alisema kwa kipindi cha mwaka 2009 watu 21waliuliwa  na polisi ama na walinzi wa mgodi huo.


Na kuwa mauaji yanaongezeka kila mwaka hivyo inatakiwa wanaharakati na mashirika ya kiraia kujitokeza ili kupinga ukatili huo.

“Kabla hawajauza ama kukodisha mgodi huo vitendo hivyo vinatakiwa kukomeshwa kwa kuwa ikiachwa watawarithisha wawekezaji wengine,tulaani vitendo hivyo”alisema.

Akizungumzia ulipuaji wa mabomu hadi kwenye makazi ya watu alisema ni utendaji mbovu wa jeshi hilo kwa kuwa hali hiyo ikiachwa iendelee madhara yanazidi kuwa makubwa.

Alibainisha kuwa serikali ni chanzo kwa kuwa imeunda vikundi vya wachimbaji wadogo lakini hawakuwahi kusaidiwa zaidi ya kuahidiwa kila kukicha.

Ushirika wa wachimbaji walia na ahadi hewa.
Mwenyekiti wa Ushirika wa wachimbaji wadogo Tarime Daud Makona alisema licha ya kusajiri ushirika wao mwaka 2010 hawajawahi kupata msaada wowote toka wizara ya Nishati na madini.

“Mauaji yanayoendelea Nyamongo yana mkono wa serikali,maana kama wangekuwa wametuwezesha wachimbaji o kusababisha vifo,naibu waziri Masele alikuja akaahidi,Waziri Profesa Sospeter Muhongo ameelezwa,hakuna kitu”alisema kwa uchungu.

Wakati analalamika serikali kutowasaidia Waziri Mkuu Mizengo Pinda ziarani Geita katika mgodi wa Mugusu alihimiza uundaji wa ushirika wa wachimbaji wadogo kuwa watasaidiwa na serikali.

Mtandao wa mashirika kukutana kutoa tamko.
Mratibu wa mtandao wa mashirika yasiyo ya kiserikali Tarime(Tangonet)Bonny Matto alisema wanakutana kesho(leo)na moja ya agenda ni kutoa tamko juu ya mauaji na ukatili unaoendelea wilayani hapo.

Wakati huo huo habari zinadai kuwa majeruhi wa mabomu yanayodaiwa kurushwa na polisi wakati wanawafukuza vijana wanaodaiwa kuvamia kifusi hali zao zinaendelea vizuri.

Mwisho.



polisi wajeruhi watu 6 kwa mabomu wakiwa majumbani nyamongo


POLISI NYAMONGO WAJERUHI SITA KWA MABOMU WAKIWA MAJUMBANI KWAO.
Na Anthony Mayunga-Nyamongo.
Septemba 10,2012.

ASKARI  wa mkoa wa Kipolisi Tarime na Rorya wanadaiwa kujeruhi watu 6 wakazi wa kitongoji cha Nyabikondo kijiji cha Kewanja kwa kuwapiga mabomu wakiwa majumbani na kazini wakati wanawatanya  wavamizi wa kifusi cha mawe mgodini.

Tukio hilo limetokea septemba 9 ,majira ya saa 6 mchana mwaka huu katika kitongoji hicho,limethibitishwa na uongozi wa kitongoji na kijiji hicho,huku kamanda wa polisi mkoa akikwepa kulizungumzia kwa madai kuwa hakuwa na taarifa.

Ulipuaji mabomu na kuleta madhara kumetokea wakati taifa likizizima kuhusiana na mauaji yaliyofanywa na jeshi hilo kwa aliyekuwa mwakilishi wa Channel Ten mkoani Iringa Daud Mwangosi septemba 2 katika kijiji cha Nyololo wakati Chadema wanafungua matawi yao.

Waliojeruhiwa wametajwa kuwa ni Suzana Mwita Gibaye (28)ambaye aliumizwa kichwani na mguu wa kushoto,Ghati Marwa ambaye ni mjamzito ambaye habari zinadai kuwa amelazwa katika hospitali ya wilaya ya Tarime.

Wengine ni Esther  Chacha(12) Chacha Chacha(10) na Daniel Chacha(6) na mama yao Marwa Chacha ambao wamepanga kwa  Magaiwa Ngewa wanadaiwa  walipigwa  mabomu na kuumizwa wakiwa nyumbani kwao ambako anaendesha biashara ya mgahawa.
Majeruhi.

Mmoja wa majeruhi  Suzana akiongea na gazeti hili kwa njia ya simu  muda mfupi baada ya kutoka zahanati ya kampuni ya African Barrick North Mara kutibiwa alikopelekwa na askari polisi wa kituo cha Nyamomngo kuwa walipigwa wakiwa wanaendelea na kazi kwenye mgahawa wa Magaiwa.

“Tukiwa tunaendelea na kazi kwenye eneo la Mrwambe tuliona polisi wanafukuzana na vijana(Intruda) waliovamia kifusi kilichomwagwa nje na mgodi huku wanapiga mabomu ,lakwanza na la pili hayakutufikia wakapiga la tatu nikastukia napigwa kichwani na kitu na mguu wa kushoto damu zikaanza kuvuja nikaanguka huko”alisema.

Na kuwa mbali na yeye mama huyo na wanae wote wakawa wamejeruhiwa vibaya ,na polisi wakaendelea kupiga ovyo ovyo hali iliyopelekea kumwaumiza wananchi wengine wakiwa majumbani.

“Lilifika gari la pili la polisi afisa mmoja wakawachukua watoto na mama yao mimi nilikuwa nimeanguka kwa chini hawakuniona ,wakawapeleka zahanati ya mgodi ,mimi nilichukuliwa na boda hadi hospitali ya Sungusungu wakaniambia niwape Pf 3,kurudi polisi wakanipeleka zahanati ya mgodi”alidai.

Na alifungwa bendeji kichwani na mguuni na dawa kisha akarudishwa polisi na kusaini maelezo na kuambiwa arudi nyumbani akizidiwa arudi polisi,maelezo ambayo pia walipewa mama na watoto wake.

Mwenyekiti wa kitongoji.

Charles Vicent mwenyekiti wa kitongoji hicho alisema tukio hilo lilitokea wakati wakiwa kwenye kikao cha usuluhishi kati ya koo ya Nyabasi na Wanyamongo baada ya kutokea kutoelewana kilichohusisha Kamanda wa polisi wilaya aliyemtaja kwa jina la Saimoni,wazee na mila na viongozi wa maeneo husika.

“Tukiwa kwenye kikao mpakani mwa Kewanja na Nyakunguru ndipo pakatokea matukio hayo ambayo yalimlazimu Ocd kukimbilia eneo la tukio na kuwachukua wale watoto na mama yao na kuwapeleka mgodini wakafungiwa bendeji kisha wametelekezwa bila msaada wowote na inasemekana gololi ziliwaumiza kichwani na vifuani ”alisema.

Alidai kuwa askari polisi waliokuwa juu wakijua chini kuna makazi ya watu  walifyatua mabomu na kuelekeza majumbani na kuwa hili ni tukio la pili kupiga na kujeruhiwa watu wakiwa majumbani na shuleni.

Hata hivyo mama aliyejeruhiwa na wanae inasemekana baada ya kutoka zahanati ya mgodi kutibiwa inadaiwa aliondoka na wanae wala haijulikani alipo ,lakini habari kutoka kwa majilani zake zinadai kuwa huenda ameenda kwao kijiji cha Magoto kwa ajili ya matibabu zaidi na kuwa huenda walitishwa na polisi akaogopa.

Mwenyekiti wa serikali ya kijiji.
Akiongea na gazeti hili kwa njia ya simu Mwenyekiti wa serikali ya kijiji aliyejitambulisha kwa jina la Tanzania O’mtima alisema mmoja wa majeruhi ambaye ni mjamzito ambaye alipigwa akiwa nyumbani kwake inasemekana amepelekwa hospitali ya wilaya ya Tarime kwa matibabu zaidi.

Maelezo yake yanadhihirishwa na juhudi za baadhi ya mashuhuda walioongea na gazeti hili ,ambao walikwenda hospitali ya Sungusungu na hawakumkuta na hata walipofuatilia nyumbani kwake waliambiwa toka alipochukuliwa siku ya tukio hajarudi nyumbani.

Mgodi.
Mmoja wa maafisa wa mahusiano wa kampuni ya African Barrick North Mara Shayo Simion alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa watu wanaohudumiwa na zahanati yao,alidai ni kwa ajili ya watumishi.

“Kama tumekuta mtu ameumia sisi hutoa msaada wa matibabu lakini kwa ajili ya majeruhi kama hao wanapaswa kupelekwa hospitali ya serikali,hilo wasiliana na kamanda kwa kuwa halituhusu”alisema.

RPC.
Kamanda wa mkoa huo wa kipolisi Justus Kamugisha alipoulizwa kuhusiana na kujeruhi watu kwa mabomu wakiwa majumbani alidai hakuwa na taarifa ya watu kuumizwa na mabomu ila vurugu za wananchi na askari.

“Vurugu ni kila siku tena leo wamepiga sana gari letu kwa mawe,hapajatokea utulivu eneo hilo ,maana watu wanajitokeza kwa wingi kutufanyia vurugu,hapa lazima maamzi magumu yachukuliwe ama kuondoa wananchi karibu na mgodi ama kampuni kutoka wachimbe kama zamani maana mgodi uko kwenye makazi ya watu ni hatari zaidi”alisema kamanda.

Baadhi ya mashuhuda wanadai kuwa wananchi walilazimika kushambulia magari ya polisi kwa kile walichodai matumizi ya nguvu ni makubwa ambayo yanasababisha madhara hata kwa wasiohusika.

Juhudi za kujua hali ya Ghati ambaye ni mjamzito alikolazwa na hali yake  zinaendelea baada ya kuwepo na usiri mkubwa ,ikizingatiwa kuwa hata majeruhi walipelekwa na polisi kutibiwa mgodini badala ya hospitali ya serikali ili kuficha taarifa.

Mwisho.



ukosefu wa maji safi na salama kwa wakazi wa nyamongo wananchi walia na serikali na mgodi



UKOSEFU WA MAJI NYAMONGO WANANCHI WAZIDI KUIKABA KOO HALMASHAURI.
Na Anthony Mayunga-Nyamongo.
Septemba 6,2012.

HALMASHAURI ya Wilaya ya Tarime na Kampuni ya African Barrick North Mara wameendelea kulaumiwa na wananchi kwa kushindwa kutatua tatizo la maji safi na salama kwa wakazi wa Nyamongo.

Mapema wiki hii gazeti hili lilifanya uchunguzi katika vijiji vinavyozunguka mgodi huo ili kubaini  wa utekelezaji wa ahadi za serikali kwa wakazi wa maeneo yanayozunguka mgodi huo baada ya chanzo cha mto Tighite kuharibiwa na sumu toka mgodi wa Gokona unaomilikiwa na kampuni ya African Barrick North Mara.

Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Kewanja Tanzania O’mtima ameliambia blogu  hii kuwa tatizo la maji safi na salama ni kubwa kwa wakazi wa kijiji chake kwa kuwa serikali imeshindwa kutimiza ahadi zake kwa wakati.

“Visima vimechimbwa na kutelekezwa havitoi maji,badala yake kampuni inatum,ia gari kusambaza maji ambayo serikali haijawahi kutuambia kama wameyapima na kubaini ni safi na salama ,kwa kuwa kampuni inadai yanatoka mgodini”alisema.

Alisema baadhi ya maeneo magari hayafiki kutokana na ubovu wa barabara hivyo wananchi wanapata shida kubwa kupata maji “hakuna nafuu yoyote maana tungekuwa na maji ya bomba tungesema limetatuliwa si kama ilivyo kwa kuletewa na gari maeneo mengine halifiki”alisema O’Mtima.

Alikwenda mbali na kudai kuwa viongozi wa serikali wamebaki kuzungumzia kwenye majukwaa wakati hakuna utekelezaji wowote ya maagizo ya toka mwaka 2009.

Hata alibainisha kuwa wamefunga mkataba na mgodi kuhakikisha kila mwaka wanawachimbia visima virefu viwili na wameanza mwaka huu ambapo yeye katika kitongoji cha Magina ambacho kina hali mbaya zaidi wamechimbiwa visima viwili.
Afisa maji.
Afisa maji wilaya ya Tarime Madaraka Mahando alikiri halmashauri kuchimba visima lakini havijatumika kwa kukosa maji huku akirusha lawama kwa jamii kuwa iliviharibu kabla ya kutumika.

“Kuna tatizo la kisiasa maana wananchi baadhi ya maeneo walikata  na kudumbukiza udongo,taarifa zipo mpaka wizarani,na Mkurugenzi baada ya kuwa umefuatilia amesema akitoka safari naye anataka tuzunguke naye kubaini vingapi havifanyi kazi”alisema.

Alivitaja visima walivyochimba kuwa ni vinne “vile vya Task Force kama serikali ilivyoelekeza tumechimba Matongo viwili,Kewanja 1 na Nyakunguru kitongoji cha Itandura kimoja lakini baadhi havifanyi kazi”alisema.

Hata hivyo alishindwa kuthibitisha kama maji yanayosambazwa kwa gari na kampuni ni safi na salama na yamepimwa na mamlaka gani.

Kampuni.
Mmoja wa maafisa katika mgodi wa North Mara upande wa maji Saimoni Shayo alikiri kusambaza maji kwa gari kutokana na kuwa maeneo mengi hayana maji kwa kuwa hakuna visima.

“Tunawasambazia maji ambayo tunatumia sisi ,wakati wa usiku kwa kuwa hatuyatumii ndipo tunachota kuwapelekea hata hivyo hayatoshi ,tuna mpango wa kuchimba visima viwili viwili kila kijiji kwa kila mwaka”alisema.

Alidai kuwa mpango mwingine ni kutandaza mabomba ambao unategemea kukamilika mwaka 2014,kuhusu visima vingi kutokuwa na maji “si kwamba kote hakuna maji kwingine kuna madini tembo ambayo hayafai kwa matumizi hiyo ni kitaalam si kwamba mgodi ndio umeharibu”alisema.

Hata hivyo alipingana na halmashauri na kauli za serikali kutoa maagizo kwa kampuni kuhakikisha wanawapatia vyanzo mbadala vya maji baada yamto Tighite kuchafuliwa na sumu kutoka mgodini kwa madai kuwa hawana waraka wowote wa serikali wa kuwataka kufanya hivyo.

Mwisho.

posho ya sensa ya tsh,15,000=yakataliwa na wenyeviti wa vitongoji Tarime


WENYEVITI WAKATAA POSHO YA SENSA TSH,15,000=,

Makarani wahofu kukabidhi madodoso mpaka walipwe,
Na Anthony Mayunga-Mara.
Septemba 5,2012.


WAKATI zoezi la Sensa likiongezewa siku hadi tarehe 8,viongozi wa vitongoji wilayani Tarime wamekataa kupokea malipo ya tsh,15,000 kwa  siku zote za kazi hiyo.

Hali hiyo inatokana na kutofautiana kwa Malipo hayo kwa kila wilaya ndani ya mkoa mmoja ,licha ya wote kudai waraka kutoka ofisi ya mkoa.

Baadhi ya wenyeviti wa vitongoji wilayani humo ambao hawakupenda kutaja majina yao waliliambia gazeti hili kuwa hawako tayari kulipwa kiasi hicho kwa kazi hiyo waliyoifanya.

“Tumezoea kutumiwa kama watu tusiokuwa na majukumu ya kifamilia,toka utekelezaji wa miradi hadi sensa,yaani unalipwa tshs  15,kwa siku 7 wastani wa tsh,2,000= kwa siku ambazo hazitoshi hata mlo wa mchana,hii ni dharau kubwa sana”alisema mmoja wao.

Walidai kuwa walilazimika kuacha shughuli za kilimo na kushinda wakizunguka na makarani ambao walikuwa wakipwa tsh,35,000= kwa siku, na kuwa wameamua kuziacha ili serikali ifaidike.

“Wengine kwa kazi hizi hizi walilipwa tsh,50,000= wilayani Serengeti,Bunda tunasikia walilipwa tsh,20,000= sisi tsh,15,000= mkoa huo huo kuna kitu kinaendelea maana hata fedha ya uhamasishaji watu wamekula sisi ndio tulifanya kazi ya hamasa na kushawishi wananchi”walisema .

Walisema hata posho kwa mwezi wenyeviti wa vijiji kwa wilaya hiyo wanalipwa tsh,5,000= kwa mwezi licha ya kuwa wanakabiliwa na kazi nyingi za kuhamasisha maendeleo.

Mratibu wa sensa wilaya hiyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Juma alikiri wenyeviti kukataa fedha hizo kwa madai kuwa ni kidogo.

“Ni kweli wamekataa tunaendelea kushughulikia ili waweze kuchukua kwa kuwa hawakuwemo kwenye hesabu,waliokuwa wanatajwa ni wenyeviti wa mitaa,watendaji wa vijiji na kata ,hivyo sisi hatuna mitaa tukawaingiza wenyeviti”alisema.
Alisema kuwa katika utafiti wake alibaini kuwa wilaya hiyo inalipa kiasi kikubwa ikilinganisha na Rorya na Serengeti ,hata hivyo wilaya ya Serengeti walilipa tsh,50,000 kama ilivyokuwa imeelekezwa awali,lakini mkoa ukabadilisha viwango.

Kwa wilaya ya Rorya wenyeviti wa vitongoji walilipwa tsh,10,000= kama mkoa ulivyoelekzwa,hata hivyo hawakushiriki zoezi hali iliyopelekea makarani kuzunguka wenyewe.

Katibu tawala mkoa wa Mara Clement Lujaji akizungumzia suala la malipo ya wenyeviti wa vitongoji alisema waraka ulisambazwa kwa waratibu wote kutokana na kuwa hawakuwemo kwenye mchakato na kuwa halmashauri zilikuwa na nafasi ya kuwalipa zaidi ya hapo kulingana na mapato yao.

Blogu hii imebaini kuwa baadhi ya makarani hawakuweza kuendelea na zoezi la sensa licha ya kuongeza siku kwa kile kinachodaiwa kuwa maelekezo hayo hayafafanuliwi jinsi watakavyolipwa.

Na kuwa walilipwa nusu ya posho na hawajalipwa nusu iliyosalia ,hata madodoso  hata waliokamilisja hawajakabidhi kwa kuwa hawajalipwa,na wanahofu kukabidhi bila kulipwa fedha zao hali .

Mwisho.